Mume auawa kwa kisu na hawara wa mkewe

Mkazi wa Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero, Amon Nyenja amefariki dunia baada ya kuchomwa
Kilombero. Mkazi wa Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero, Amon Nyenja amefariki dunia baada ya kuchomwa kwa kisu na anayedhaniwa kuwa ni hawara wa mke wake mdogo.
Tukio hili lilitokea usikuwa Desemba 23 huko Mang’ula na inadaiwa kuwa marehemu alirudi nyumbani saa 3.30 usiku na kumkosa mkewe hivyo kuamua kumtafuta katika maeneo mbalimbali.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mang’ula, Shabani Lichaula na Mkuu wa kituo cha Polisi Mang’ula, Nkilijia Lazaro walisema polisi inamshikilia mke huyo mdogo wa marehemu huku likimtafuta mtuhumiwa.
Lichaula alidai kuwa marehemu katika kumtafuta mkewe huyo alimkuta akiwa amesimama mahali na mwanamume na mwanamke huyo alikimbia na kutokomea na marehemu Nyenja aliamua kumvaa mgoni wake lakini alizidiwa baada ya mtu huyo kumchoma kisu cha ubavuni hadi utumbo kutoka nje.
Lichaula alisema baada ya Nyenja kuchomwa kisu alipiga kelele za kuomba msaada na wasamaria wema walijitokeza na kumpeleka Kituo cha Afya Mang’ula.
Mganga Mkuu wa Mang’ula, Eugen Shirima alisema baada ya huduma ya kwanza walimpatia rufaa ya kwenda Hospitali ya Mtakatifu Francis, Ifakara kwa matibabu lakini alifariki dunia wakiwa njiani.
Powered by Blogger.