Oktoba 25, siku muhimu ya mabadiliko ya Watanzania


Oktoba 25 mwaka huu ni siku muhimu ya historia ya Tanzania, siku ambayo Watanzania milioni 22,751,292 wanatarajiwa kujitokeza kupiga kura kumchangua rais wa awamu ya tano.
Siku hii pia, majimbo mengi yatachaguwa wabunge na madiwani kwa upande wa Tanzania bara, huku Zanzibar wakichagua, rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge.
Nasema siku hii ni ya kihistoria kwa sababu, tumeshuhudia
kampeni ambazo hazijawahi kuonekana hapa nchini, vyama vimekuwa vikisaka kura kwa nguvu zote.
Safari hii, tumeshuhudia vyama vinne, vikiungana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, Edward Lowassa.
Ukawa ambayo inaundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD pia katika majimbo mengi wamefanikiwa kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge na udiwani.
Safari hii pia tumeshuhudia Chama cha Mapinduzi (CCM) kikifanya kampeni kubwa kwa kutumia viongozi wengi wastaafu, wasanii, matangazo ya redio, runinga na mitaani katika kila kona nchini.
Chama kingine ambacho kimeleta ushindani ni ACTWazalendo
ambacho, mgombea wake Anna Mnghwira ameweza kuvuta hisia kwa watu wengi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzungumza majukwaani.
Hivyo, itoshe kusema huu ni mwaka wa mabadiliko ya kweli kwani tumeshuhudia kila mgombea akihubiri mabadiliko katika serikali ya awamu ya tano.
Tofauti na chaguzi zilizopita, safari hii mgombea wa urais wa chama tawala (CCM), Dk John Magufuli amekuwa pia akihubiri mabadiliko kama akichaguliwa kuwa rais.
Anasema Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli, ambayo anaamini yeye ndiye atayaleta, kwani ana dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania, huku akiahidi kuwa hatawaangusha.
Dk Magufuli safari hii, jina la CCM ameliweka kando kwenye kampeni zake na amekuwa akitumia kauli ya chagua Magufuli
siyo chagua CCM, kauli ambayo imezoeleka.
CCM miaka ya nyuma ilikuwa na msemo kuwa Watanzania wanapaswa kuchagua chama na siyo mtu, lakini sasa katika mazingira yaliyopo, inasema Watanzania wachague mtu na siyo chama.
Hii inaonekana ni karata ya CCM katika kuhak ikisha inaendelea kushika dola kwani pia tumemsikia, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana akieleza kuwa kina wanafiki na wafitini, lakini CCM ijayo ya Dk Magufuli itakuwa tofauti.
Dk Magufuli anasema Tanzania yake, itakuwa ni ya viwanda huku akitangaza elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari, kuongeza vita dhidi ya rushwa na ufisadi huku huduma muhimu zikiboreshwa.
Kwa upande wa upinzani, tumeshuhudia makada wa CCM, Kingunge Ngombale- Mwiru, Frederick Sumaye, Balozi Juma Mwapachu na wengine wengi wakikihama chama hicho na kujiunga na harakati za upinzani kutaka mabadiliko.
Kingunge ameibuka na hoja kuwa, CCM imeishiwa pumzi hivyo kutaka ipumzishwe, kwani miaka zaidi ya 50 imekwama na sasa imechoka inafaa kuwapisha wengine.
Hivyo, itoshe kusema huu ni mwaka wa mabadiliko, kwani tumeshuhudua msuguano wa kaulimbiu za vyama, kati ya CCM na Chadema na mgombea wa CCM, Dk Magufuli ameibuka na kusema kaulimbiu ya M4C ni ‘Magufuli kwa Mabadiliko’.
Kauli hiyo inatumiwa na Chadema kuchochea vuguvugu la mageuzi nchini.
Mussa Juma ni mwandishi wa mwananchi mkoa wa Arusha anapikana 0754296503, mjuma@tz.nationmedia.com.
-
Powered by Blogger.