Dk Slaa azidi kumbana Kikwete achukue hatua dhidi ya Prof Muhongo
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amesema Rais Jakaya Kikwete asitumie kivuli cha
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa
amesema Rais Jakaya Kikwete asitumie kivuli cha mapumziko ya sikukuu
kuchukua uamuzi dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo anayehusika katika kashfa ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow
ya Sh306 bilioni.
Pia, amemtaka Rais Kikwete kuwaeleza
ukweli Watanzania kuhusu kigogo wa Ikulu aliyenufaika na mgawo wa fedha,
Sh800 milioni za akaunti hiyo zilivyotumika na mnufaikaji alikuwa nani.
Dk
Slaa aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru
wananchi wa Somangila-Kigamboni Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam
kwa kuwachagua wenyeviti sita kati ya 13 wa Ukawa wa kata hiyo yenye
mitaa sita.
“Tunamtaka haraka Rais Kikwete amfukuze
kazi Profesa Muhongo, asiseme anakula ‘bata’ Msoga (Kijijini kwake
Bagamoyo mkoani Pwani) eti sikukuu...Tumemchagua atusimamie na
kutuongoza kwa saa 24 kwenda kula Krismasi huku wagonjwa wanakufa
hospitalini ni dharau kwa Watanzania,” alidai.
“Rais ni
mtumishi wa Watanzania, wachache hawawezi kunufaika na mabilioni hayo
huku wengi wanaendelea kusota na ugumu wa maisha...Unakulaje ‘bata’
wakati Watanzania kila kona wanataka uchukue uamuzi kwa masilahi ya
Taifa, hiyo ‘bata’ kweli au ndiyo msemo unaosema ukimwaga mboga mimi
ninamwaga ugali anamwogopa Muhongo kumwajibisha?” alisema Dk Slaa.
Alisema
kumfukuza kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka pekee hakutoshi, huku wengine waliofanya makosa kama
hayo bado wanaendelea kuzunguka mitaani.
“Huyu
Tibaijuka ametolewa kafara tu, kuna kigogo wa Ikulu ambaye anaratibu
shughuli za Ikulu za nchi nzima (jina tunalihifadhi) alipewa Sh800
milioni lakini yeye hajaguswa, sasa Rais Kikwete atueleze kwa nini
alimchukulia hatua Profesa Tibaijuka na huyu kigogo wake amemwacha kuna
nini hapa kinachoendelea,” alisema Dk Slaa.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka
huu, Rais Kikwete alisema amemweka kiporo waziri huyo hadi atakapopata
ufafanuzi wa mambo kadhaa na kwamba atakapojiridhisha ataujulisha umma.
Dk
Slaa alisema, “Rais Kikwete anatumia maneno ya yasiyofaa katika jambo
lenye masilahi mapana, kumweka kiporo kisheria au utawala bora halipo na
mimi kwa miaka zaidi ya 60 nimekuwa Padre, Mbunge kwa miaka 15 na sasa
mtumishi wa umma sijawahi hata siku moja kusikia mtu badala ya
kuchukulia hatua anawekwa kiporo.”
Juzi, Ikulu kupitia
kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema suala la Profesa
Muhongo litatolewa uamuzi wakati wowote baada ya mapumziko ya sikukuu.
Rais
Kikwete bado hajakamilisha kulishughulikia suala hilo na kwamba
litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa hatua alizozichukua.
“Unakumbuka
Rais alichosema? Bado analifanyia kazi, atakapomaliza tu mtajulishwa,
sasa hivi ni kipindi cha sikukuu,” alisema Sefue.
Katika
mkutano huo, Dk Slaa alisema, “Hamkukosea kuwachangua wenyeviti wa
Chadema wanaotokana na Ukawa kwani dhamira yetu ni kuhakikisha tunaitoa
CCM madarakani mwaka 2015 na hii ilikuwa njia tu.”
Aliongeza:
“Ninyi viongozi hakikisheni mnatekeleza yale mliyoyaahidi kwani
kutokufanya hivyo mtakuwa mnakichimbia kaburi Chadema mwakani.