Krismasi ni Escrow kila kona
Krismasi ni Escrow kila kona
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk Alex
Malasusa akimbariki mtoto baada ya kumalizika kwa ibaada ya Krismasi
iliyofanyika katika Usharika wa Azania Front, Dar es Salaam jana. Picha
na Said Khamis.
Kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow inayoendelea kulitingisha Taifa, jana ilitawala mahubiri
Dar/mikoani. Kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow inayoendelea kulitingisha Taifa, jana ilitawala mahubiri
ya Sikukuu ya Krismasi katika makanisa mbalimbali nchini, viongozi wa
dini wakionyesha kutoridhishwa na maelezo na hatua zinazochukuliwa.
Wakihutubia waumini wao, viongozi hao walitumia siku hiyo kukemea vitendo vya ufisadi, wizi na uzembe.
Hofu ya Escrow
Ujumbe
wa Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) wa Kanisa la
Anglikana, Dk Dickson Chilongani ulilenga kueleza hofu ya wananchi
kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ugumu wa maisha, ukosefu
wa ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu na elimu pamoja na
wimbi la viongozi waandamizi wasiokuwa waaminifu na waadilifu.
Akihubiri
katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, Askofu Chilongani
alisema mbali na maisha ya ufukara na ukosefu wa huduma, sakata la
Escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Jumatatu vimezidi
kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya waonekane kama hawana
tumaini.
Akitumia mtindo wa kuhoji, Askofu Chilongani
alianza kwa kuhoji, “Kitu gani kinakutia hofu unaposherekea sikukuu hii,
watu wengi tunaishi katika ulimwengu wa hofu kutokana na ufukara,
ukosefu wa huduma, tunajiuliza tutawasomeshaje watoto wetu, tutapataje
huduma bora za matibabu, yaani kila mmoja wetu ana hofu,” alisema.
Askofu
Dk Chilongani alisema ingawa kila mtu ana hofu yake lakini sakata la
akaunti ya Escrow limejenga hofu kwa mwananchi, kila mmoja akihoji na
kutengeneza majibu yake jambo linalotoa picha kuwa jibu sahihi
halijatolewa au kupatikana.
“Mimi siyo mwanasiasa wala
mtaalamu wa masuala ya siasa lakini kuna hili sakata la Escrow ambalo
juzijuzi Rais amelitolea ufafanuzi, hili nalo linazidi kuwajengea
wananchi hofu, wengine wanakosoa maazimio ya Bunge, wengine wanataka
Serikali itoe maamuzi yenye tija kwa umma, yaani ni hofu tu,” alisema.
Escrow ni fedha za umma
Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo alisisitizia kuwa fedha
zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ni mali ya umma kutokana na
taarifa iliyowasilishwa na PAC bungeni.
Kauli hiyo
inakuja baada ya Rais Kikwete kusema fedha hizo ni mali Kampuni ya IPTL
na zilikuwa Sh202 bilioni na si Sh306 bilioni kama inavyodaiwa.
Akihubiri
katika kanisa hilo jana, Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema:
“Niliisikiliza kwa makini mwanzo hadi mwisho (hotuba ya Rais) leo
nimeona niseme machache kwamba fedha hizo ni mali ya umma. Mimi siungani
na hao wanaodai fedha hizi siyo za umma lakini kwa hali hii hakuna
jinsi inabidi tumwachie Mungu maana yeye ndiye atakayeweza kutuvusha
kutoka hapa tulipo,” alisema.
Padri: Viongozi wa dini waliotajwa wajipime
Paroko
wa Parokia ya Mugumu, Serengeti, Padri Aloisi Magabe amesema viongozi
wa dini ambao wametajwa kuhusika na fedha kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow wanatakiwa kujipima kwa kuwa maadhimisho ya Krismasi yana maana
kubwa, hivyo kuwa sehemu ya watu wanaotuhumiwa si jambo jema.
Akihutubia katika ibada ya Krismasi, Padri Magabe alisema vitendo hivyo vinazidi kushika kasi lakini hatua hazichukuliwi.
