Sethi:Tegeta Escrow namwachia Mungu
Wednesday Dec 3, 2014
Na Thobias Mwanakatwe
3rd December 2014
B-pepe
Chapa
Sitakubali kutaifishwa mitambo ya IPTL
Akana kuangamiza Kanu Kenya
Akana kuangamiza Kanu Kenya
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwa simu katika mahojiano maalum na NIPASHE kuhusu mambo yaliyojitokeza katika mkutano wa16 na 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wabunge walipokuwa wakijadili kashafa ya uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Sethi alisema maamuzi yaliyofikiwa na Bunge kimsingi ni ya kumuonea kwa sababu alifuata taratibu na sheria za nchi wakati wa kutoa fedha hizo, hivyo anamuachia Mwenyezi Mungu ndiye ataamua hatma ya suala hilo.
Sethi ambaye hakutaka kueleza alipo kwa sasa, alisema uamuzi wa Bunge haujamtendea haki kwa sababu kwanza hakupewa nafasi na chombo chochote kutoa maelezo yake na badala yake yamefikiwa maamuzi mazito kama hayo.
Mahojiano kati ya mwandishi wa habari hii na Sethi yalikuwa kama hivi:
Mwandishi: Umesikia maamuzi yaliyotolewa na Bunge kuhusu suala la akaunti ya Escrow, je, unasemaje?
Sethi: Suala hili lipo mahakamani naomba msamaha siwezi nikajibu chochote, lakini kimsingi wabunge wamenionea tu, hizo fedha nimechukua kihalali kwa kufuata sheria za nchi sijaenda kumwibia mtu yeyote. Kunionea hivyo ni kitu kibaya sana, mimi namuachia Mungu tu.
Mwandishi: Kama unaona umeonewa na Bunge, je, unakusudia kuchukua hatua zozote za kisheria?
Sethi: Kwa sasa siwezi kuchukua hatua zozote kwa sababu suala hili kwanza bado lipo mahakamani, tunasubiri uamuzi wa mahakama. Mimi naheshimu mahakama ya kila nchi na Tanzania zaidi kwa sababu hii ni nchi yangu.
Mwandishi: Kufuatia maamuzi yaliyotolewa na Bunge, je, utakuwa tayari kufuta kesi mahakamani inayoendelea kuhusiana na suala hili.
Sethi: Hapana, hatufuti kesi yeyote, tutaendelea mahakamani ili haki iweze kupatikana.
Mwandishi: Zipo taarifa kuwa rekodi yako ni mbaya na ulisababisha hadi serikali ya chama cha KANU nchini Kenya ikaangushwa kwenye uchaguzi.
Sethi: Mimi siyo mtu wa siasa, mimi ni mfanyakazi na ni mfanyabiashara wa kuzalisha umeme siyo siasa, siwezi kuangusha serikali wala chama cha mtu yeyote. Mimi siyo mtu wa siasa kazi yangu ni kuzalisha umeme na Tanzania nimefanya kazi kubwa hiyo kabla ya uwekezaji wangu umeme ulikuwa unazalishwa megawati 10 leo hii zinazalishwa megawati 100.
Pia umeme uliokuwa unazalishwa uliuzwa kwa senti 36 mimi nauza kwa senti 25, wengine wanazalisha kwa senti 50 na wakitaka kufunga kiwanda (mitambo) sawa ili waendelee na umeme wa bei ya juu, Mungu mkubwa tunamuachia yeye ndiye ataamua.
Mwandishi: Moja ya maamuzi ya Bunge ni kwamba watataifisha mitambo. Je, unasemaje?
Sethi: Hilo haliwezekani kabisa na kufanya hivyo tutakuwa tunaipeleka nchi kubaya sana na hakuna atakayeingia Tanzania tena. kwanza sikupewa nafasi hata ya kujieleza.
Miongoni mwa tuhuma alizozitoa Kafulila bungeni ni madai kwamba Seth alichangia kukizamisha chama kilichokuwa tawala nchini Kenya cha Kanu kutokana na kashfa maarufu ya ufisadi nchini humo ya Goldenberg.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge walitoa maazimio manane kuhusu sakata la Escrow likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema.
Wengine waliopendekezwa kuvuliwa yadhifa zao ni wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Pia wamo Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini waliohusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Kadhalika, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kutakiwa kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na watakaobainika kuhusika kwenye vitendo vya jinai hatua za sheria zichukuliwe dhidi yao.
Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda tume ya uchunguzi ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo.
Majaji waliotakiwa kuchunguzwa ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha, Bunge lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Pia, serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge la kupitia mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi za kufua umeme na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba hiyo kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.
CHANZO:
NIPASHE
Habari Zaidi