Mfanyabiashara ashikiliwa kwa kutishia kuuwa wafanyakazi wa kampuni ya ukandarasi ya Hema Tec mkoani Rukwa.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida mfanyabiashara mmoja wa maeneo ya mazwi
kwenye manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, amewatishia kuwapiga risasi
wafanyakazi wa kampuni ya ukandarasi ya Hema Tec, inayotekeleza mradi wa
kuchimba mtaro wa kupitishia mkongo wa taifa wa mawasiliano mjini humo,
kwa kukataa kutii amri yake ya kuwakataza kuchimba kwenye eneo lake, na
wafanyakazi hao kutimua mbio kunusuru maisha yao.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Rukwa kamishna msaidizi wa
polisi Lewins Rwegasira, amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo ambaye
amemtaja kuwa Juma Mussa mkazi wa maeneo ya mazwi, kwa tuhuma za
kutishia kuuwa kwa bastola aina ya Browning yenye namba a 729321, na
kuwakimbiza wafanyakazi wa kampuni hiyo ya Hema Tec kwa gari lake, ambao
waliamua kukimbia baada ya kuona ameingia ndani na kutoka na bastola
hiyo.
Akiongea na ITV msemaji wa kampuni hiyo ya ukandarasi ya Hema Tec
Bw Abdallah Seleman, amesema mtuhumiwa huyo kwanza aliwakataza
wafanyakazi hao wasichimbe mtaro kwenye eneo hilo, lakini wao
wakawaambia waendelee na kazi kwani wanaitekeleza kwa mujibu wa ramani
iliyotolewa na manispaa ya Sumbawanga, na ndipo alipoamua kuchukua
bastola yake baada ya kuona ameshindwa kupambana na mmojawao aliyemtaja
kwa jina la Daud William.