Mdomo wamponza Mourinho afungiwa, kupigwa faini
Kocha Jose Mourinho
London, England. Klabu ya Chelsea na kocha
wake, Jose Mourinho wamepinga uamuzi wa Chama cha Soka (FA) kumwadhibu
kocha huyo kwa kauli alizozitoa karibuni.
Juzi,
Mourinho alifungiwa mechi moja na kupigwa faini ya Pauni 50,000 kwa
kauli dhidi ya waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu. Adhabu hiyo dhidi ya
Mourinho imetolewa wiki moja baada ya mbaya wake, Arsene Wenger wa
Arsenal kunusurika adhabu kwa kauli dhidi ya mwamuzi Mike Dean
aliyemwita dhaifu na asiyejua wajibu wake.
Mourinho ambaye ataikosa mechi dhidi ya Aston Villa Jumamosi alionyesha kuwa mwenye hasira.
Kocha huyo Mreno aliwatuhumu waamuzi kuwa walikuwa wakizipendelea timu nyingine za Ligi Kuu zinapocheza na Chelsea.
Mourinho alimwelekezea shutuma Wenger akidai kuwa amekuwa akifanya mambo yake na kuonekana kuwa juu ya sheria na FA.
Baada ya mechi dhidi ya Southampton, Oktoba 3, ambayo Chelsea ilifungwa mabao 3-1, Mourinho aliwashushia lawama waamuzi.
Kauli hiyo ilimlenga mwamuzi Robert Madley baada ya
mshambuliaji Radamel Falcao ambaye kwa mtazamo wa Mourinho aliangushwa
na kipa wa Southampton, Maarten Stekelenburg. Picha za marudio za
televisheni zilipingana na mtazamo wa Mourninho.
Mourinho
alisema: “Ninafikiri kwamba ni muda mwafaka kuwa wakweli na kusema bila
kificho kwamba waamuzi wanaogopa kutoa uamuzi unaoinufaisha Chelsea.”
“Kama
FA inataka kuniadhibu, inaweza kufanya hivyo. Lakini, hawatoi adhabu
kwa makocha wenzangu, wananiangalia mimi. Hilo siyo tatizo kwangu.”
Klabu
yake, Chelsea ilieleza jana kuumizwa na kufungiwa kwa kochake ambaye
akirudia kosa hilo ndani ya mwaka mmoja atazuia kuingia uwanjani.
Naye
Mourinho alieleza kusikitishwa na uamuzi dhidi yake huku baada ya
kumshambulia mwamuzi Dean kwenye mchezo wa ligi ambao Arsenal ilifungwa
mabao 2-0 na Chelsea, Septemba 19.
Kocha huyo, The
Special One amekuwa akidai kwamba kauli zake zimekuwa zikichukuliwa
kinyume na kile alichokimaanisha, kuonyesha kuwa wanamlenga yeye zaidi.