Tanzania yaikosoa filamu ya albino UN
Mwakilishi
wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi
(kulia) akizungumza kwenye umoja huo ikiwa ni muda mfupi kabla ya
kuonyeshwa kwa filamu ya “The Boy from Geita” ambayo inaelezea uovu
wanaotendewa watu wenye ulemavu wa ngozi. Picha na UN
-
New York, Marekani. Siku moja baada ya
mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, kuelezea kwa
waandishi wa habari juhudi zinazofanywa na Serikali dhidi uovu
wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi, Kamisheni ya Haki za Binadamu
ya Umoja wa Mataifa (UNHR ) imesema itashirikiana na Serikali ya
Tanzania katika juhudi hizo za kuukabili uovu unaofanywa dhidi ya jamii
hiyo ya Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu
Msaidizi wa Ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu, Ivan Simonovic muda
mfupi kabla ya kuonyeshwa kwa filamu iliyochezwa Tanzania ya “The Boy
from Geita”.
Simonovic alisema kuwa ushirikiano huo ni
katika kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika siyo kwa
kuhakikisha tatizo hilo linatoweka pia kwa kuwachukulia hatua za
kisheria wale wote wanaohusika na ukatili huo.
“Tofauti
na nchi nyingine, Serikali ya Tanzania imeonyesha ujasiri na uthubutu
wa kukabiliana na uovu unaofanywa dhidi ya watu wenye ualibino. Ni kwa
kutambua juhudi hizo tutashirikiana na serikali katika kukomesha uovu
huu,” alisema Simonovic.
Kauli Simonovic ya kutambua
juhudi hizo imetokana na juhudi iliyofanywa na Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania, Balozi Tuvako Manongi ya kuonana na wakuu wa idara ambazo
zimefadhili kuonyeshwa kwa filamu hiyo UN pasipo kuushirikisha wala
kuujulisha uwakilishi wa Tanzania. Maelezo ya awali kuhusu filamu hiyo
yanadaiwa kupotosha baadhi ya mambo hali iliyomfanya mwakilishi huyo wa
Tanzania kuchukua fursa ya kuyatolea ufafanuzi.
“Usiku
huu ninapenda kutambua juhudi zinazofanywa na moja ya nchi mwanachama wa
Umoja wa Mataifa, Tanzania, ambayo mwakilishi wake yupo pamoja nasi.
Siyo tu kwamba Tanzania imeonyesha ujasiri na uthubutu wa kutambua
ukubwa wa tatizo linalowakumba watu wenye ualibino pia imefanya juhudi
za kuwaelimisha wananchi wake huku ikichukua hatua muhimu,” alieleza
Simonovic. Alipopewa nafasi ya kuzungumza mbele ya hadhara hiyo. Balozi
Manongi alirejea kauli aliyoitoa mbele ya waandishi siku ya Jumatano,
kwamba, Tanzania haikatai na wala haipingi kwamba kuna tatizo kwa watu
wenye ulemavu wa ngozi. Alisema pamoja na kukiri kuwapo kwa matukio ya
uovu dhidi ya Watanzania hao, lakini angependa pia kuweka rekodi sawa na
hasa kufuatia maelezo ya upotoshaji ambayo yametolewa kwenye
vipeperushi vinavyoitangaza filamu hiyo.
Baadhi ya
mambo ambayo balozi ameyatolea ufafanuzi ni lile linaloelezwa na
waandaaji wa filamu hiyo wanaodai kuwa ualbino ulianza Tanzania miaka
2000 iliyopita jambo analosema halijathibitishwa kisayansi.