Dk Makaidi kuzikwa Dar
Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi.
-
Dar es Salaam. Mwili wa Mwenyekiti Mwenza
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi unatarajiwa
kuletwa Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika
Oktoba 20, mwaka huu.
Dk Makaidi ambaye pia alikuwa
Mwenyekiti wa Chama cha NLD na mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi mkoani
Mtwara, alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi
baada ya kupata shinikizo la damu.
Akizungumza na
gazeti hili kwa njia ya simu jana, msemaji wa familia hiyo, Oscar
Makaidi ambaye pia ni mtoto wa Makaidi alisema wameamua mwili huo uzikwe
Dar es Salaam baada ya kujadiliana.
“Kuna sababu
nyingi zilizosababisha tufikie uamuzi huo, ikiwamo kwamba baba mwenyewe
enzi za uhai wake alituagiza kuwa akifa tumzike alipozikwa mkewe wa
kwanza,” alisema.
Oscar alisema pia mama mzazi wa Dk
Makaidi alizikwa Dar es Salaam, suala ambalo litawafanya watoto na
wajukuu wanapozuru makaburi wafanye hivyo kwa pamoja.
Alisema
kutokana nafasi ya kisiasa aliyokuwa nayo baba yake, wameamua azikwe
Dar es Salaam ili kutoa nafasi watu wengi washiriki kwenye maziko hayo
tofauti na iwapo watamzika kwao Masasi.
“Jumanne
tunatarajia ndiyo tutaupumzisha mwili wake. Tumesogeza siku kutokana na
maombi ya viongozi wa kitaifa wa Ukawa ambao walituomba ili wapate
nafasi ya kushiriki. Tunashukuru kwa ushirikiano wa wananchi wa huku,
akiwamo mbunge wa Masasi anayemaliza muda wake, Mariam Kasembe,” alisema
msemaji huyo.