Presha ya uchaguzi yamtesa Dk Kamala

Mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Nkenge, Dk Diodorus Kamala.
Misenyi. Mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Nkenge, Dk Diodorus Kamala amesema uchaguzi wa mwaka huu lazima viongozi wa chama hicho wawe makini kuweka mawakala wa kusimamia kura.
Akifunga kambi ya vijana eneo la Gera wilayani Missenyi juzi, Dk Kamala alisema vijana wa CCM wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ya kuomba kura kwa kutumia hoja za ushawishi.
Aliwashauri vijana hao watakapoona mtu hajaelewa, wasitumie nguvu wala malumbano, bali wajipange na kurudi kuomba tena kwa lugha nzuri zaidi hadi mhusika ashawishike kutoa kura yake.
Mgombea huyo alisema kuna baadhi ya mambo ambayo anaweza kuyatekeleza nje ya mipango ya Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Dk Kamala alisema lengo ni kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi wa Jimbo la Nkenge, hasa vijana wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira.
Alisema iwapo atachaguliwa, atahakikisha anafanikisha mipango yake ya kuondoa umaskini kwa kutumia wadau wa maendeleo badala ya kuisubiri Serikali.
Alisema baadhi ya mambo muhimu atakayoanza nayo atakapochaguliwa ni kupambana na umaskini kwa vitendo, atahakikisha anawagharamia masomo vijana 10 kila kijiji kwenye vyuo mbalimbali vya ufundi na maendeleo ya jamii.
Pia, alisema dhamira yake ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi za mikono, jambo ambalo litaongeza kasi yao ya kujiajiri.
Alisema atahakikisha Sh50 milioni zitakazotolewa na Serikali kila kijiji zinasaidia kupunguza umaskini na zinapatikana kwa muda mwafaka.
Katika hatua nyingine, Dk Kamala alisema kwa kushirikiana na Serikali, atahakikisha jitihada zinafanyika kuboresha Chuo cha Maendeleo ya Jamii Gera.
Mgombea huyo aliahidi iwapo atachaguliwa atahakikisha anatoa kompyuta mpya za kisasa kwa chuo hicho, kwani zilizopo hazina programu za kisasa jambo linalowafanya wanachuo kupitwa na teknolojia.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itawashawishi vijana kujiunga wengi na kuzalisha wataalamu wenye uwezo tofauti.
Kijana kutoka Kata ya Mtukula, Jenipher James (30) alisema wamejifunza ujasiri wa kwenda kwa wananchi kuwashawishi kwa kutumia lugha nzuri na kujenga hoja za kuomba kura, huku wakieleza mazuri ambayo CCM imeyafanya.
Naye Shadrack Joas wa Kata ya Buyango, alisema amejifunza kutowachukia wapinzani wanapoonyesha ishara zao, bali awaelimishe na kuwasikiliza ili kujua kinachosababisha waichukie CCM.
-
Powered by Blogger.