Wanasiasa wahimiza amani wakati wa uchaguzi


Dar es Salaam. Vyama vya siasa vimewataka wadau wote wa uchaguzi kuzingatia amani katika Uchaguzi Mkuu, huku vikisisitiza haki kutendeka ili kuiwezesha nchi
kubaki salama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, viongozi wa vyama hivyo walisema amani ni suala la muhimu kuliko kitu chochote na wengine wamedai kuna vikundi vilivyoandaliwa kufanya vujo.
Mbowe ataka haki na amani
Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kama vyombo vinavyosimamia Uchaguzi Mkuu vinahubiri amani bila kutenda haki, ni sawa na kazi bure, akifananisha kitendo hicho na kumlisha mtu upepo.
“Mamlaka zote zinatakiwa kuheshimu sheria zilizopo,” alisema Mbowe. “Tunaamini wananchi ndiyo wanaopaswa kuchagua kiongozi. Hilo likifanyika na kama matokeo hayatabadilishwa uchaguzi utakuwa wa amani.
“Ila kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wengine wakiminya
haki na kulazimisha matokeo yawe kinyume na kura zilizopigwa na wananchi, sidhani kama Amani tunayoihubiri itakuwapo.”
Mbowe alisema chaguzi nyingi nchini hulalamikiwa kutokana na mamlaka mbalimbali kukiuka sheria. Alipotakiwa kueleza mambo yanayotakiwa kuzingatia na vyombo hivyo, alisema: “Ninachoweza
kusema ni hiki; vyombo vyote vizingatie sheria na taratibu ila kinyume na hapo amani hakuna.” Mbowe pia alisisitiza suala la wananchi kukaa nje ya mita 200 kutoka vituoni baada ya kupiga
kura.
“Kukaa mita 200 ni suala la kisheria halihitaji tamko la Rais. Tutalinda
kura zetu na kama wanadhani jeshi litaweza kuzuia, hakika watakuwa wanajidanganya. Habari ndiyo hiyo,” alisema Mbowe.
Alisema Ukawa na Chadema watakakubali matokeo ya uchaguzi huo kama utakuwa wa haki na kusisitiza kuwa iwapo kutafanyika kwa hila yoyote, watayakataa.
Msajili wa vyama anena
Suala hilo pia liligusiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi. Jaji Mutungi aliwataka wanasiasa wanaokutana misibani kuitumia kujadili amani ya nchi kwa maelezo kuwa misiba huwakutanisha watu ambao licha ya uchungu walionao, wanaweza kujadiliana masuala ya msingi sana.
Mghwira hataki vitisho
Akizungumzia suala hilo, mgombea urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Anna Mghwira alisema ili kudhibiti machafuko, viongozi waache kutumia kauli za vitisho na NEC ifanye kazi kwa uhuru na haki bila kukipendelea chama chochote.
Alisema matumizi ya nguvu bila hekima hayatasaidia kuondoa tatizo, bali yatasababisha Amani kuvunjika, hivyo alitaka polisi wakae pembeni kama walivyokuwa wakisimamia mikutano ya kampeni, bila kumkamata wala kumzuia mtu kuzungumza anachotaka na Amani ikatawala.
Mghwira alisema NEC ina kila sababu ya kuhakikisha nchi inabaki na amani baada ya uchaguzi kwa hatua watakazochukua wakati wa kutangaza matokeo.
“Wakitangaza matokeo kwa kusuasua wanaweza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema.
“Hakuna ubishi kuwa uchaguzi wa mwaka huu una mhemko mkubwa
hasa kwa vijana, hivyo Tume, viongozi walio madarakani, wakitumia nguvu wakati wa kutangaza matokeo, wataleta machafuko makubwa. Ili kuyaepuka hekima inahitajika,” alisema Mghwira.
Mghwira alifafanua kuwa kama ilivyoonekana kwenye majukwaa ya siasa, vivyo hivyo wakati wa kupiga kura na kutangaza matokeo ukomavu wa kisiasa uonyeshwe kwa kuwaweka mbali wanajeshi, polisi
ili wananchi wafanye uamuzi wakiwa huru bila kutishwa na mitutu ya
bunduki.
Samia
Wakati wapinzani wakihamasisha wafuasi wao kukaa mita 200 kutoka vituoni, mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan aliwataka kurejea nyumbani mara baada ya kupiga kura ili kazi hiyo imalizike kwa usalama.
Samia, ambaye amekuwa akirejea kauli hiyo mara kwa mara katika
mikutano ya kampeni, alisema hakuna haja ya kubakia vituoni, badala yake warejee nyumbani kuendelea na shughuli zao.
“…Na siku ya kupiga kura tukapige kwa usalama naomba vijana wa CCM na wananchi wote, muwalinde dada zenu na mama zetu wakapige kura kisha warudi nyumbani salama,” alisema Samia.
“Kuna wanaoandaliwa kufanya fujo, lakini nataka niwaambie mwanaume mwenye nguvu kuliko Serikali Tanzania hii bado hajazaliwa,
kwa hiyo hakuna haja ya kuogopa.

Imeandikwa na Suzan Mwillo,Kalunde Jamal na Fidelis Butahe
-
Powered by Blogger.