CCM, Chadema wapigana, wachoma moto maduka
Kyerwa. Zikiwa zimebakia siku saba kabla ya
kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, hali ni tete katika Kijiji cha Nyamiyaga,
Kata ya Bugomora wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera baada ya wafuasi
wanaodaiwa kuwa wa vyama vya CCM na Chadema kupigana kisha kuharibu
magari, pikipiki na kuchoma moto maduka.
Tukio hilo
lililotokea Jumatano kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 4:00 usiku, chanzo
kikielezwa kuwa ni baada ya misafara ya wagombea udiwani wa kata hiyo
kukutana eneo la Stesheni ya Nyamiyaga na wafuasi wao kuanza kurushiana
maneno. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamiyaga, Ferdinand Bashasha
ambaye pia ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bugomora, alisema wafuasi
wa CCM walikuwa kwenye stesheni hiyo wakiendelea na kampeni zao, huku
wakipiga muziki, wenzao wa Chadema walifika eneo hilo ambalo pia kuna
saluni ya mgombea wao wanayoitumia kama ofisi.
Kwa
mujibu wa ofisa mtendaji huyo walipofika walianza kurushiana maneno na
Bashasha aliingilia kati kuzima muziki wakati huo pamoja na
kuwasuluhisha.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha
Nyamiyaga, Hilalius Yustad alisema hali tete katika eneo hilo ilianza
tangu uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu wapo baadhi ya watu
hawaamini mpaka sasa kuwa yeye ndiye mwenyekiti.
Magari
mawili, maduka matatu na pikipiki mbili viliteketezwa moto, huku
pikipiki moja ikiwa haijulikani ilipo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera,
Ollomi Augustine alisema watu 20 wamekamatwa kwa mahojiano.