Magufuli asaini ujenzi wa ‘flyover’ D’Salaam
Mchoro wenye kuonesha mfano wa barabara za juu zinatarajiwa kuanza kujengwa katika eneo la Tazara zitakavyokuwa.
-
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na ya
Japan, zimetiliana saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa barabara ya juu
(flyover) na Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction utakaogharimu zaidi
ya Sh87 bilioni.
Ujenzi huo ambao utafanyika katika
makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, eneo la Tazara jijini Dar es
Salaam utaanza mwezi huu na ukamilika katika kipindi cha miezi 35.
Akizungumza
wakati wa utiaji saini mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli,
alisema Serikali imekuwa ikihangaika kwa zaidi ya miaka saba ili
kupunguza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam.
“Nawashangaa
wanasiasa wengine wanapanda majukwani na kusema wataondoa tatizo la
foleni kwa siku 90 wakati kupata mkandarasi tu imechukua miaka mingi.
Ujenzi wenyewe hadi kukamilika ni zaidi ya miaka miwili,”alisema.
Dk
Magufuli aliishukuru Serikali ya Japan kwa kukubali kujenga barabara
hiyo ya juu kwa bei inayoendana na bajeti iliyotengwa na kuitaka Wakala
wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuusimamia vema mradi huo.
Awali,
akizungumzia sababu za kuchelewa kwa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Tanroads, Patrick Mfugale alisema ilitokana na kupandishiwa bei na
makandarasi waliokuwa wakipewa kazi hiyo.
“Utiaji saini
wa mkataba wa mradi huu ni faraja kwa wakazi wa jiji hili, kwani
ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu ili kupunguza kero ya msongamano wa
magari,” alisema.