CHIMBUKO LA USHAIRI; UBORA NA UDHAIFU WAO.
CHIMBUKO LA USHAIRI; UBORA
NA UDHAIFU WAO.
Dhana
ya ushairi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili
yake. Baadhi ya wataalam hao ni kama ifuatavyo:
Mssamba,
D.P.B. (2003) akimnukuu Shaban Robert, anasema; “ushairi ni sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi zaidi ya kuwa na sanaa ya vina
ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.”
Mnyampala
(1970) anasema kuwa “ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho
kitu kilichobora sana maongozo ya Dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha
nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.”
Amri
Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi
haliimbiki halina maana.”
Encyclopedia
American (EA) inaeleza kuwa ushairi ni kauli zenye hisia na ubunifu, mpangilio
fulani wenye urari, uwasilishaji wa tajiriba au mawazo ya mtunzi kwa maana
ambayo huibua tajiriba kama hiyo katika nyayo za wasomaji au wasikilizaji na
kutumia lugha ya picha yenye wizani wa sauti.
Mulokozi
na Kahigi (1982) wanasema ushairi ni “sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio
maalum na fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika
usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au
kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia
inayogusa moyo.”
Hivyo
basi tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa
kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana
kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na
ujumbe.
Dhana
ya chimbuko inafasiliwa na TUKI (2004) kuwa ni mwazo au asili ya kitu.
Baadhi
ya wataalamu wameweza kuelezea chimbuko la ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia
mitazamo au nadharia mbili ambazo ni kama zifuatazo:
Nadharia
ya kwanza inadai kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa
Waarabu.
Na
nadharia ya pili inasema kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la jamii
ya waswahili wenyewe.
Kwa
kuanza na nadharia ya kwanza isemayo kuwa chimbuko la ushairi wa Kiswahili
ulitokana na ujio wa Waarabu ambayo inaungwa mkono na wataalam mbalimbali kama
vile Lyndon
Harries (1962) na Knappet (1979)
Kwa
kuanza na Lyndon (1962) “Swahili Poetry” anatoa hoja tatu ambazo ni ushairi wa
Kiswahili umetokana na Uislamu, ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa
Kenya hususani Lamu. Na maudhui ya ushairi wa Kiswahili yalitokana na ushairi
wa Kiarabu. Utungo wa kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka,
Mwengo bin Athmani (1728)
Ubora
wa nadharia hii au mtazamo wa Harries kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili
ni kwamba umesaidia wengine kuendelea kuchunguza zaidi kuhusu chimbuko la
ushairi wa Kiswahili.
Udhaifu
wa nadharia hii ni kuwa si kweli kwamba ushairi wa Kiswahili uliletwa na
Uislamu bali ulikuwepo hata kabla ya ujio wa Uislamu, kwani ushairi
hautenganishwi na jamii husika. Hivyo jamii za waswahili walitumia Nyanja
mbalimbali za ushairi katika shughuli zao mbalimbali au shughuli zao za kila
siku, kama vile; shughuli za kilimo na ufugaji.
Pia
ushairi wa Kiswahili ulianza karne ya 10BK na ushairi wa Kiswahili ulikuwa
ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa. Wataalam wengi wanakubaliana
kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo.
Udhaifu
mwingine katika mtazamo wake wa kusema kuwa ushairi ulianzia pwani ya kaskazini
ya Kenya si kweli kwa kuwa waswahili walikuwepo hata sehemu nyingine kama vile
Kilwa na Bagamoyo ambapo ushairi wa Kiswahili ulitumika.
Hoja
ya kusema ushairi wa Kiswahili ulitokana na Kiarabu haina mashiko kwa kuwa
waswahili walikuwepo hata kabla ya waarabu na walikuwa na ushairi wao isipokuwa
ujio wao ulileta athari kubwa kwa kuwa ulichanganya na mambo ya dini ya
kiislamu na hati.
Knappert
(1979) “Four centuries of Swahili verse” anasema; “Ushairi wa Kiswahili
ulichipuka kwenye upwa wa Kenya kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na
ulianza katika karne ya 17 na pia ni ushairi wa Kiislamu wenye kuchanganya sifa
za tungo za kiafrika na za kiajemi.
Ubora
wa hoja hii ni kwamba, ni kweli Knappert amekubali kuwa, ushairi wa Kiswahili
ulitokana na waswahili wenyewe.
