Wajisaidia vichakani kwa kukosa choo
Moshi. Kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika
mazingira magumu cha Global Vision, kilichopo Chekereni Wilaya ya Moshi,
Kilimanjaro kinakabiliwa na ukosefu wa choo hali inayosababisha watoto
kujisaidia vichakani.
Mlezi wa kituo hicho Anastasia
Peter alisema alipopokea msaada na magodoro kutoka kwa wafanyakazi wa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Alisema hali hiyo inasababisha
watoto hao kupata magonjwa ya mlipuko mara kwa mara.
Peter aliitaka Serikali kutenga fungu kwa ajili ya kuvisaidia vituo vya kulelea watoto vinavyomilikiwa na watu binafsi.
Alisema
hiyo itwasidia kuwajengea uwezo badala ya kuwaachia mzigo huo wamiliki
peke yao. Kaimu Meneja wa Tanesco, mkoani Kilimanjaro Mathias Solongo
alisema msaada huo umetolewa ili kukabiliana na changamoto walizonazo.
Alisema wafanyakazi hao wametoa Sh5 milioni kwa ajili ya kununua magodoro na chakula na wakiahidi kujenga choo kituoni hapo.
Mmiliki
wa kituo hicho, Mchungaji Saimon Sori alisema msaada huo utaondoa
tatizo la muda mrefu kituoni hapo watoto kulala kitanda kimoja na
wengine wakitandika maboksi sakafuni.
Sori alisema mashirika mengine yaige mfano huo wa kutembelea watu wenye uhitaji ili wawasaidie na watabarikiwa na Mungu.