Polisi aliyejeruhiwa kwa bomu afanyiwa upasuaji wa mkono


Askari polisi WP. 8616 PC Mariam ambaye alijeruhiwa kwa bomu kwenye bega la mkono wa kushoto juziAskari WP 8616 Mariam,  akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma jana, baada ya kujeruhiwa na bomu la kienyeji la kurushwa kwa mkono lililotaka kurushwa kwa askari hao waliokuwa doria wakati wa sherehe za Krismasi eneo la Kotazi, mjini Songea juzi na kumuua mtu mmoja anayedaiwa kutaka kufanya shambulio hilo.  Picha ya Maktaba

Songea. Askari polisi WP. 8616 PC Mariam ambaye alijeruhiwa kwa bomu kwenye bega la mkono wa kushoto juzi baada ya mmoja ambaye jina lake bado alijafahamika, amefanyiwa upasuaji.
Mariam ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma amefanyiwa upasuaji wa kurekebisha mifupa na kutoa vipande vya bomu.
Tukio hilo la shambulio la bomu lilitokea usiku wa mkesha wa Krismasi, wakati mtu ambaya hajafahamika kujaribu kuwarushia bomu polisi waliokuwa doria, lakini kabla ya kufanya hivyo lilimlipukia na kumuua na kujeruhi polisi wawili.
Mariam alikutwa na mkasa huo akiwa na wenzake kwenye doria siku ya siku kuu ya Krismasi katika eneo la Kotazi ya Majengo Kata ya Majengo Manispaa ya Songea.
Baada ya tukio hilo WP Mariam pamoja na PC Mselem mwenye namba G 7903 ambaye alijeruhiwa mkono wake wa kushoto walipelekwa hospitalini ambapo Pc Mselem alitibiwa na kuruhusiwa na Mariam alilazwa na kuendelea na matibabu.
Akizungumza na gazeti hili WP Mariam alisema anamshukuru Mungu kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na tayari amefanyiwa upasuaji katika bega lake la kushoto jana saa saba mchana, lakini bado ana maumivu katika mkono huo.
Wakati huohuo , baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea, wameviomba vyombo vya usalama mkoani Ruvuma kuwachukulia hatua kali watu wote ambao wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
“Kwa kweli hali inatisha tunaomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vyote vya usalama, mgambo, jeshi na wananchi tushirikiane kukomesha uharifu huu kwani tayari hali inatisha tunaogopa, hatujui usalama wetu hili ni tukio la tatu ndani ya mwaka huu kutokea na askari wetu wanashambuliwa huu ni unyama usiokubalika, wananchi tuwafichue waharifu hao kwani watatuangamiza,” alisema Michael.
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na timu ya makachero kutoka makao makuu ya jeshi hilo, wanawasaka watu watatu ambao wanasadikiwa kujihusisha na ulipuaji wa mabomu huku mwenzao mmoja akiwa amefia katika eneo la tukio.
Powered by Blogger.