Coastal Union kujiuliza kwa Kagera Sugar
Kagera Sugar
Dar es Salaam. Coastal Union haijawahi
kushinda katika michezo sita iliyocheza hadi sasa na itabidi iingie
uwanjani leo kusaka ushindi wake wa kwanza mbele ya Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Mechi nyingine za
leo za Ligi Kuu Tanzania Bara ni kati ya Prisons itakayokuwa ugenini
kuikabili Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Ndanda
watakuwa wenyeji wa Toto African kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona,
wakati Majimaji watacheza na African Sports kwenye Uwanja wa Majimaji
mjini Songea.
Coastal Union inashika nafasi ya pili
kutoka mkiani ikiwa na pointi tatu, lakini si tu haijawahi kushinda
mechi yoyote, lakini haijawahi hata kufunga hata bao la kuotea tangu
kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kinachofurahisha ni
kuwa kati ya michezo sita iliyocheza Coastal Union, mitatu imecheza
kwenye uwanja wake wa nyumbani wa CCM Mkwakwani na ndiyo hiyo
iliyowapatia pointi tatu baada ya kutoka sare tatu, hivyo Mtibwa Sugar
wanapaswa leo kujipanga kuwakabili.
Kocha wa Coastal,
Union Jackson Mayanja aliliambia gazeti hili kuwa watahakikisha
wanashinda mchezo wa leo ili kupata ushindi wao wa kwanza kwani
wamechoka kuwa wasindikizaji tangu ligi ianze.
“Tunacheza
nyumbani na Mtibwa, ni timu ngumu, kwani ipo nafasi za juu kwenye ligi,
hivyo haitakuwa kazi rahisi, lazima tupambane hasa kuhakikisha
tunashinda mchezo huo.
“Tangu tumeanza ligi tumekwenda kwa kusuasua, hivyo wachezaji wangu hawana budi kukomaa kesho (leo),” alisema Mayanja.