Wanasiasa watakiwa ‘kuvaa viatu’ vya Filikunjombe
Rais Jakaya Kikwete akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa marehemu aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deogratius Filikunjombe katika Hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam jana. Picha na Said NgÕamilo
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana
aliongoza waombolezaji kuuaga mwili wa mgombea ubunge wa Ludewa (CCM),
Deo Filikunjombe ambaye wanasiasa wametakiwa kuvaa ‘viatu vyake’ kuiga
mema aliyokuwa anayatenda.
Filikunjombe na wenzake
watatu walifariki dunia Alhamisi kwenye ajali ya helikopta iliyotokea
katika Hifadhi ya Selous mkoani Morogoro. Wengine waliofariki kwenye
ajali hiyo ni rubani Kepteni William Silaa, Francis Nkwera na Pladsus
Ngabuma Haule.
Walioagwa jana pamoja na Filikunjombe ni
Nkwera na Haule. Kepteni Silaa ambaye ni baba mzazi wa Meya wa Manispaa
ya Ilala Jerry Silaa, naye anatarajiwa kuzikwa leo.
Wakitoa
salamu za rambirambi katika Hospitali ya Lugalo, viongozi mbalimbali
walioambatana na Rais Kikwete kuaga miili hiyo, walisema Filikunjombe
alikuwa mpiganaji, mpenda haki na mwenye upendo, hivyo viongozi
waliobaki wanatakiwa kuvaa viatu vyake.
Spika Anne
Makinda alisema viongozi na wananchi wote kuishi kwa upendo kwa kuwa
duniani wote ni wapitaji, huku akihimiza familia yake kuiga tabia njema
aliyokuwa nayo marehemu.
“Fanyeni aliyotaka Deo,
msibadilishe, mtakuwa mnamchukiza huko aliko, pia niwaambie ndugu zangu
mliopo hapa, hii dunia ni mapito, tuache roho za chuki na kufitiniana,
tuishi kwa kupendana kwani hapa duniani tunapita,” alisema.
“Alikuwa
mtu wa msimamo, alifanya kazi na watu wote hata vyama vya upinzani
katika kusimamia masilahi ya umma, aliwapenda watu na Taifa lake, hakika
ni wa kuigwa kwa aliyoyafanya,” alisema January Makamba wakati akitoa
salamu kwa niaba ya CCM.
Makamba alisema hili ni pengo
kwa CCM, wabunge waliopo na watakaokuja ‘wavae viatu’ vya Filikunjombe
katika kueleta maendeleo ndani ya Taifa la Tanzania kwa kupigania
masilahi ya wananchi.
Mgombea ubunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila alisema Filikunjombe alikuwa mtu muhimu katika Bunge la
Tanzania, alionyesha mfano wa wabunge wanaohitajika nchini hasa katika
sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Hatuna
namna nyingine ya kumuenzi Deo zaidi ya kuendeleza yale aliyokuwa
ameanza kuyapanda, niseme kwamba Tanzania tumepoteza kiongozi,” alisema
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kwa niaba ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali waliyokuwa wanaiongoza pamoja na
Filikunjombe.
Hali ilivyokuwa
Miili
hiyo mitatu iliagwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, saa 5:00
asubuhi na baada ya kuagwa ilipelekwa nyumbani kwa marehemu
Filikunjombe, Mtoni Kijichi wilayani Temeke, kwa ajili ya ibada kabla ya
kusafirishwa kwenda Ludewa kwa mazishi yatakayo fanyika leo.
“Tumefiwa,
kwa heri Deo,” Ni kauli zilizosikika katika Hospitali ya Lugalo na
nyumbani kwa marehemu na viongozi mbalimbali walitoa salamu, huku
wakionyesha kuumizwa na kifo cha mpendwa wao.
Kijichi wamlilia
“Deo
hana muda mrefu tangu ahamie kwenye nyumba yake, lakini alikuwa mtu wa
watu, aliwajali majirani, hatuna cha kusema zaidi ya kusema tumefiwa,”
alisema Elisia Bernado, mkazi wa Kijichi.
“Amekufa Deo
basi tuamini hivyo, maana hakuna jinsi, ila kifo chake kimeniumiza, siyo
mimi pekee hata wakazi wa Kijichi,” alisema Asia Juma.