Hata
hivyo hoja yake ina udhaifu kwa kuwa ushairi wa Kiswahili ulianza kabla ya
karne ya 10 BK na pia amejikita katika maudhui ya mambo mengine kama vile
siasa, uchumi na kijamii. Vilevile amechanganya chimbuko la ushairi wa
Kiswahili na Uarabu.
Nadharia
ya pili inasema kuwa ushairi ni zao la waswahili wenyewe.
Nadharia hii imejadiliwa na wataalam mbalimbali akiwemo Shaban Robert, Jumanne Mayoka (1993) na F.E.M.K. Senkoro, Mulokozi na
Sengo.
Jumanne,
M. Mayoka (1993) anasema ushairi umetokana na jamii ya wanadamu wenyewe na
umesheheneza ukwasi mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika katika hatua zote
za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika historia ambayo mwanadamu amepitia,
Kwa mfano kuwa msamiati uliotumika tangu enzi za kuishi mapangoni, enzi za
uwindaji, ujima, utumwa, vita vya makabila, uvamizi wa wageni, ukoloni na
harakati za kupambana na ukoloni hadi kupata uhuru na maendeleo yake.
Ubora
wa hoja hii ni kwamba ina mashiko ndani yake kwa sababu, kila jamii ina sanaa
yake na ushairi ni moja kati ya sanaa hizo ingawa inaweza ikaathiriwa na sanaa
ya jamii nyingine. Pia ushairi umekuwa ukikua na kuendelea kadri jamii
inavyokuwa na kuendelea.
Udhaifu
wa hoja hii ni kwamba si kweli kuwa katika kipindi hicho ushairi ulikuwa tayari
umesheheni ukwasi mkubwa wa lugha, na kama ulikuwa kweli umesheheni huu ukwasi
wa lugha alipaswa kutuonesha huo utajiri wa lugha anaouzungumzia katika
ushairi.
Senkoro
(1988)
anasema kuwa ushairi uliibuka pale lugha ilipoanza katika kipindi cha uhayawani
(kipindi ambacho mwanadamu alipoanza kupambana na mazingira yake) kwenda katika
kipindi cha urazini (maana) ili kumwezesha binadamu na mazingira yake kwa
mfano, zana za kazi zilizotumika ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana
hizo.
Ubora
wa hoja hii ni kwamba unathibitisha kuwa chimbuko la ushairi ni waswahili
wenyewe, kwani umefanikiwa kueleza kuwa katika jamii yoyote ile maendeleo ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii huambatana au huenda sambamba na maendeleo ya
sanaa mbalimbali ikiwemo ushairi uliotumika katika harakati mbalimbali za
maisha ya mwanadamu.
Pamoja
na kuwa nadharia hii imeonesha kukubalika na wataalamu mbalimbali kama vile Senkoro, Mayoka na Shekhe Amri Abeid, lakini bado ina mapungufu. Hii ni kwa sababu
imeshindwa kuonesha muda maalumu ambapo ushairi wa Kiswahili ulianza na ni wapi
ulianza kutumika. Hili ni suala ambalo linaumiza vichwa vya wataalamu
mbalimbali hadi hivi sasa, kwani hakuna mtaalamu yoyote aliyefanikiwa kuonesha
ni wapi na ni lini ushairi wa Kiswahili ulianza.
Hivyo
basi, kutokana na nadharia hizo mbili tunaungana na nadharia inayosema kuwa,
chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la waswahili wenyewe, kwa sababu
waswahili wana utamaduni wao ambao ulikuwepo kabla ya ujio wa Waarabu. Na
waliutumia ushairi huo katika shughuli mbalimbali za kijamii, kwa mfano katika
harusi, jando na unyago.
MAREJEO:
Knappert,
J. (1979). Four centuries of Swahili
Verse. Heinemann. London.
Mayoka,
J.K. (1993). Mgogoro wa Ushairi na Diwani
ya Mayoka. Ndanda Mission Press.Tanzania.
Mulokozi,
M.M. (1996). Fasihi ya Kiswahili.Chuo
Kikuu cha Dar-es-Salaam.
Senkoro,
F.E.M.K. (1987). Ushairi, Nadharia na
Tahakiki. DUP. Dar-es-Salaam.
TUKI.
(1983). Makala ya Semina ya Kimataifa ya
Waandishi wa Kiswahili. (Toleo la III) TUKI.Dar-es-Salaam.
TUKI.
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.TUKI.Dar-es-Salaam.