Filikunjombe, rubani makada CCM wafa katika ajali ya helikopta
Marehemu Deogratius Filikunjombe, aliyekuwa Mgombea ubunge jimbo la Ludewa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
-
Mgombea ubunge jimbo la Ludewa kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) Deogratius Filikunjombe, rubani na abiria wengine wote
wamekufa baada ya helkopta kuanguka na kuteketea katika hifadhi Selou.
Jeshi
la Polisi pamoja na Bunge limethibitisha leo mchana kutokea ajali hiyo
mbaya na miili ya marehemu inasubiriwa uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, Meya
anayemaliza muda wake wilaya ya Ilala, Jerry Silaa amempoteza baba yake
mzazi, William Silaa ambaye ndiye aliyekuwa akirusha helkopta hiyo
iliyoanguka jana jioni.
Kabla ya vyombo hivyo viwili
kuthibitisha kutokea vifo hivyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu aliiambia Mwananchi Digital kuwa ilikuwa inawawia vigumu kupata
taarifa kutoka katika timu ya uokoaji kutokana na mazingira ya ajali
kuleta utatanishi.
“Timu ya uokoaji inashughulikia
suala hilo. Ila hatuwezi kusema iwapo wamefariki wote ama la kwa amana
helkopta imeungua na pia ile ni mbuga, kuna wanyama wakali,” Waziri
amesema.
Hata hivyo, katika kurasa za Twitter na
Instagram za Meya Silaa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, January Makamba
zilitoa rambirambi hata kabla ya Jeshi la Polisi kuthibitisha vifo
katika hifadhi hiyo kubwa nchini.