Serikali yaanza kulipa madeni ya walimu
Mwalimu wa shule ya msingi akifundisha darasani
-
Sengerema. Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, imeanza kulipa madeni ya walimu yanayofikia Sh162.1 milioni.
Ofisa
Elimu ya Msingi wa wilaya hiyo, Oscar Kapinga alisema juzi kuwa hatua
hiyo inatokana na Serikali kusikia kilio cha muda mrefu cha walimu
kuhusu madeni yao.
Kapinga alisema kabla ya uhakiki
madeni ya walimu yalikuwa Sh276.4 milioni kwa idara za elimu ya msingi
na sekondari, lakini baada ya uhakiki ilibainika yaliyokuwa halali ni
Sh162.1 milioni.
Alisema kwa Idara ya Elimu ya Msingi
pekee, walimu walikuwa wanadai Sh130 milioni ambazo zimeanza kulipwa na
kwamba, madeni hayo hayahusu mishahara bali ni malimbikizo ya likizo,
uhamisho, masomo, wastaafu, mazishi na matibabu.
Ofisa
huyo alisema halmashauri itaendelea kulipa madeni hayo kwa wakati ili
kuondoa kero za walimu zinazotokana na kudai malimbikizo mbalimbali.
Aliongeza
kuwa licha ya malipo hayo, Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara ya
Januari, Mei, Juni na Agosti huku walimu 591 wakilipwa Sh141 milioni.
Aliwataka walimu kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuwa Serikali imesikia kilio chao.
Katibu
wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Sengerema, Luhumbika
Francis alisema licha ya kuanza kulipwa madeni hayo, wanaidai Serikali
zaidi ya Sh800 milioni zikiwa ni fedha za malimbikizo ya mishahara.