Maana ya ushairi.
Massamba
(2003) akimnukuu Shaaban Robert (1968) anasema Ushairi ni sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa sanaa ya vina na
mizani, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Senkoro
(1988) Katika kitabu chake cha Ushairi, “Nadharia na Tahakiki” anasema ni
utanzu wa fasihi utumiao mpangilio wa lugha ya mkato, picha, iliyopangwa kwa
njia iletayo mapigo mahususi au yaliyomo ndani yake.
Kezilahabi,
(1974) katika kitabu chake cha “Kichomi”
anadai ushairi ni tukio, hali, au wazo, ambalo limeoneshwa kwetu kutokana na
upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonesha ukweli
fulani wa maisha.
Wamitila,
(2008) ushairi ni utungo wa sanaa ya
lugha na mpangilio maalum wa mishororo, ama kisauti na kwa maneno mateule kwa
kubuni mbinu za lugha zenye mnato na mbinu nyingine za kibalagha na kimtindo
zinamwezesha mtunzi kuwasilisha ujumbe kwa kifupi na kwa mkokotezo mkubwa
unaoelezea hisia, tukio, ama hali kwa lugha ya mvuto.
Kwa
ujumla ushairi ni sanaa ya lugha ya mkato yenye ughunaji inayosawiri, kueleza
au kuonesha jambo, hisia au katika mpangilio mahususi wa maneno wenye urari wa
vina na wizani wa sauti.
Baada
ya kuangalia tofauti ya ushairi ifuatayo ni tafsiri ya ushairi wa Kiswahili.
Ushairi wa kiswahili umeelezwa na Senkoro (1988) kuwa ni ule ushairi unaotumia
lugha ya Kiswahili katika kuwasilisha mawazo, fikra na vionjo vya moyo wa watu
wanaotumia lugha ya Kiswahili.
Ushairi
wa kiswahili umefafanuliwa tena katika mitazamo mingine miwili. Mtazamo wa
Kimapokeo na mtazamo wa Kisasa.
Katika mtazamo wa Kimapokeo wanadai
kuwa ushairi wa kiswahili ni ule unaotungwa kwa kufuata kanuni za urari wa vina
na mizani, ambazo ni kanuni za ushairi wa Kiswahili. Miongoni mwao ni wazee na
vijana wa UKUTA ( Chama cha usanifu wa Kiswahili na ushairi Tanzania) Amri
Abedi.
Mtazamo wa wanausasa;
Ushairi wa Kiswahili si lazima ufuate kanuni za utungaji wa mashairi. Vina na
mizani si vya lazima katika ushairi. (Kezilahabi, E, Mulokozi, M.M na K.
Kahigi) maelezo haya yanayofafanua maana ya ushairi wa Kiswahili yana mapungufu kadhaa kama ifuatavyo;
Wanamapokeo
wameshindwa kuelezea vipengele vya maudhui. Wamejikita zaidi katika vipengele
vya kifani (urari wa vina na mizani) hawajaeleza waswahili ni watu gani?
Mashairi haya yanazungumzia mawazo yapi?
Wanausasa
wamepinga hoja tu ya wanamapokeo kuwa ushairi wa kiswahili si lazima ufuate
kanuni za urari wa vina na mizani. Hawajatoa maana yao kuhusu ushairi wa
Kiswahili.
Kwa
hiyo, ushairi wa Kiswahili ni utungo unaotumia lugha ya kiswahili kuelezea
maisha ya waswahili (watumiaji wa lugha ya kiswahili) katika Nyanja mbalimbali
za maisha, wenye kusheheni fani na maudhui yanayohusu watumiaji wa kiswahili
Ama
kuhusu Muhula ni kipindi fulani katika mwaka kinachohusishwa na tukio fulani
pia huzingatia kigezo cha mwaka muafaka.
Mihula ya ushairi wa kiswahili.
