Lowassa aionya NEC, Magufuli atambia barabara
Mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa (kushoto) na Mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM John Magufuli.
Dar es Salaam/Magu. Mgombea urais kwa
tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesifu kazi ya ujenzi wa barabara
katika miaka 10 iliyopita, huku mgombea wa Chadema, Edward Lowassa
akiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa imempotosha Rais Jakaya
Kikwete.
Dk Magufuli alisema hayo jana kwenye mkutano
wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, muda mfupi kabla
ya kwenda kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara za
juu eneo la Tazara, wakati Lowassa alitoa kauli hiyo akiwa mjini Magu.
Akizungumzia
utendaji wake kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema katika kipindi
cha Serikali ya Awamu ya Nne pekee, Wizara ya Ujenzi aliyokuwa
akiiongoza, imefanikiwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za urefu
wa kilomita 17,762 na akaahidi kuendelea na kasi ya ujenzi atakapopata
fursa ya kuchaguliwa kuwa Rais.
“Kuwepo kwa barabara za
lami ndiyo ujenzi wa uchumi imara,” alisema Dk Magufuli. “Leo mnasikia
huko Mara kuna watu waliamua kudeki barabara ili mgombea wa chama fulani
aweze kupita. Kwanza nawapongeza sana wale vijana kwa kazi ile ya
kudeki barabara kwa sababu zingekuwa za changarawe wasingeweza kufanya
usafi wa kiwango kile.”
Pia, aliwataka wananchi
wasidanganyike na kauli za baadhi ya wagombea kuwa watamaliza tatizo la
foleni jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku 100, akisema hizo ni sawa
na ndoto za mchana.
“Hakuna mwenye miujiza ya kuiondoa
foleni kwa siku 100, anayedai ataweza anawadanganya. Ujenzi wa barabara
za juu siyo jambo la siku moja, ni suala lenye taratibu na mipango yake
na tayari Serikali imeshaianza.
“Leo ninapotoka hapa
nakwenda kuweka saini makubaliano ya kuanza kwa ujenzi wa flyovers za
Tazara na pale Ubungo, tayari tumepata fedha kutoka kwa wahisani.
Tunasubiri kuanza ujenzi wa barabara yenye ghorofa tatu, ya juu, kati na
ya chini.”
Dk Magufuli alishambulia makada waliowahi
kushika nyadhifa kubwa serikalini ambao wanaiponda Serikali kuwa
haijafanya chochote, akisema wengine hawakustahili nafasi hizo.
Pia,
alisema vyama vya CCM na Chadema vyote vina mafisadi, lakini akasema
waliokuwa chama hicho tawala wameanza kukimbia baada ya yeye kuteuliwa
kuwa mgombea urais.
“Mafisadi hawapo Chadema pekee,
wapo pia CCM na ndiyo hao mnawasikia kila kukicha wanakimbia na
mtawasikia na kuwaona wakiendelea kukimbia. Nawahakikishia wataendelea
kukimbia maana wananijua mimi sina mchezo. Hapa ni kazi tu,” alisema.
Lowassa aishangaa NEC
Mjini
Magu, Lowassa amekuwa mmoja wa watu waliostushwa na idadi ya wapiga
kura iliyotamkwa na Rais Kikwete na akaitupia lawama NEC kuwa ndiyo
iliyompotosha mkuu huyo wa nchi.
Rais Kikwete,
aliyekuwa akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 16 ya kifo cha
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere juzi mjini Dodoma, alitaja idadi ya
wapigakura walioandikishwa na NEC kuwa milioni 28 wakati idadi
iliyotangazwa na tume hiyo ni milioni 22.75.
Jana, Lowassa aliyekuwa akihutubia kwenye mkutano wa
kampeni uliofanyika Uwanja wa Sabasaba mjini Magu, alisema kuna kazi
kubwa kwa NEC kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
“Tume
ina kazi kubwa sana, wasipoangalia watavuruga uchaguzi na ukivurugwa ni
mwanzo wa matatizo katika nchi,” alisema waziri huyo mkuu wa zamani.
“Sielewi
inakuwaje Rais anapewa takwimu halafu baada ya saa mbili zinakanushwa?
Ni nani anampa Rais takwimu hizi? Tulisema tume ni huru, sasa kwa hali
hii ni huru?”
Muda mfupi baada ya hotuba ya Rais, Ikulu
ilitoa taarifa ikisema uhakika wa idadi hiyo ni 22,751,292 kwa Bara na
503,193 Zanzibar.
Lowassa, ambaye jana alifanya
mikutano mitatu katika majimbo ya Magu, Misungwi, Sumve na Sengerema,
aliitaka NEC isifanye mambo yatakayoharibu uchaguzi.
Mgombea
huyo, ambaye pia hujinadi kwa kufanikisha mradi wa maji ya Ziwa
Victoria, aliahidi kuwaletea wakazi wa Magu maji ya ziwa hilo ili
kuwaondolea usumbufu. Alisema yeye ni mtaalamu wa masuala ya maji na
wakimpa kura, atakamilisha ahadi yake kwenye mji huo.
Mkazi wa Magu, John Chacha alisema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na kwamba wananunua dumu moja kwa Sh800.
Alisema
tatizo jingine ni maeneo ya kilimo kuchukuliwa na Serikali na kugeuzwa
kuwa hifadhi na kusababisha wananchi kukosa maeneo ya kilimo.
Mkazi mwingine, Filipo Lucas alitaka kuimarishwa kwa huduma za afya pamoja na elimu.
Hata
hivyo, alilalamikia kitendo cha walimu kuagiza wanafunzi kupeleka
mahindi shuleni pamoja na mlolongo wa michango shuleni, ambayo alisema
inakwaza maendeleo ya elimu.
Kabla ya kumkaribisha
Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliendelea kupinga kauli
ya Rais Kikwete ya kuwataka wananchi kurudi nyumbani baada ya kupiga
kura.
“Mimi nasema, tuko tayari kupigwa, lakini
hatuondoki mpaka matokeo yatoke. Hatutaki kura za maruhani,” alisema
Mbowe huku akiwataka polisi kutenda haki kwa kuwa hawana mpango wa
kufanya fujo zaidi ya kulinda kura.
Kingunge Ngombale Mwiru alimsifu Balozi Juma Mwapachu kwa hatua yake ya kuihama CCM
a amefanya uamuzi sahihi.