HOJA YA UCHUMI: Hatuhitaji kusubiri rais mpya kuiokoa shilingi
Mwishoni mwa wiki iliyopita nilipata fursa ya kubadilisha
kiasi kidogo cha fedha za kigeni katika moja ya maduka ya kubadilishia
fedha Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Mara nyingi
nikibadilisha fedha hizo katika maduka mbalimbali huwa sipatiwi risiti
zinazonitambulisha kuwa nimeuza Shilingi au nimenunua fedha ya kigeni.
Hali hiyo nimekumbana nayo kwa muda sasa kiasi cha kunipa wasiwasi juu ya ufanisi katika udhibiti wa fedha za kigeni nchini.
Tofauti
na kipindi cha nyuma safari hii nilikuta tangazo la Benki Kuu ya
Tanzania lililoandikwa kwa Kiingereza likiwa limebandikwa katika duka
hilo.
Tangazo hilo lilikuwa linayataka maduka ya
kubadilishia fedha kutoa risiti kwa wateja mara baada ya mauzo ya fedha
za kigeni ikiwa ni utekelezaji wa kanuni ya 15 (C) ya Sheria ya
Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2008.
Kama wateja
wengine, nilitoa Dola za Marekani nilizokuwa nahitaji kuziuza nipate
fedha za nyumbani, lakini baada ya kukokotoa kiwango na kupatiwa fedha
hizo, mhudumu hakunipatia risiti zaidi ya kunishukuru kwa kufika dukani
kwake.
Kwa kuwa nilidhamiria kudai risiti nilimuomba
mhudumu huyo haki yangu ambaye alishtuka na kuuliza “kaka kwani unataka
na risiti?”
Kwa mazingira ya haraka haraka duka hilo
huwa halina utamaduni wa kutoa risiti kwa wateja, kwani iliwabidi waanze
kuhangaika kuwasha kompyuta mpakato kuunganisha na printa ili
wachapishe risiti hiyo.
Kama njia ya kunikatisha tamaa
walitumia takriban dakika tano hivi na kunieleza niwe mvumilivu kwani
kulikuwa na tatizo wanashughulikia. Baada ya kuona sikati tamaa
waliharakisha “kutatua tatizo” na baada ya dakika 10 hivi walichapisha
risiti hiyo huku mmoja akikejeli “kaka unapeleka ofisini nini wakaiweke
kwenye rekodi.”
Nimeamua kusimulia kwa kirefu kisa hiki
kwa kuwa umekuwa utamaduni kwa wafanyabiashara kukwepa kutoa risiti na
wateja tumekuwa tukishawishika kufuata uovu huo hata katika mahali
ambapo hautengenezewi ahueni ya aina yoyote.
Tofauti na
nchi za wenzetu hata kwa majirani zetu wa Kenya, ukibadilisha fedha
katika maduka ya kubadilishia fedha ni lazima wahudumu wakuhoji
kitambulisho chako, wachukue jina lako na kukupatia risiti. Huo ndiyo
utaratibu mzuri ambao hata sheria hapa nchini zinausisitiza.
Hata
hivyo, hapa nyumbani jambo hilo siyo la msingi licha ya kuwa ni kinyume
na sheria za nchi. Kuna kila dalili kuwa Watanzania tuna matatizo
makubwa ambayo hayahitaji rais mpya kuyatatua kama kuilinda Shilingi.
Pia, hii ni ishara kuwa mamlaka zinazohusika kusimamia sheria kama BOT
hazifanyi kazi ipasavyo.
Kwa elimu yangu ndogo ya
uchumi kinachofanywa na maduka hayo ya kubadilishia fedha ni hatari kwa
uchumi wa nchi yetu, hasa katika kipindi hiki ambacho Shilingi inazidi
kushuka thamani dhidi ya fedha za kigeni, hususan Dola.
Pamoja
na ukweli kuwa kuna sababu kubwa za kushusha thamani ya Shilingi yetu
kama kuongezeka kwa thamani ya Dola ya Marekani ulimwenguni na kupungua
kwa uuzaji bidhaa nje ya nchi, bado maduka hayo yanaweza yakafanya uovu
wa makusudi kuingamiza Shilingi yetu.
Hii itatokana na
ukweli kuwa, tabia ya kutokutoa risiti kwa wateja kunaficha taarifa za
ukweli juu ya mzunguko wa fedha za kigeni ambazo wakati mwingine BOT
huziingiza sokoni nje ya viashiria vya kisoko
Mtindo
huo unaweza kusababisha mahitaji bandia ya fedha za kigeni hasa Dola na
kusababisha Shilingi yetu kushuka thamani na kupandisha bei ya bidhaa na
huduma kutokana na kuongezeka kwa gharama za uingizaji wa bidhaa kutoka
nje ya nchi.
Iwapo hakuna kumbukumbu ya mauzo ya fedha
hizo katika maduka ya fedha kwenda BOT, itafahamika vipi kuwa kiwango
cha fedha za kigeni zinazouzwa na kununuliwa kila siku nchini? Mamlaka
ya Mapato Tanzania itafahamu vipi kiasi cha kodi inayopatikana katika
biashara hiyo?
Ni wazi kuwa kitendo cha maduka hayo
kutotoa risiti na wananchi kutodai kunasababisha Serikali ipoteze mapato
yake kwani katika kila biashara inayofanyika kuna kodi inayotakiwa
kulipwa.
Kuendelea kuwakumbatia wafanyabiashara hao
kutaifanya nchi iendelee kupoteza mapato ambayo yangesaidia kugharamia
miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii.
Pia,
jitihada za kuzuia uvunjaji huo sheria zikawabane na wafanyabiashara
wanaolazimisha wananchi kupata huduma zao kwa kutumia Dola ya Marekani
kinyume na sheria hasa katika sekta ya nyumba na makazi.
Nuzulack Dausen ni mwandishi wa gazeti hili. Anapatikana kwenye mtandao wa Twitter @nuzulack