Kwa mujibu wa Kezilahabi (1983) amebainisha Mihula ifuatayo;
Muhula wa Urasimu
(hadi 1885). Katika kipindi hiki kanuni za utunzi ziliwekwa na ushairi
ulitawaliwa sana na mitazamo ya kidini na Kimwinyi. Mfano; wa tungo za ushairi
zilizokuwepo kipindi hiki ni utenzi wa
tambuka 1728 kilichoandikwa na Bwana
Mwengo, utenzi wa Hamziyyah 1690
Sayyid Abdarus , utenzi wa Al-Inkishafi utenzi uliojadili maswala
ya matatizo na mazingira yaliyohusu Afrika Mashariki (1810-1820). Uliandikwa na
Sayyid Abdalah A. Nassir. Makala za semina ya Kimataifa ya waandishi wa
Kiswahili (uk. 148-150)
Muhula wa Utasa
1885-1945. Kipindi hiki ni kipindi cha mabadiliko ya kiutawala na kielimu.
Kubadilika kwa hati ya maandishi kutoka Kiarabu kwenda Kirumi. Kipindi hiki
maandishi machache yaliandikwa wakat huu, mengi yakiwa maandishi ya Hemed
Abdallah. Baadhi ya tenzi zilizopatikana ni Utenzi wa Vita vya Majimaji. Kanuni
za uandishi wa mashairi zilianza kupotea. Makoloni ya Ulaya yalikuwa
yakigawanwa Afrika (uk. 149-150)
Muhula wa Urasimi mpya
(1945-1960) kipindi hiki kilikuwa ndicho kipindi cha kufufua kanuni za utunzi.
Shaaban Robert, Amri Abeid Khamis Amani, M. Mnyampala, Ahmmed Nassir na
wengineo. Kipindi hiki ndipo kitabu cha sheria za kutunga mashairi kiliandikwa
wakati ambao kilikuwa kinahitajika sana ili kuweka kiungo kizuri na wakati
uliopo. Yaani kueleweka vizuri katika
wakati uliopo (1954)
Mtindo
uliotumika sana ni ule wa mizani 16 yaani 8+8 kwa kila kipande cha mshororo
katika mishororo minne . Mtindo uliotumika sana na Muyaka bin Haji katika karne
ya 18
Wanamapokeo
waliamini kuwa shairi liliandikwa ili liimbwe wakati huo mghani Radioni
Athumani Khalfani alikuwa amezoea kuimba mtindo huo na katika mahadhi ya aina
moja.
Muhula wa Usasa
(1967-hadi leo) ni muhula wa mtazamo mpya kimawazo kisanaa, hivyo kuna mgogoro
katika uwanja wa ushairi. Kipindi hiki washairi walikuwa wanatafuta uhuru wa
kisanaa.
Mgogoro
juu ya kanuni uandishi wa ushairi uliongezeka zaidi.
Muainisho
huu wa mihula ya ushairi kwa mujibu wa Kezilahabi, unamapungufu yafuatayo yaliyobainika;
Hujahusisha
usimulizi na usimulizi, inaaminiwaka kuwa asili ya ushairi wa kiswhili ni tungo
simulizi hasa nyimbo zinazofungamana na ngoma. Wataalam wanaounga mkono hoja
hii ni Chiraghdin (1971), Shariff (1988), Nassir (1977) na Ohly (1985).
Pia
haja zungumzia ushairi kabla ya karne ya 17. Kutokana na wataalam inaonekana
ushairi wa kiswahili ulianza kutungwa na kughanwa kwa ghibu/kuandikwa karne ya
10BK.
Hajabainisha
wazi muhula wa Utasa uko vipi? Kwa sababu bado washairi wengi walikuwepo kutoka
Tanga, Mombasa mfano; Shaabani Robert.
Kwa
mujibu wa Anord, R. (1973) mtaalam huyu ameainisha mihula ya ushairi katika
vipindi vitatu kama ifuatavyo;
Kipindi cha kabla ya Ukoloni:
yeye alitumia mtazamo wa matabaka. Ushairi uliokuwepo ni ule ulioakisi hali ya
watu, mamwinyi na ufalme. mfano; ushairi wa Mwanakupona ulisisitiza kuwatukuza
mamwinyi na wafalme. Ushairi huu wa Mwanakupona uliandikwa na Bi Mwanakupona
binti Mshamu.
Muhula wa Upinzani:
ni kipindi ambacho upinzani ulijitokeza katika utetezi wa Uislam na mila za
jadi dhidi ya Ukristo baada ya vita vya majimaji. Kipindi hiki ushairi ulipo na
hadi kilipofika kipindi cha mwaka (1930). Kipindi hiki kiliwakilishwa na
Shaaban Robert.