Alisema
ufisadi ulijichomoza kwa nguvu kwenye Richmond, Epa na sasa Escrow,
huku viongozi wa dini wakihusika, hatua ambayo ni hatari huku akisema
juhudi za kuwashughulikia wahusika huchukua muda mrefu, chanzo kikiwa ni
kulindana na rushwa. “Sina hofu ya kusema waziwazi matukio kama hayo,
nimefuatilia magazeti jinsi wanavyojitetea, bado kuna haja ya kuwa wazi
zaidi, maana nchi yetu ni ya haki na usawa, tutaupataje usawa kwa
‘skendo’ kama hizi?”
Askofu Mkude: Nina imani kubwa na JK
Askofu
wa Jimbo la Morogoro, Telesphol Mkude amesema ana imani kubwa na Rais
Kikwete kwa namna anavyolishughulikia suala la kuwajibisha waliotajwa
katika sakata la Tegeta Escow na kuwaomba Watanzania kumpa muda wa
kutosha ili aweze kuendelea kutoa uamuzi ulio sahihi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa katika ofisi ndogo ya Kanisa Kuu la
Mt Patrick, Mkude alisema suala la Escrow limepita katika mchakato mrefu
na baadhi ya wameanza kuchukuliwa hatua, wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu na Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyefukuzwa.
“Haya
mambo yanaenda na uchunguzi, sidhani kama Rais anaweza kutoa uamuzi
pasipo kujiridhisha, pamoja na kuwapo kamati iliyojiridhisha na
uchunguzi na kubaini uchotaji wa fedha za umma, lakini na yeye kwa
nafasi yake anapaswa kujiridhisha kupitia jopo lake,” alisema Askofu
Mkude.
Hofu ya Mungu na ufisadi
Hofu
ya Mungu imeelezwa kuwa ndiyo pekee itakayoondoa wizi na ufisadi
miongoni mwa viongozi na watendaji badala ya kutegemea sheria pekee.
Hayo
yalisemwa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa wakati akihubiri katika ibada ya
Krismasi katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam.
Kauli
hiyo inafanana na ile iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la
Gloryland International la jijini Tanga, Manase Maganga.
Malasusa alisema kutokuwapo kwa hofu ya Mungu miongoni mwa Watanzania, ndiyo sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya ufisadi.
“Wakristo
tunahitaji kusimama kwa ujasiri na kukemea mabaya yote katika jamii
yetu hata kama yanafanywa na marafiki zetu kwa kuwa neno linatuagiza
kufanya hivyo. Bwana anasema ‘woga ni dhambi’, hivyo tuwe makini ili
kuepuka dhambi hii yenye madhara kwa watu wengi katika Taifa hili,”
alisisitiza Dk Malasusa.
Vijana na siasa
Askofu
Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya akiwataka vijana kujitosa
kwenye siasa ili kuondoa giza nene ambalo limetawala katika nchi.
“Vijana
mliopo ndani humu leo, mshughulike na siasa kwa kuingia katika chama
ambacho mnaona kitachochea amani, utulivu, uvumilivu, ustahimilivu
miongoni mwa wafuasi wenu lakini siyo chama kinachowakumbatia mafisadi,
wabinafsi na wenye kujilimbikizia mali na kitakachosababisha chokochoko
yoyote ya kutoweka kwa amani,” alisema Askofu Chengula bila kutaja jina
la chama hicho.
Aliongeza: “Furaha imetoweka miongoni
mwa Watanzania na furaha tunayoizungumzia hapa siyo kunywa, kucheza na
kula, bali ni kuwa na amani, utulivu ndani ya mioyo yetu. Kutoweka kwa
amani si lazima watu wapigane vita na damu imwagike, hapana, hata wale
walioko maofisini wanaposhindwa kutimiza wajibu wao, mtu akabaki
akinung’unika moyoni mwake huo ndiyo mwanzo amani wa kutoweka.
Tatizo uongozi mbovu
Askofu
wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa amesema umaskini
unaolikabili Taifa kwa sasa unatokana na sera mbovu za nchi pamoja na
uongozi mbovu.
Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alitoa kauli hiyo katika
ibada ya Krismasi huku akisisitiza kuwa Taifa la Tanzania linao utajiri
mkubwa unaoweza kuwasaidia wananchi wake kuishi bila ya matatizo.
“Tanzania
siyo nchi maskini, bali kinachosababisha iwe hivyo ni sera mbovu
zilizopo na uongozi mbovu. Hivi kweli sisi hatuna mahali pa kuwahifadhi
watu wetu? Ardhi? (waumini wakajibu tunayo), madini? (tunayo) misitu?
(tunayo), mahindi? (tunayo), unawezaje kusema Taifa hili ni maskini?
“Mimi
nimekuwa nikishangaa na hata ninyi mmesikia haya mabilioni ya fedha
unayochukua mtu mmoja utakula hadi lini, umaskini tulionao unatokana na
mtu mmoja kula chakula kinachoweza kuliwa na watu zaidi ya milioni moja,
katika mazingira kama hayo ni lazima watu wengine wawe maskini,”
alisema.
Uchaguzi wa mitaa
Askofu
wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemuguzi aliwataka waumini wa
Kikristo na watu waliopewa nafasi za utendaji kuwa wavumilivu na
kuwajibika bila kuwakwaza wenzao.
Akihubiri katika
ibada ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mt. Francisco wa Asiz,
Parokia ya Ngara Mjini, juzi usiku, Askofu Niwemugizi aliwataka waumini
kutimiza wajibu wao wakitanguliza subira, kutokata tamaa na kuwa makini
kuzikabili changamoto za dunia.
Katika mahubiri hayo,
askofu huyo ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania
(TEC), alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika hivi karibuni,
haukufanyika vizuri kama ilivyotarajiwa, taratibu zilivurugwa na
tathmini yake inatia shaka.
Kutenda haki mwakani
Paroko
wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay Dar es Salaam, Padri Stephano
Kaombe aliwataka Watanzania kuacha woga wanapotekeleza majukumu yao na
kuhakikisha wanafanya mambo hayo kwa kiasi na haki.
Katika
mahubiri yake ya dakika 15 kwenye mkesha wa Krismasi kitaifa juzi
usiku, Padri Kaombe alisema waumini wanafunzwa kuwa watenda haki na
katika mwaka ujao ambao utakuwa na mambo mengi yanayohitaji kiasi na
haki.
“Tunapoalikwa kwenye daftari la wapigakura
tutende haki, katika kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa
tutende haki, tunapofanya uchaguzi napo tutende haki na tunaweza
kuyafanya hayo iwapo tutakuwa na kiasi na hatuna woga.”
Viongozi na amani
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe
amesema hatakuwa tayari kuhubiri amani inayoshinikizwa na viongozi wa
Serikali wakati wao ndiyo wanaoivuruga: “CCM imekuwa na hofu ya
kuondolewa madarakani, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulikuwa umejaa
ujanjaujanja na hata kuwafukuza wakurugenzi ni kiini macho.”
Mchungaji
Kiongozi wa Kanisa la Anglikana, St Albano, Aidano Mbulinyingi
akihubiri katika mkesha wa Krismasi aliwataka Watanzania kuwaombea
viongozi wa nchi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Tusiwe
na vinyongo, tukunjue mioyo yetu tuwaombee Rais, mawaziri na viongozi
wengine ili Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu,” alisema
Mbulinyingi na kusisitiza kuwa bila kuwaombea hawawezi kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza kwenye ibada ya misa
iliyoadhimishwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa alitoa wito
kwa jamii kusherehekea sikukuu hii kwa upendo na amani bila kuwasahau
watu wasiojiweza ili na wao wajisikie kuwa ni sehemu ya jamii.
Imeandikwa
na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge, Nuzulack Dausen, Julius Mathias,
Susan Mwilo, Bakari Kiango, Ibrahim Yamola, Kelvin Matandiko (Dar);
Burhani Yakub (Tanga); Godfrey Kahango (Mbeya); Shabaan Ndyamukama
(Ngara); Geofrey Nyang’oro (Iringa); Israel Mgussi (Dodoma); Anthony
Mayunga (Serengeti) na Juma Mtanda (Morogoro).