Mwalimu ampiga mwandishi
Mwalimu
Willibroad Samson wa Shule ya Sekondari Kitunda iliyopo Wilaya ya
Ilala, akimdhibiti mwanafunzi, Elia Simion aliyekuwa akipigana na
mwenzake. Picha na Tumaini Msowoya
-
Dar es Salaam. Mwandishi wa Mwananchi,
Tumaini Msowoya jana alipigwa ngumi kadhaa kichwani na mwalimu wa Shule
ya Sekondari Kitunda wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Msowoya
alipigwa na mwalimu aliyefahamika kwa jina la Willibroad Samson
alipokwenda shuleni hapo kufuatilia madai kwamba baadhi ya wanafunzi wa
shule hiyo, wiki iliyopita waliandikishwa na kupewa vitambulisho vya
kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi, Msowoya alisema kwamba tukio hilo lilitokea
kati ya saa 4.30 na saa 5.00 asubuhi karibu na jengo la ofisi za walimu.
“Nilifika shuleni pale saa 3.00 asubuhi kwa ajili ya kuonana na mkuu wa
shule, sikumkuta ila nilipokewa na makamu mkuu wa shule. Lakini wakati
nikiendelea na mazungumzo ofisini kwa mwalimu huyo tulisikia wanafunzi
wakipiga kelele,” anasema Msowoya.
Alisema kuwa
alipotaka kutoka nje baada ya kukamilisha mazungumzo na makamu mkuu wa
shule alisikia kelele zikipigwa huku mawe yakirushwa na kupiga jengo la
ofisi ya walimu wa shule hiyo. “Hivyo tukaufunga mlango na baada ya muda
mfupi nilitoka nje na kushuhudia wanafunzi wawili wakipigana huku
wenzao wakishangilia,” alisema.
Kwa mujibu wa Msowoya,
alianza kupiga picha za tukio hilo, na punde alimwona mwalimu Samson
akiamulia wanafunzi waliokuwa wanagombana. Pia, alimwona mwalimu huyo
akimdhibiti Elia Simion, mmoja wa wanafunzi wa kidato cha kwanza
waliokuwa wanapigana huku akitoka damu mdomoni baada ya kupigwa na
mwenzake.
Katika tafrani hiyo, Msowoya alisema mwalimu
huyo alimpiga huku akimvutia katika ofisi ya walimu, lakini walimu
wengine waliingilia kati kumzuia.
Kutokana na kipigo
hicho, alitoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kitunda ambako alipewa fomu
ya PF3, kisha akapatibiwa katika Zahanati ya Kitunda.
Alipoulizwa
makamu mkuu wa shule aliyejitambulisha kwa jina moja la Masatu
kuhusiana na tukio hilo alikiri kushuhudia lakini akasema mwalimu
aliyefanya tukio hilo anajitolea kufundisha, siyo mwajiriwa wao.
Mwalimu
Samson alipoulizwa sababu za kumpiga mwandishi alisema kuwa
alikasirishwa na kitendo cha kupigwa picha wakati akiamulia ugomvi wa
wanafunzi. Hata hivyo, kuhusu madai kwamba wanafunzi waliandikishwa na
kupewa vitambulisho kwa ajili ya kupiga kura, Masatu alikanusha akidai
wanafunzi walipigwa na kupewa vitambulisho vya shule ambavyo mpigaji ni
mtu binafsi.