Wamiliki wa viwanda na
kampuni nchini wameshauriwa kuwasiliana na Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia Mbeya (Must) kama wanahitaji mafundi mchundo na wahandisi ili
waweze kuwapata vijana wenye elimu sahihi.Naibu makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Osmund
Kaunde alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa
viwanda, taasisi na kampuni zilizoko mkoani hapa katika kikao maalumu
kilichoandaliwa kwa ajili ya kuelezea umuhimu wa ushirikiano kati ya
waajiri na vyuo vikuu nchini.
Profesa Kaunde alisema chuo chake kimeanzisha
tovuti ambayo waajiri wanaweza kutangaza mahitaji ya watalaamu
wanaowataka na tovuti hiyo itatoa fursa kwa wahitimu wenye sifa kuomba
kazi.
“Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
Tanzania na nchi ya Italia na unahusisha vyuo vitatu vya Must, Taasisi
ya Ufundi Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC),” alisema.
Meneja wa mradi huo, Dk Danielle Pascallaqua
kutoka Italia alisema vyuo vya Must, DIT na ATC kwa sasa vimepata vifaa
vya kisasa vya kufundishia.
Naye mratibu wa kuhamasisha wasichana wasome
masomo ya ufundi na uhandisi wa Must, Dk Lusajo Minga alisema mpango huo
umeongeza idadi ya wasichana kutoka 11 mwaka 2005/06 hadi wasichana 269
kwa mwaka 2013/14.
Alisema wasichana hao wameonyesha umahiri katika
masomo ya ufundi mchundo na uhandisi na wana uwezo wa kufanya kazi kwa
ufanisi mahali popote duniani.