CCM, Chadema ‘wakwepa’ mdahalo wa urais
Wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli, pamoja na Edward Lowassa wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameshindwa kushiriki
mdahalo maalum wa wagombea urais ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza
pamoja na wadau wengine.
Mdahalo huo ambao umefanyika
kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo,
ulirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star TV. Anna
Mghwira kutoka Chama cha ACT-Wazalendo na Chief Lutasola Yemba wa ADC na
mgombea kutoka CHAUMMA, Hashim Rungwe ndiyo wagombea pekee wa urais
waliopewa mualiko rasmi na kushiriki mdahalo huo.
Hata
hivyo, Rungwe alifika wakati mdahalo huo ukiwa unaelekea ukingoni ambapo
awali ilitaarifiwa kuwa angefika kwa kuchelewa kwa kuwa wakati mdahalo
umeanza yeye ndio alikuwa akiwasili Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere
akitokea Mtwara.
Katika mdahalo huo, maswali
mbalimbali yaliulizwa ikiwemo dhana nzima ya mabadiliko ambayo awali
ilikuwa ikitumiwa na Chadema kisha kuenea kwenye vyama vingine, imepata
tafsiri tofauti kutoka kwa wagombea urais wa ACT-Wazalendo Anna Mghwira
na Chief Yemba wa ADC.
Kwa mujibu wa Mghwira, dhana ya
mabadiliko katika ACT-Wazalendo ni hoja mbadala inayolenga
kushughulikia matatizo ya jamii. Alisema ACT-Wazalendo imebuni mikakati
madhubuti wa kuongeza uzalishaji kupitia rasilimali za nchi kama vile
misitu, madini na uwekezaji kwenye kilimo.
“Matumizi
bora ya rasilimali na uwekezaji katika kilimo vitasaidia kuongeza pato
la taifa na hivyo itarahisisha utoaji wa huduma bora za jamii kama vile
elimu na afya,” alisema Mghwira.
Kwa upande wake,
Chief Yemba alisema dhana ya mabadiliko kwa mujibu wa ADC ni kuondoa
maradhi, ujinga na umasikini. Alisema mabadiliko siyo kuiondoa CCM
madarakani na kisha kuiongoza nchi kwa misingi ileile ya CCM.
Kuhusu
Muungano, Chief Yemba alisema ADC itapitia kero zote ili Muungano uweze
kutoa haki sawa kwa watu wote tofauti na ilivyo sasa. Alisema Muungano
unapaswa kusimamia na kutekeleza hoja ya haki sawa kwa wote kama vile
kutoa huduma za jamii kwa usawa kwa pande zote za Muungano.
“Sisi
ACT-Wazalendo tunasema Muungano ni lazima utokane na ridhaa ya wananchi
kikatiba tofauti na ilivyo sasa. Hoja za wananchi kudai serikali ya
Tanganyika au Zanzibar yenye mamlaka kamili, zinaonyesha wazi kwamba
Muungano tulionao unahitaji marekebisho ili wananchi wenyewe waridhie,”
alisema Mghwira.
Mgombea urais kupitia Chama cha TLP,
Maxmilian Lyimo, pamoja na kwamba hakuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye
mdahalo huo, alipata fursa ya kujibu baadhi ya hoja za wananchi kama
vile afya bora. Alisema serikali yake haitafanya dawa kweye hospitali za
umma kuwa bidhaa adimu kama ilivyo sasa.