Sakata la kulinda kura latua Mahakama Kuu
Peter Kibatala
Dar es Salaam. Hatimaye mvutano kati ya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu umbali wa mwananchi kusimama baada ya
kupiga kura, umetinga Mahakama Kuu.
Aliyefungua kesi
hiyo ya kikatiba mahakamani ni mpigakura na mgombea ubunge wa viti
maalumu katika Jimbo la Kilombero kupitia Chadema, Amy Pascience
Kibatala akiomba litolewe tamko kuhusu tafsiri ya kifungu cha 104 (1)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 Ilivyorejewa mwaka 2010.
Chadema,
Amy Pascience Kibatala akiomba litolewe tamko kuhusu tafsiri ya kifungu
cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 Ilivyorejewa
mwaka 2010.
Kibatala amefungua kesi hiyo dhidi ya
Mwasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mwenyekiti wa NEC, chini ya hati ya
dharura. Shauri hilo namba 37 la mwaka 2015, limefunguliwa baada ya NEC
kuwataka wananchi, baada ya kupiga kura Oktoba 25, warudi nyumbani huku
Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD wakihimiza
wanachama na wafuasi wao kulinda kura kwa kukaa umbali wa mita 200 baada
ya kupiga kura kama sheria inavyosema.
Awali NEC
iliwataka wapigakura kurudi nyuma hadi mita 200 baada ya kupiga kura
lakini baadaye iliwataka wapigakura kurudi nyumbani. Msimamo huo
ulitolewa pia na Rais Jakaya Kikwete siku ya maadhimisho ya kumbukumbu
ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambapo
aliwataka wapigakura kwenda nyumbani baada ya kupiga kura.
Akihutubia
katika maadhimisho hayo Oktoba 14 yaliyokwenda sambamba na tukio la
kuzima Mwenge wa Uhuru, mjini Dodoma, Rais Kikwete alitoa wito kwa watu
wote kurudi majumbani kwao mara tu baada ya kumaliza kupiga kura.
Katika
shauri hilo, Kibatala anaiomba Mahakama Kuu itoe tamko la tafsiri
sahihi ya kifungu hicho kinachohusu haki ya wapigakura na wadau wengine
wa uchaguzi kukaa zaidi ya umbali wa mita 200 kutoka katika kituo cha
kupigia kura na cha kuhesabia kura.
Kwa mujibu wa
Kibatala msimamo wa NEC ni kinyume cha Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania hususan Ibara ya 18 (1), 21 (2), 29 (2). Pia, anadai kuwa Rais
Kikwete wakati akihutubia wananchi kwenye maadhimisho ya kifo cha Baba
wa Taifa,licha ya kuamuru watu wasikae katika eneo hilo, pia alikwenda
mbali kwa kuwatisha wapigakura kuwa watakaokaidi amri hiyo vyombo vya
dola vitatumia nguvu dhidi yao.
Kibatala anadai kuwa
akiwa mpigakura aliyesajiliwa na anayekusudia kutumia haki ya msingi
kushiriki mchakato huo wa uchaguzi, zuio hilo linakiuka haki za kikatiba
zinazobainishwa katika Ibara ya 5(1), 18 (1), 21 (2) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kibatala anadai kuwa
zuio hilo linaathiri haki ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
uchaguzi uliotangazwa kuwa utakuwa wa wazi.
Vilevile,
anadai kuwa zuio hilo linaelekea kumnyima haki ya kufuatilia kwa karibu
mchakato wa uchaguzi kutoka umbali uliowekwa kisheria ambao unamwezesha
kuwapo wakati wa kutangazwa kwa matokeo kwa kuzingatia kuwa hakuna
utaratibu rasmi wa NEC kuwaita wapiga kura kusikiliza matokeo.