Vijana kete muhimu kupata urais 2015
ya urais ashinde
Dar es Salaam. Wiki moja kabla ya Uchaguzi
Mkuu imebainika kwamba, ili mgombea yeyote wa nafasi ya urais ashinde
kiti hicho ni lazima awe na ushawishi mkubwa kwa vijana, hasa wa kike.
Taarifa
iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiainisha idadi ya watu
waliojiandikisha kiumri, inaonyesha kuwa asilimia 57 ya wapigakura wote
waliojiandikisha na kuthibitishwa kupigakura Oktoba 25, wana umri chini
ya miaka 35.
Taarifa hiyo ambayo imewagawa wapigakura
wote 22.75 milioni kwenye makundi matatu; miaka 18 mpaka 35; 36 mpaka 50
na 51 na kuendelea, inaonyesha mshindi wa urais ni lazima alishike
kundi hilo ili aibuke kidedea wakati kinyang’anyiro hicho kitakapokuwa
kinahitimishwa.
Taarifa hiyo ambayo imewagawa
wapigakura wote 22.75 milioni kwenye makundi matatu; miaka 18 mpaka 35;
36 mpaka 50 na 51 na kuendelea, inaonyesha mshindi wa urais ni lazima
alishike kundi hilo ili aibuke kidedea wakati kinyang’anyiro hicho
kitakapokuwa kinahitimishwa.
Kati ya wapigakura wote
waliopo, vijana wenye umri kati ya 18 na 35 ni 12,894,576. Kati yao
wanaume ni 6,155,613 (asilimia 27) na wanawake ni 6,738,964 ( asilimia
30) ya wapigakura wote waliojiandikisha mwaka huu.
Hii
ina maana kwamba, endapo kundi hili lote litamuunga mkono mgombea mmoja
na kumchagua, basi atashinda kwa asilimia 57 na ambazo haziwezi
kupatikana kwa rika nyingine zilizobaki.
Takwimu hizi
zinadhihirisha mikakati ya ziada, ambayo vyama husika inatakiwa kuwa
nayo ili kuongeza wafuasi na kujihakikishia ushindi.
Mchanganuo
huo unaonyesha zaidi kuwa watu wa rika ya kati, kati ya miaka 36 mpaka
50 hawafiki hata nusu ya vijana hawa, kwani wapo 5,690,668. Hiyo ni
asilimia 25 ya wote waliojiandikisha. Wao wanajumuisha wanaume 2,744,422
(asilimia 12) na wanawake 2,946,247 (asilimia 13) ya wapigakura wote.
Makundi
haya mawili pekee yanatengeneza asilimia 82 ya wapigakura wote huku
asilimia 18 zinazosalia yaani wapigakura 4,165,544 zikiwa ni za wazee.
Kwa wazee hawa, wamo wanaume 1,900,555 au asilimia nane ya wanawake 2,264,990 ambao ni asilimia 10.
Akizungumzia
takwimu hizo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(Udsm), Dk Benson Bana alisema kuna haja kwa washauri na wagombea
kuzitumia vizuri taarifa hizi katika kunadi sera zao, kwani kila kundi
lina mahitaji yake maalumu na ndani yake pia yapo madaraja.
Alifafanua
kwamba haitoshi kusema vijana au wanawake wanajitokeza kwa wingi bila
kueleza ni kwa namna gani kero zao zitataliwa, endapo chama au mgombea
husika atapewa ridhaa na kundi hilo.
“Ni vigumu
kutabiri misimamo ya kiitikadi ya kundi hili. Inaweza kuwa rahisi kujua
wanafunzi wa vyuo wanahitaji nini kwa sababu mawazo na mitizamo yao ni
kama huwa inafanana, lakini haiwezekani kwa wale wanaofuga, kulima au
waliojiajiri.
Ni muhimu sera zikabainisha zitafanya
nini na wajane, wasio na ajira, wajasiriamali na makundi mengineyo ndani
ya lile la vijana,” alisema Dk Bana.
Profesa Gaudence
Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), alisema kuna umuhimu
wa kila kundi kushiriki kwa mapana kwenye mchakato wa uchaguzi ili kuwa
na nafasi nzuri ya kufanya uamuzi unaostahili. Alisema ingawa ipo dhana,
inayohitaji kufanyiwa utafiti, kwamba wanawake wanaipenda CCM na vijana
upinzani bado haitoshi kujiaminisha juu ya ushindi.