Kipindi cha baada ya Uhuru:
hiki ni kipindi ambapo washairi wengi walitunga mashairi kushughulikia masuala ya ujenzi wa jamii mpya. Hii ni
kutokana na mabadiliko ya fani ya ushairi. Mfano; mashairi ya Mohammed S.
Khatibu ya Fungate la Uhuru na Wasakatonge yanasisitiza juu ya ujenzi wa jamii
mpya.
Mapungufu ya Anord.R (1973)
katika uainishaji wa mihula ya ushairi wa kiswahili;
Hajaonesha
muda halisi kwani anaweka muda katika majumuisho. Mfano; anasema “Kipindi kabla
ya uhuru” kuanzia lini hadi lini, kipindi cha upinzani ni lini hadi lini na
kipindi baada ya uhuru kuanzia mwaka gani hadi mwaka gani na lini?
Hajahusisha
ushairi wa kiswahili na usimulizi kama ndicho chanzo (asili) ya ushairi wa
Kiswahili, kwani nyimbo zilizofungamana na ngoma.
Kwa
mujibu wa Ohly,R. (1973) mtalaam huyu amegawa mihula ya ushairi katika vipindi
vifuatavyo;
Kipindi
cha kabla ya mwaka 1888 kwa mujibu wa Ohly;
anasema kipindi hiki kilibainisha mashairi/ushairi wa aina tatu. Ushairi wa
Kidini uliozungumzia masuala ya kidini. Mfano; utenzi wa Hamziyya, pamoja na ule wa Inkishafi. Ushairi wa kawaida
ni ushairi ambao ulikuwa haufungamani na upande wowote isipokuwa unatoa maadili
ya dunia. Ushairi wa tungo za Jadi ambazo zipo 13 baadhi ya hizi tungo za jadi
ni shairi, utenzi, wimbo, ukwafi, zivindo, kimai, Hamziyya, Inkishafi
au Dura mandhuma.
Kipindi
cha 1888-1918; mtalaam anaeleza kuwa katika kipindi
hiki kumekuwapo na ushairi wa maelezo usiofungamana na siasa. Ushairi wa
kutathimini, ushairi wa kupinga ukoloni mfano; Saadan Kandoro, Amri Abeid
pamoja na Shaaban Robert. Mashairi ya vikaragosi ambayo ni ya wale wenye hali
ya chini/duni. Mfano; mashairi ya Shaaban Robert, mashairi ya S. A. Kandoro.
Kipindi cha 1918-1949; Ohly
anasema kuwa kipindi hiki kilitawaliwa na fasihi ya ukoloni. Mikondo ya ushairi
iliyokuwepo kipindi hiki ni ushairi wa maadili, ushairi wa malimwengu, na
tafsiri kama aliyoifanya Nyerere J.K. (1968) katika ushairi wa kidrama wa kazi
ya Shakespeare ambazo ni kazi za mabepari wa Venis. Mfano wa ubeti;
Nerissa: Naam nitampa bure bila
ficha,
Poveeni na Jesika kutoka kwa myahudi,
Hati maalum ya hiba baada ya kifo chake,
Ataacha kwenu nyingi kila atakacho.
Mapungufu
ya uainishaji wa Ohly (1973) yanakumbwa na changamoto zifuatazo;
a.
Hajatueleza uhusiano uliopo kati ya
ushairi simulizi na ushairi aliouainisha katika vipindi vyake.
b.
hajaeleza baada ya muhula wa 1918-1949
mashairi yaliyoendelea mapaka leo yana maudhui gani
Baada
ya kuangalia wataalam hawa katika kuainisha vipindi vya ushairi tunabaini kuwa
mihula ya ushairi inaweza ikagawanywa kama ifuatavyo;
Muhula wa usahiri simulizi mpaka
1500.
Muhula huu unatueleza kuwa asili ya ushairi unaonyesha kuwa ni Ngoma na nyimbo
ambazo zinafungamana na ngoma. Mfano; utenzi
/ tungo za Fumo Liyongo.
