Mwanamke aliyetekwa nyara Kenya aokolewa
- 16 Oktoba 2015
Wanajeshi wa Kenya
na Somalia wamefanikiwa kumuokoa mwanamke aliyekuwa ametekwa nyara
katika eneo la Dadaab, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Operesheni hiyo imeshirikisha majeshi ya Kenya, kikosi cha polisi wa utawala Kenya, na wanajeshi wa Somalia.
Bi Mutua, aliyetekwa nyara Oktoba 12 na watu wasiojulikana, anapokea matibabu na atasafirishwa hadi Nairobi baadaye leo, Kanali Obonyo amesema.
Ameongeza kuwa mtekaji nyara mmoja ameuawa na mwingine kukamatwa.
Mkuu wa usalama wa serikali ya Kenya eneo la Kaskazini Mashariki Mohammud Swaleh amesema Bi Mutua alipelekwa mji wa Dobley kwenye mpaka wa Kenya na Somalia baada ya kuokolewa.
Ingawa kundi ya al-Shabab halijadai kuhusika katika utekaji nyara huo, Kanali Obonyo amedai ndio waliohusika katika utekaji nyara huo kwenye taarifa yake.
Bi Mutua alikuwa akifanya kazi na shirika shirika lisilo la kiserikali la Windle-trust, moja ya mashirika yanayohudumu katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, inayotoa hifadhi kwa takriban wakimbizi 450,000 kutoka Somalia.