Wanafunzi wa ualimu, sayansi walalamika kukosa mikopo


Wednesday Dec 3, 2014

3rd December 2014
Waziri wa Elimu na Mafunzo na Ufundi, Dk.Shukuru kawambwa.
Licha ya  Serikali kutangaza kutoa mikopo asilimia 100 kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi na ualimu, ahadi hiyo imeyeyuka na wanafunzi hao wanalalamika kukosa fedha hizo.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika vyuo mbalimbali umebaini kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi hao wamekosa mikopo na hata wengine kupelekea kusitisha masomo yao.

Mwanafunzi wa mwaka wa pili  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayechukua masomo ya ualimu, Danford Damian, alisema  ni mbaya chuoni hapo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutokana na wengi wao kutopata mikopo, na kulazimika kutafuta kazi za kufanya ili kupata fedha za kujikimu.

Alisema Serikali iliweka utaratibu kwa walimu wa masomo ya sayansi kupata mkopo bila kuangalia kigezo chochote, ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wa elimu ya juu kujiunga na masomo ya sayansi.

“Kipindi  ambacho mimi naingia chuo miaka mitatu iliyopita, hatukupata shida ya kupata mikopo kutokana na kipaumbele ambacho Serikali iliweka kwa walimu wa masomo ya sayansi, lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti sana wanafunzi wengi wamekosa mikopo,” alisema 

Mwanafunzi mwingine wa UDSM, Rahima Moshi, anayesomea ualimu alisema zaidi ya wanafunzi 60 wanaosoma kozi ya ualimu wamekosa mkopo mwaka huu.

Alisema wengi wao walipewa maelezo kutoka Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwa bajeti imebana.

Aliongeza kuwa baada ya kulalamika kwa HESLB waliambiwa waombe kwa mara ya pili, na waliomba maombi mapya Agosti, mwaka huu.

Alisema hadi Novemba mwaka huu, maombi yao ya mara ya pili yalikuwa hayajajibiwa.

Naye mwanafunzi kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM ), Scolastica  Ndahani  alisema wanafunzi wengi katika chuo hicho  hawajapata mikopo kitu ambacho kinasababisha baadhi yao kushindwa kumudu maisha ya chuo.

Alisema baada ya kufatilia HESLB walimwambia aombe kwa mara ya pili ambapo alijaza upya fomu hiyo Agosti mwaka huu.

Baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamelalamika kutopata mkopo hadi hivi sasa licha kuchaguliwa kusomea ualimu.

Agness Gregory alisema baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaochukua shahada ya elimu kama hawajapata mikopo. “Kuna kozi zingine za elimu hawajapewa mkopo ila wameamua kukata rufani kwa wale ambao hawajaridhika na baadhi ya wanafunzi wameamua kukata rufaa,”  alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi wanaosoma udaktari na uhandisi chuoni hapo wamepatiwa mkopo.

Mwanafunzi katika chuo kikuu cha Iringa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini ambaye yupo mwaka wa pili anayechukua masomo ya ualimu, alisema walipokuwa mawaka wa kwanza walipata mikopo, lakini walipo fika mwaka wa pili na watatu kuna kiasi ambacho kinakatwa na HESLB, lakini walipo uliza uongozi wa chuo ili kupatiwa ufafanuzi walikuwa wakizungushwa bila kupatiwa majibu ya uhakika.

“Tunashangazwa sana na utaratibu ambao hautendi haki kwetu kwani mwanafunzi anayelipiwa na HESLB milioni moja wanakatwa, laki tatu huku wanaolipiwa laki tisa wakatwa laki mbili na wanaolipiwa laki sita wanakatwa laki moja, na tunapouliza kuhusu makato hayo hatupatiwi majibu ya kueleweka ,” alisema 

Waziri wa mikopo Chuo Kikuu Kishiriki (DUCE) cha UDSM, Yohana Lulyeho, alisema, HESLB iliwaambia wanafunzi waliokosa mikopo waombe upya, kwa kuwa walilemewa na bajeti.
Happy Silas, mwanafunzi wa ualimu mwaka wa kwanza katika chuo hicho, alisema aliomba, lakini hakupata mkopo, lakini alipofungua tovuti ya HESLB hakukuta jina  na kwamba hivyo ina maana kuwa anasoma bila mkopo.

Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta  Mkurugenzi Msaidizi wa HESLB, Cosmas Mwaisoba, kwa ajili ya kutolea ufafanuzi malalamiko hayo, alisema kuwa bajeti kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi ilikuwa finyu na kwamba imesababisha wanafunzi  8,000 kukosa mikopo.

Alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliahidi kuwa Serikali bado inatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wote waliokosa wanapata mikopo, hivyo wanasubiri ahadi hiyo ili waweze kutoa mikopo.

Imeandikwa na Frank Monyo , Enles Mbegalo, Gwamaka Alipipi, Christina Mwakangale na Adela Josephat.
CHANZO: NIPASHE
Powered by Blogger.