Muhula wa Urasimu 1500-1890;
kipindi hiki cha ushairi kilitambulika kwa kuwepo kwa tungo za utenzi wa
Tambuka 1728, Utenzi wa Hamziyya 1644
na utenzi wa Al-Inkishafi 1820. Hiki
kipindi ambacho kanuni za utunzi wa ushairi zilitumiwa kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na sababu hiyo pia kipindi hiki kilipewa jina la kipindi cha Utasa hii
ni kwa mujibu wa Kezilahabi.
Muhula wa Mzinduko na Urasimi
mpya 1946-1967 kutoka kipindi cha utasa ufufuo wa
kanuni na mwongezeko wa kazi za ushairi zilionekana. Mfano; 1957 kitabu cha sheria za kutunga mashairi cha Amri
Abeid kilichapishwa. Washairi kama vile M. M. Mlokozi na M. Mnyampala, Kandoro.
S. Hivyo ikaonekana kazi za ushairi zimezinduka.
Muhula wa Mageuzi na Majaribio
1968-hadi leo. Kipindi hiki kinaonesha majaribio na
migogoro mbalimbali juu ya kujadili kanuni za kutunga mashairi (ushairi).
Majaribio hayo yamefanya kuzuka kwa ushairi mpya ujulikanao kama ushairi wa
Mavue (masivina, huru, mlegezo) aina ya Bongo Flava, ambapo kuna uimbaji na
utendaji.
Katika taaluma ya fasihi
simulizi, suala la kuwa na mitazamo tofautitofauti miongoni mwa wataalamu ni
kitu cha kawaida tangu kale. Fasihi simulizi kiulimwengu imekuwa ikitazamwa na
kuchambuliwa kwa nadharia kadhaa tangu zamani. Katika bara la Afrika kuna
wataalamu wengi kutoka ndani na nje ya bara hili waliotoa michango yao kadhaa
katika kuichambua fasihi simulizi ya kiafrika (hasa kipengele cha ngano). Kwa
ujumla nadharia hizi zinaonekana kujumuisha hata ngano za Kiswahili. Kwa hiyo
hapa katika kuzijadili nadharia hizo tutachukulia kuwa nadharia hizo baadhi
kati yake zinaweza kutumika katika kuchambua ngano za Kiswahili. Okpewho
(1992:164-181) na pia Finnegan (1970:315-334) wanajadili nadharia mbalimbali
zinazolinda fasihi simulizi za kiafrika hasa ngano kama ifuatavyo:
Mosi, nadharia ya ubadilikaji
taratibu, (Evolutionism). Nadharia hii iliasisiwa na mwanabiolojia wa
Kiingereza Charles Darwin na
baadaye kuungwa mkono na wananadharia wa Kiingereza kama Edward Burnet Tylor, James George Frazer na
Andrew Lang. Pamoja na kwamba asili ya nadharia hii ni mawazo ya
kisayansi hasa biolojia, wanafasihi simulizi wanaitumia wakidai kuwa masimulizi
tunayoyasikia hivi leo ni ubadilikaji wa taratibu kwa miaka mingi. Wataalamu
hudai kuwa tafiti nyingi zinaonesha kuwa masimulizi mengi ya kiafrika hasa ngano
hufanana kwa kiasi fulani, hii ni uthibitisho kuwa masimulizi haya yana asili
moja kwa miaka mingi iliyopita. Inasemekana kuwa usimulizi wa msingi wa ngano
hizi ulikuwa mmoja lakini kutokana na ubadilikaji taratibu kila jamii imekuwa
ikiongeza vikorombwezo kadhaa katika masimulizi kutoka kizazi kimoja hadi
kingine. Ili kuhahikikisha kuwa masimulizi haya yanabaki imara, jamii zimekuwa
zikiaminishwa kuwa masimulizi mengi ni ya kweli lakini katika hali halisi,
masimulizi haya hutokana na kuendelea kukarabati masimulizi ya mwanzo.
Nadharia hii ina udhaifu
katika kuamini kuwa fasihi simulizi za kiafrika zinachukuliwa kuwa hazina
mwenyewe, lakini ukweli ni kwamba fasihi simulizi za kiafrika ni mali ya jamii
nzima, japo si kweli kwamba kila mtu katika jamii anaweza kuwa fanani kwa
kiwango kile kile sawa na fanani mwingine.
