Sumaye: Chagueni kiongozi mzalendo asiye na makundi
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Mbeya. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataka
Watanzania kuchagua kiongozi mzalendo asiye na makundi atakayewainua kwa
kadri inavyowezekana ili wawe na maisha bora.
Sumaye alisema hayo jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya katika tamasha la kuliombea Taifa na kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.
“Watanzania,
mwakani tunayo nafasi ya kumuweka kiongozi wa aina hiyo. Hivi sasa kuna
tatizo la kuporomoka kwa uzalendo katika nchi yetu.
“Watu
wanaanza kuthamini masilahi binafsi na hili limewakumba viongozi wengi
wa umma hadi wanasiasa,” alisema na kuongeza kuwa upotevu wa uzalendo wa
kweli unasababisha hasara nyingi kwa mali za nchi hasa maliasili.
“Mauaji
ya wanyama wetu kama tembo, faru, utoroshaji wa rasilimali zetu,
uharibifu wa misitu, mikataba isiyofaidisha wananchi, vyote hivi ni
matunda ya watu kukosa uzalendo wa dhati,” alisema.
Alisema watu huangalia zaidi kujitajirisha hata kama ni kwa gharama kubwa kwa nchi.
“Hili
ni jambo la hatari sana kwa amani ya nchi likiachiwa kuota mizizi,
hivyo ni vyema kiongozi tutakayemtafuta mwakani awe mzalendo wa dhati
adhibiti hali hiyo,” alisema.
Sumaye anayetajwa kuutaka
urais mwakani, alisema nchi inahitaji kiongozi mwenye upeo, kuielewa
nchi barabara, kuwaelewa Watanzania vyema na matatizo yao yawe yanamgusa
moyoni mwake.
“Kiongozi huyo lazima aelewe Watanzania wanataka nini,
yeye anataka kutupeleka wapi na anatufikishaje huko. Asiwe kiongozi wa
kutuburuza anavyotaka au asiyejali yanayotupata ambayo yana maumivu
kwetu,” alisema Sumaye.
Huku akisikilizwa na waumini hasa wa madhehebu ya dini ya Kikristo, Sumaye alisema utawala wa sheria na demokrasia ni muhimu.
Alisema
nchi nyingi zimejikuta katika machafuko kwa sababu kiongozi wake wakati
mwingine huweka katiba na sheria kando na kutawala kwa imla kadiri
anavyoona inafaa.
“Utaratibu unaomweka madarakani
kiongozi ni vyema akauheshimu na kuutii. Tunahitaji atakayeheshimu
katiba ya nchi na sheria zinazowekwa mara kwa mara kwa masilahi ya
umma,” alisema.
Sumaye alisema kiongozi anayefaa
kuongoza Tanzania ni lazima awe tayari kuilinda na kuikuza demokrasia ya
vyama vingi ambayo imeanzishwa kwa masilahi ya wananchi.
“Ili
aina hii ya utawala iwasaidie wananchi ni lazima vyama vya upinzani
viwe na nguvu ya kuwa changamoto kwa chama tawala, hiyo ndiyo maana na
faida ya demokrasia ya vyama vingi,” alisema na kuongeza kuwa:
“Kiongozi
mkuu wa nchi hawezi kuongoza Serikali peke yake bila wasaidizi kama
mawaziri, wakuu wa vyombo vya dola, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na
wilaya, ni wajibu wake kuwaweka watakaomsaidia na wanaoelewa majukumu
yao vyema kwa wananchi.
Sumaye alisema kiongozi stahiki
ni lazima awe na uwezo wa kuweka madarakani serikali itakayowajibika
kwa umma na kusimamia masilahi yake.