Idadi ya wapigakura siyo msingi wa vyama kushinda-Wachambuzi
Mwananchi akipiga kura
Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya
kisiasa nchini wamesema idadi kubwa ya wapigakura katika mikoa ambayo ni
ngome kuu za baadhi ya vyama vya siasa siyo msingi wa vyama hivyo
kushinda Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Wamesema
sababu za wananchi kujiandikisha kupigakura zipo nyingi, ikiwamo
kuhitaji vitambulisho vya kupigia kura kufanyia shughuli nyingine,
kusisitiza kuwa sera nzuri za vyama husika ni msingi mkuu wa ushindi.
Kauli
hiyo inakuja siku moja baada ya gazeti hili kukokotoa na kubaini mikoa
tisa yenye idadi kubwa ya wapigakura baada ya mapema wiki hii Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza idadi ya wapigakura waliojiandikisha
kuwa ni milioni 22.75 watakaogawanywa katika vituo 65,105 kila kimoja
kikiwa kimepangiwa wapigakura wasiozidi 450.
Mikoa
yenye wapigakura zaidi ya milioni moja ni Mbeya, Mwanza, Morogoro,
Tabora, Dodoma, Kagera, Tanga na Arusha huku Dar es Salaam ukiwa na
wapigakura milioni mbili.
Wakizungumza na gazeti hili
kwa nyakati tofauti Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim
alisema, “Tanzania hakuna utafiti uliotolewa unaoonyesha sababu za
wananchi kutojitokeza kupigakura. Taarifa nyingi zinazotolewa ni za
kuhisi tu.”
Alisema wapo wanaojiandikisha na kuvitumia
vitambulisho vya kupigia kura kwa shughuli nyingine, “Pia wapo ambao
hawaoni umuhimu wowote na wapo ambao hawavutiwi na sera za vyama.”
Alisema
wananchi wa sasa wanahoji ahadi na kauli zinazotolewa na wagombea ambao
hushindwa kutoa majibu sahihi wanapotakiwa kueleza mikakati
watakayoitumia kutekeleza mambo hayo.
“Ahadi pia
zimekuwa nyingi kiasi cha kuwafanya wananchi kuamini kuwa wagombea
wanataka kupigiwa kura tu maana siasa sasa ni ajira. Kifupi ni kwamba
ahadi nyingi zinazotolewa hazitekelezeki,” alisema Salim.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu (UDSM), Richard Mbunda alisema jambo la msingi la
kutazama ni idadi ya wananchi wanaojitokeza katika mikutano ya kampeni
kwa maelezo kuwa wana nafasi kubwa ya kusikiliza sera za vyama na
wagombea na kumchagua mwenye sera watakazoridhika nazo.
“Ukitaka kuthibitisha hilo tazama mijadala kuhusu sera
inayoibuka baada ya kumalizika kwa kampeni za vyama mbalimbali. Sera
nzuri ndiyo zitavipa vyama ushindi si vinginevyo,” alisema.
Mhadhiri
mwingine wa UDSM, Bashiru Ally alisema takwimu za idadi ya watu ni kitu
kingine na wanaojitokeza siku ya kupigakura ni kitu kingine na kwamba
takwimu hizo hazipaswi kuchambuliwa na watu waliovaa miwani ya vyama vya
siasa.
“Tangu Uchaguzi Mkuu wa 2010 wanaojiandikisha
kupigakura ni wengi kuliko wanaojitokeza kupigakura. Wengi hutumia
vitambulisho vyao kwa shughuli nyingine na ili kuvipata ni lazima
wajiandikishe na hakuna vitambulisho mbadala wanavyoweza kuvitumia
katika mabenki na shughuli nyingine.
“Thamani ya kura
inahusiana zaidi na utendaji wa wale wanaochaguliwa. Kama wananchi
wataona watu hao ni viongozi bora wataona thamani ya kujitokeza kwa
wingi kuwachagua,” alisema.
Alifafanua kuwa zipo sababu
nyingine za wananchi kushindwa kupigakura ambazo ni kufariki dunia,
kubanwa na shughuli nyingine muhimu na kuogopa vurugu siku ya uchaguzi.
“Pamoja
na hayo hatujawahi kuwa na rais aliyeshinda chini ya asilimia 60 na pia
hatujawahi kuwa na rais ambaye hakuchaguliwa na wananchi wote kwa maana
kila mkoa,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu
Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alitofautiana na wenzake akieleza kuwa
vyama vitapata kura nyingi katika mikoa ambayo vinakubalika zaidi.
“Sera
za chama na mgombea ni moja ya sababu ya msingi lakini kukubalika kwa
chama katika mkoa husika ni kete muhimu sana. Mfano ni mkoa wa Mwanza,
Mbeya, Dar es Salaam na Morogoro chama kikikubalika katika mikoa hiyo
kinaweza kupata ushindi.
“Morogoro ni ngome ya CCM ila
Dar es Salaam CCM na Ukawa watagawana kura. Mwanza na Mbeya pia
wapinzani wanakubalika na wanaweza kupata kura huko. Ruvuma hakuna
wapigakura wengi lakini ni ngome ya CCM. Ukifuatilia idadi ya wapigakura
katika kila mkoa unaweza kubashiri chama kitakachoshinda,” alisema.