Nadharia ya msambao au uenevu (Diffusionism). Nadharia hii iliasisiwa na
wataalamu kama Jacob na Wilhelm Grimm,
baadaye mawazo yao yakaendelezwa na Max
Muller. Mtaalamu mwingine ni Mmarekani
Steve Thompson. Pamoja na kuwepo tofauti ndogondogo za wataalamu wa
nadharia hii, mawazo yao yanalenga kueleza kuwa kuna kitovu cha fasihi simulizi
dunia nzima. Kwa sababu ya jamii kuingiliana kutokana na sababu mbambali,
masimulizi haya yalianza kuhama kutoka jamii moja hadi nyingine hasa kutoka
kwenye jamii zilizostaarabika kimaisha kwenda kwenye jamii ambazo
hazijastaarabika. Waataalamu hawa walisema kwamba kukitokea kufanana kati ya
hadithi moja toka jamii mbili tofauti basi jamii hizo zilipata kuwasiliana na
kuathiriana kwa upande wa utamaduni. Hapa wataalamu kama Jacob na Wilhelm
walisema kuwa kama kuna kufanana kokote kwa ngano za kiafrika na ulaya, basi
ngano za kiafrika ni chipukizi toka kwa wazazi wenye utamaduni wa India na
Ulaya.
Tukichunguza ngano za
Kiswahili kwa jicho la nadharia hii, tunaweza kusema kuwa ngano nyingi
zinaonekana kufanana kutoka jamii mbalimbali za waswahili hivyo kuna uwezekano
wa kuwepo kwa kitovu cha usimulizi huu katika jamii fulani. Lakini nadharia hii
ina upungufu mkubwa hasa kwa kupuuza utu na utamaduni wa mwafrika, inapodai
kuwa mwafrika alikopa ngano kutoka kwa mzungu na mhindi inaelekea kusema kuwa
mwafrika kabla ya kuwa na mahusiano na watu hawa hakuwa na utamaduni suala
ambalo ni la kibaguzi zaidi.
Nadharia ya kisosholojia.
Nadharia hii iliasisiwa na Bronislaw Malinowski (1922, 1926) na
kuwa na wafuasi kama Edmund Leach, Raymond Firth, William Bascom
na kadhalika. Mtazamo wa nadharia hii ni kuwa ngano za kiafrika zipo na
kuibuka kwa sababu ya utumizi katika jamii. Watafiti hawa kama wanasosholojia,
waliamua kuchunguza vipera vya fasihi simulizi (na ngano zikiwemo) kwa upekee
wa kila jamii. Walichunguza mila na desturi kwa kuzingatia uamilifu wake katika
jamii. Wataalamu mbalimbali kwa kutumia nadharia hii waligundua kuwa ngano za
kiafrika zina majukumu muhimu katika jamii husika kwa mfano, Jan Vansina katika
kuzijadili simulizi za utawala wa Waganda aligundua kuwa simulizi hizo
zinaakisi utawala wa kurithi unaolinda umoja wa jamii ya Waganda. R.G. Willis katika kuchanganua ngano za
kihistoria za Wafipa wa Tanzania, anatumia ufafanuzi wa kiishara kugundua
mihimiri miwili ya kimaendeleo katika jamii. Adward Shorter (1969) alifanya utafiti kwa Wakimbu wa Tanzania
akagundua kuwa ngano za Wakimbu ni muhimu sana kwa kuhifadhi vipindi mbalimbali
vya kihistoria katika jamii husika.
Nadharia hii katika ngano za Kiswahili
tunaweza kusema kuwa maisha ya jamii za waswahili ndiyo yanayozifanya ngano
ziwepo kutokana na matumizi mbalimbali kijamii. Kazi za ngano katika jamii za
waswahili huwa mhimili wa kuwepo ngano hizo bila kupotea.
Nadharia ya urasimi (formalism). Kwa kiasi kikubwa nadharia
hii ilikuja kupiku ile ya msambao au uenevu. Zote zililenga kuvunjavunja ngano
ili kuona vipengele vinavyoiunda. Wakati nadharia ya msambao ikilenga
kuivunjavunja ngano katika vipengele vyake na hatimaye kuanza kutafuta mahali
ilipoanzia na hatimaye kuunda ngano chanzi, nadharia ya urasimi yenyewe iliona
huu ni upotezaji wa muda na nguvu kwani yote haya yaliishia kuleta utata
kimgawanyo. Wanaurasimi wao waliona kuna haja ya kuchunguza jinsi vipengele
hivi vya ngano vimepangika kimfuatano katika kuiunda ngano yenyewe kuliko
kuanza kuhangaika kutafuta dhamira na hatimaye kusema chimbuko la ngano.
