Hakimu ajitoa kesi ya jumuiya ya Uamsho
Baadhi ya watuhumiwa wa Ugaidi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, jijini Dar es Salaa. Picha na Tausi Ali
Dar es Salaam.Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen
Liwa amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
Ni
baada ya wakili wa washtakiwa hao wa ugaidi, Abubakar Salim kumtaka
ajitoe kuisikiliza kesi hiyo ili iweze kupangiwa hakimu mwingine ambaye
atatoa uamuzi juu ya hoja zao walizozitoa mahakamani hapo Septemba
19,2014.
Salim aliiambia mahakama kuwa baada ya
kushauriana na wateja wao na uamuzi uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu,
Dk Fauzi Twaib wakaona kuwa ni ukweli kuwa Hakimu Liwa alikwisha toa
uamuzi wake juu ya hoja zao Oktoba Mosi, 2014 kuwa mahakama hiyo ya
kisutu haina mamlaka ya kuzikiliza.
Alidai Mahakama Kuu
katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Twaib umeelekeza kuwa Mahakama ya
Kisutu inayo mamlaka ya kuzisikiliza hoja za washtakiwa hao wa
ugaidi na hata kuzitolea uamuzi.
“Mahakama Kuu
imeelekeza mawakili wa upande wa utetezi kama tutakuwa na hoja mpya
ama za zile za awali tuzitoe kwenye mahakama hii ya Kisutu ili ziweze
kutolewa maamuzi hivyo naona ni bora ujitoe tupate neno kutoka kwa
hakimu mwingine.”Alisisitiza kusema wakili huyo mahakamani hapo.
Wakili
wa Serikali Mkuu, Benard Kongola alimuomba Hakimu Liwa asijitoe
katika kuisikiliza kesi kwa madai sababu zilizotolewa na upande wa
utetezi za kumtaka ajitoe hazina msingi.
Kongola
alieleza kuwa uamuzi uliotolewa na Jaji Twaib aliamuru utekelezaji wa
hoja za upande wa utetezi katika kesi hii ya ugaidi zisikilizwe na
kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Kisutu.
“Tukiendekeza
hii tabia tutamaliza mahakimu wote wa mahakama hii tunasisitiza upande
wa utetezi utoe sababu za msingi za wewe kujitoa.”Alisema Kongola.
Akijibu
hoja hizo, Wakili Salim alieleza kuwa ili haki ionekane inatendeka wewe
Hakimu Liwa ujitoe ili hakimu mwingine atoe maamuzi wa hoja zetu.
Hakimu
Liwa alisema ni kweli nilikwisha toa uamuzi wangu juu ya maombi ya
washtakiwa lakini Mahakama Kuu imeona kivingine kuwa sijatumia mamlaka
yangu vizuri nakubaliana na uamuzi huo.
Lakini uamuzi
huo wa Jaji Twaib haukufafanua nini kifanyike, umetuacha hoi, ila
alitoa angalizo kuwa ushahidi wa kesi hauwezi kutoka hewani na kwamba
maelezo yaliyomo katika hati ya mashtaka ya kesi hiyo yapo sahihi.
“Kitu
ambacho hata mimi nilikuwa nakishangaa ni hii hati ya mashtaka kuletwa
Tanzania Bara badala ya Visiwani, lakini nilipoisoma sheria ya ugaidi
nikabaini mtu anaweza kushtakiwa mahali popote.” Alisema Hakimu Liwa.
Alisisitiza
kuwa kwa mujibu wa sheria Mahakama Kuu ndiyo yenye uwezo wa kuisikiliza
kesi hii na siyo mahakama ya Kisutu hivyo yeye hawezi kusema kitu labda
kesi ingekuwa imefikia kwenye mwenendo wa uhamishaji shauri (Committal
Preceding).
Hatua hiyo inafikiwa baada ya upelelezi
wa kesi kukamilika inahamishwa kutoka mahakama ya Kisutu kwenda
Mahakama Kuu ambayo inamlaka ya kusikiliza kesi hizo.
“Mimi
nimejifunza kitu hapa, kuwa mimi najua nini na wenzangu wanajua nini
hivyo siwezi kuendelea na kesii haitakuwa haki najitoa.”Aliongeza
kusema Hakimu Liwa na akajitoa na kuiahirisha hadi Januari 13,2015 ili
ipangwe kwa hakimu mwingine.