Tatizo la Luku latesa wananchi
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema linaendelea na kazi ya kurekebisha hitilafu kwenye mfumo wa Luku kwa njia ya mitandao ya simu ili kuwalipa ‘units’ wateja wake waliokatwa pesa zao kabla ya kupata huduma hiyo.
Siku mbili zilizopita, huduma ya Luku imekuwa haipatikani kwa njia ya simu, jambo lililosababisha vituo vingi vinavyotoa huduma hiyo kwa mashine za Maxi Malipo kuwa na msongamano mkubwa wa watu.
Akizungumzia suala hilo, Meneja Uhusiano wa
Tanesco, Adrian Severin alisema jambo la kwanza ni kuwapa ‘units’ wateja
ambao tayari wameshalipia, baadaye wateja wengine watanunua umeme
kupitia simu zao.
“Kuna hitilafu ya kiufundi imetokea kwenye mfumo
wa Luku, tunatarajia usiku wa leo (jana) kazi itakamilika. Baada ya hapo
tutatoa huduma kwa wote waliokatwa pesa zao bila kupata huduma,”
alisema Severin.
Msemaji huyo wa Tanesco alisema huduma ya Luku bado inapatikana kupitia Maxi Malipo na Benki za CRDB, NMB.
Alisisitiza watu kutumia miamala ya kibenki kulipia umeme ili kupunguza foleni kwenye mashine za Maxi Malipo.
Wananchi wengi wameonekana kujazana kwenye vibanda
vya Luku wakitaka huduma hiyo, baadhi yao walizoea kununua umeme kwa
njia ya simu ili kuokoa muda wa kukaa kwenye foleni muda mrefu.
Mkazi wa Tabata Segerea, George Ismail alisema tangu juzi wanapata usumbufu maeneo ya kununulia umeme wa Luku.
“Jana nimekaa kibandani saa matatu nikisubiri
kununua umeme. Sijazoea hali hii, ninajua kuna shida fulani, lakini
sijui tatizo ni nini, sijapata taarifa zozote kutoka Tanesco,” alisema
Ismail na kuongeza kuwa alijaribu kwa njia ya simu pia huduma hiyo
ilishindikana.
Hata hivyo, jana Tanesco lilitoa taarifa kupitia
gazeti hili juu ya tatizo la kiufundi lililotokea kuanzia Februari 28 na
kubainisha kuwa mafundi walikuwa wakiendelea kulifanyia kazi tatizo
hilo.
Hii siyo mara ya kwanza huduma ya Luku kuleta adha
kwa wananchi. Januari, mwaka huu kulikuwa na tatizo la upatikanaji wa
Luku katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam.