Moto wateketeza maduka 18, magari na pikipiki Handeni
MOTO mkubwa umeteketeza maduka 18 katika mtaa wa Kwakivesa wilaya ya Handeni mkoani Tanga ba
MOTO mkubwa umeteketeza maduka 18 katika mtaa wa Kwakivesa
wilaya ya Handeni mkoani Tanga baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta
kugonga nguzo ya umeme kupinduka na kisha kuanza kuwaka moto uliosambaa
hadi kwenye maduka hayo.
Taharuki hiyo imetokea leo
majira ya saa 5:00 asubuhi baada ya lori hilo lililokuwa kwenye mwendo
kasi kutaka kumkwepa mwendesha bodaboda na kujikuta likiacha njia na
kugonga nguzo ya umeme na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi huo.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai kuwa moto huo ulitokea saa 5.asubuhi katika mtaa huo
kufuatia roli la mafuta aina ya Fuso kugonga nguzo ya umeme na
kusababisha betri kutoa cheche zilizosababisha moto kuanza kuwaka.
Kamanda
Kashai amesema roli hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Ali Makelele
ambaye bado hajapatikana huku utingo wake aliyemtaja kwa jina moja la
Mfundo akiwa amekimbizwa hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu
Zaidi baada ya kuungua vibaya.
“Moto ulianza
kuliteketeza roli hilo la mafuta na baadaye ukasambaa kwenye maduka
jirani ,hali ilikuwa mbaya sana, hadi sasa hatujajua hasara
iliyopatikana, tutakapokuwa na taarifa kamili tutawataarifu“, amesema
kamanda Kashai.
Aidha mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza
kuwa moto huo ulishika kasi kwa haraka kutokana na hali ya hewa kuwa ya
upepo mkali licha ya juhudi za wananchi kuuzima lakini uliwashinda
nguvu.
Aidha jeshi la polisi limelaani mtindo unaoota
mizizi hivi sasa wa wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani baada ya
tukio la moto kutokea kikosi cha zimamoto kutokea Korogwe kilifika
katika eneo la tukio lakini badala ya kuachwa kufanya kazi yake
kikashambuliwa.
Shambulio hilo la wananchi kwa zimamoto
limesababisha hasara ikiwa ni pamoja na kuvunjwa vioo vya gari, kupotea
kwa vitendea kazi pamoja na baadhi ya askari wa zimamoto kujeruhiwa.
Usiache kusoma gazeti la Mwananchi kesho kwa habari Zaidi