Mwaasisi wa nadharia hii ni mrusi aitwae Vladimir Propp (1928) na baadae
kufuatiwa na Eleazer Meletinsky, Marion Kilson na Alan Dundes. Kwa kupanua
mawazo ya Propp, Dundes (1971) baada ya kuzichunguza ngano za Uganda hasa
zile zinazohusisha wahusika wajanja kama sungura na kobe, aligundua kuwa ngano
hizi zina dhima tano. Mosi, zile za urafiki zinazoonesha umoja na mshikamano
katika kudumisha urafiki, pili zile za mvutano unaolenga kupima urafiki. Tatu,
zile ngano zinazoonesha kuharibu urafiki. Hizi ni ngano zinazoonesha kundi moja
la urafiki kuonesha hali ya kuharibu uaminifu katika urafiki hasa kwa
kuwadanganya wenzao. Nne, ngano zinazoonesha ugunduzi yaani upande wa urafiki
uliodanganywa hugundua ujanja na uongo uliofanywa na kundi jingine katika
kuharibu uaminifu. Tano, ni ngano zinazoonesha mwisho wa urafiki. Ngano hizi huonesha hatima ya kuvunjika kwa
urafiki wa makundi na mara nyingi huishia kutoa adhabu kwa mwanzilishi wa
uhasama.
Nadharia hii katika ngano za Kiswahili
tunaweza kusema, inamaanisha kuzielewa ngano hizi kwa kuchunguza jinsi ngano
hizi zinavyoweza kuvunjwavunjwa katika vipengele vyake na hivyo kubainisha
muundo wake.
Nadharia ya uhulutishi (hybridization). Nadharia hii ina
wafuasi wengi wa kiafrika kwa mfano Ngugi wa Thiong’o, Chinua Achebe, Frantz
Fanon na wengine. Mtazamo mkuu wa nadharia hii ni kuangalia namna
ambavyo nadharia zingine zinaweza kufaa na kushirikiana katika kuchunguza
fasihi simulizi za kiafrika. Hawa walilenga kuchunguza fasihi simulizi ya
mwafrika kwa kuangalia uzuri unaojitokeza katika kazi za waafrika wenyewe.
M.M.Mulokozi ni mfuasi wa nadhari hii kwa Tanzania. Mawazo ya wanauhulutishi
yanajibainisha kwa kutoa matamko kadhaa wanayoyatoa kuihusu fasihi simulizi ya
mwafrika, kwa mfano wanasema kuwa kuna haja ya kutojali mwonekano na uzuri wa
nje wa fasihi na kujali zaidi utendekaji ambao umejikita kwenye utendaji halisi
wa msanii na hadhira yake kifani na kimaudhui, utendekaji unatakiwa uwe na
uwili unaokamilishana yaani usielekee tu kwenye utamu bali uwe sanjali na
hadhira na mazingira yao, ni kosa kubwa kwa waafrika kuiga mambo bila kuchukua
tahadhari ya kujua kama wayaigayo yanawafaa katika jamii zao, pia fasihi
simulizi si sanaa ya kimapokeo isiyo na upya wowote bali inapaswa kutiwa
ubunifu ulio hai.
MAREJEO
F. E. M. K. Senkoro (1982) Fasihi. Press and Publicity Centre. Dar
es Salaam.
F. Ruth (1970) Oral Literature in Africa. Oxford: Clarendon Press
K. W. Wamitila
(2004) Kichocheo cha Fasihi, Simulizi na
Andishi. Focus Publications Limited: Nairobi
M.M. Mulokozi (1989) Tanzu za fasihi simulizi. Katika Mulika.
Na 21
M. Msokile (
1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi.
E.A.E.P. Nairobi
P.Mhando na N.Balisidya (1976) Fasihi na sanaa za maonyesho. T.P.H.
Dar es Salaam
S. Okpewho (1992) African Oral Literature. Backgrounds, Character, and Continuity.
Indiana University Press. U.S.A