Boban, Kaseja kuitibulia Simba SC
Wachezaji wa Mbeya City, Haruna Moshi ‘Boban’ (kushoto) na Juma Kaseja (kulia)
Mbeya. Mshambuliaji wa zamani wa Simba,
Haruna Moshi ‘Boban’ na kipa Juma Kaseja ni miongoni mwa silaha za Mbeya
City zilizoandaliwa kuiua timu ya Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
Boban
alijiunga rasmi na kikosi cha Mbeya City juzi na jana asubuhi aliungana
na wenzake kwenye mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya
kujiandaa kuikabili Simba.
Kocha msaidizi wa City, Meja
Mstaafu Abdul Mingange aliliambia gazeti hili jana kwamba Boban ni
mmoja wa wachezaji wanaotarajia kuchezeshwa kwenye mechi ya kesho dhidi
ya Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mbeya City, pia inaye kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Juma Kaseja aliyesaini mkataba wa msimu mmoja.
Alisema,
“Leo nimesema afanye zoezi kwa lengo kumwangalia, lakini nimeona yupo
vizuri na lazima mechi ya keshokutwa (kesho), Jumamosi atacheza dhidi ya
Simba.”
Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo haukutaka kuelezea
matumaini ya ujio wa Boban ndani ya klabu hiyo, huku ukisema Boban ni
mchezaji wao halali na hawawezi kumzungumzia mtu mmoja, bali
wanawazungumzia wachezaji wote.
Mwenyekiti wa Mbeya
City, Mussa Mapunda alisema, “Kwanini Boban, sisi hapa wachezaji wote
wapo sawa, hivyo hatutaki ubaguzi wa kumzungumzia mchezaji mmoja hapa.”
Kuhusu
mechi ya kesho dhidi ya Simba, Meja Mingange alisema anaouna mchezo huo
kuwa utakuwa mgumu kwake kutokana na kila timu kupania kushinda katika
mechi hiyo, lakini amejipanga vizuri kuhakikisha waendeleza ubabe kwa
Simba.
Kuhusu mazingira ya ugumu wa mechi hiyo, Afande
Mingange alisema kwanza yeye binafsi ana siku tatu tangu aanze kuinoa
timu hiyo, hivyo hawezi kuwa jipya la ziada kuwabadili wachezaji wake,
lakini pia kuna mchanganyiko mkubwa wa wachezaji ambao ni wapya kwenye
kikosi chake.
Alisema, “Kubwa zaidi historia inaonyesha
Simba haijawahi kushinda dhidi yetu ( Mbeya City), iwe ni ugenini ama
nyumbani, hivyo watakaza ili kuvunja mwiko. Ila, nasema hivi tutapigana
hadi dakika ya mwisho na Mungu atakuwa upande wetu.”