Magufuli akubali, Lowassa achomoa mdahalo
Dar es Salaam. Siku moja kabla ya kufanyika
kwa mdahalo wa wagombea urais nchini, Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) umesema mgombea wao kupitia Chadema, Edward Lowassa hatashiriki
shughuli hiyo huku CCM ikithibitisha mgombea wake, Dk John Magufuli
kushiriki.
Kitendo cha Lowassa kutokuwapo katika
mdahalo huo utakaofanyika kesho saa 7:30 mchana hadi saa 10 jioni,
kutapunguza ushindani miongoni mwa wagombea wakuu wawili ambao
wanachuana vikali katika uchaguzi unaotajwa kuwa wa kihistoria.
Licha
ya vyama vinane kusimamisha wagombea urais, vinavyochuana zaidi ni
Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa na CCM, huku ACT-Wazalendo ikionekana
kuleta upinzani.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum
Mwalimu aliliambia Mwananchi jana kuwa, kwa sasa mgombea wao yupo katika
Kanda ya Ziwa kwenye kampeni, hivyo itakuwa ngumu kuhudhuria mdahalo
huo unaosubiriwa kwa hamu.
Hata hivyo, wakati Lowassa
akikosekana katika mdahalo huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan
Eyakuze alisema hadi jana vyama vinne vilikuwa vimethibitisha ikiwamo
CCM.
Vyama vingine vitakavyoshiriki mdahalo huo kwa
mujibu wa Eyakuze ni Alliance for Democratic Change (ADC), ACT-Wazalendo
na Chaumma.
Alisema jana walipokea barua ya
uthibitisho kutoka CCM ikisema itashiriki, hivyo kuongeza idadi ya vyama
vitakavyochuana hadi kufikia vinne kati ya vitano ambavyo vilikidhi
vigezo vya kushiriki mdahalo.
“Tunatarajia atakuwapo Dk John Magufuli katika mdahalo
wetu na bado tunaendelea na mazungumzo na Ukawa ili watupatie majibu kwa
maandishi kama watashiriki au la.
“Mlango wetu utakuwa
wazi kuhakikisha tunawapatia fursa ya kujibu maswali ya wananchi
watakayowauliza, lakini tumeshaeleza kuwa watakaoshiriki mdahalo huu ni
wagombea wa urais na siyo vinginevyo,” alisema Eyakuze.
Hata
hivyo, Mwalimu alisema suala la muda ni kikwazo kwao kitakachofanya
mgombea wao kutoshiriki mdahalo huo ulioandaliwa na Twaweza, Tanzania
Media Foundation (TMF), Taasisi ya CEO roundtable na Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).
“Huwezi kumwondoa
mgombea kwenye kampeni aende kwenye mdahalo akatumie siku mbili
kujiandaa na kusafiri bila kuwafikia wananchi vijijini ambao wanamsubiri
kwa hamu, kifupi sisi tunawatakia kila la kheri,” alisema Mwalimu kwa
njia ya simu.
Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi,
Uendeshaji na Utawala wa ADC, Jumanne Magafu alipendekeza maboresho ya
sheria ya uchaguzi ili midahalo iwe sehemu ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu
siku zijazo.
Alisema kwa sasa hakuna sheria wala kanuni
zinazowalazimisha watu muhimu kama wagombea wa urais kuhudhuria
midahalo na kujibu maswali ya wananchi, jambo ambalo huwa ni adimu
katika mikutano yao ya kampeni.
“Tunaendelea kujiandaa
vizuri na mdahalo huu, mgombea wetu wa urais, Anna Mghwira kwa sasa yupo
kwenye kampeni atarudi kesho maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo ya
Jumapili,” alisema Vanance Msebo, Mkurugenzi wa Kampeni wa
ACT-Wazalendo.