Baadhi ya wakazi wa
Kata ya Mbugani, Mtaa wa Mbugani A na B wameathiriwa na mafuriko
yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana kwa saa nne.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema mvua hiyo imesababisha vitu vyao kusombwa na maji na nyumba kubomoka.
Esther Misanga, mkazi wa mtaa huo, alitaja baadhi
ya vitu vilivyoharibiwa na mvua hiyo kuwa ni magunia 20 ya mahindi,
magunia 10 ya daga na mifuko 20 ya unga wa sembe, vyote vikiwa na
thamani ya jumla ya Sh2 milioni.
“Nimepoteza magunia 50 ya mahindi na unga wa dona.
Nimepata hasara kubwa sana. Sikutegemea yangetokea mafuriko makubwa
kama haya,” alisema Misanga.
Alisema Serikali iliwaahidi kuwahamisha maeneo
hayo kutokana na kupata adha ya mafuriko ya mara kwa mara, lakini hadi
sasa utekelezaji huo haujafanyika.
“Serikali ilituahidi kutupatia maeneo kule Kisesa,
lakini tangu wazungumze hadi sasa mwaka umepita hawajatuonyesha maeneo
hayo. Tunaiomba Serikali ifanye kila liwezekanalo ituhamishe katika eneo
hili tunusuru maisha yetu,” alisema Misanga.
Akizungumza kwa simu, mtendaji wa Kata ya
Mbungani, Baruani Hawadhi alisema maafa hayo siyo makubwa kwa kuwa
hajapata taarifa za vifo vya watu zaidi ya uharibifu wa mali za watu.