Dk Shein awataka vijana CCM kuepuka fujo

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Ali Mohammed Shein akizungumza katika moja ya mikutano ya chama hicho. Picha na Maktaba
Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Ali Mohammed Shein amewataka vijana kutokukubali kutumiwa kufanya fujo na kwamba Serikali itahakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Kauli kama hiyo ilitolewa na mpinzani wake, Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye aliwataka wafuasi wa chama chake cha CUF kutokubali kuingia kwenye vurugu akidai kuwa CCM imepanga kuwachokoza ili wafanye fujo.
Jana, Dk Shein aliyekuwa akizungumza katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale na kuhudhuriwa na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, aliwataka vijana kutokubali kutumiwa kufanya vurugu katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25.
“Wananchi msiwe na hofu, uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Hakuna fujo yoyote itakayotokea,” alisema Dk Shein ambaye anawania kuongoza visiwa hivyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Alisema anasikitishwa na vitisho wanavyopewa wafuasi wa CCM wakati walipokuwa wakifanya maandalizi ya mkutano wa Dk Magufuli kisiwani Pemba.
Dk Shein aliwaambia wakazi wa Pemba kuwa atahakikisha wanakuwa na meli kubwa ya uvuvi ili wavuvi waweze kufika bahari kuu kuvua samaki kwa urahisi.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni, Dk Magufuli alisema Serikali atakayoiongoza itaimarisha sekta ya uvuvi na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara ya samaki kwa nchi za Afrika Mashariki na dunia.
Alisema Zanziba ina rasilimali ya samaki ambayo inahitaji mipango madhubuti ili iweze kutoa ajira kwa vijana.
“Hilo litawezekana mkinichagua kuongoza nchi. Zanzibar itakuwa soko kuu la samaki duniani,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliwataka wananchi wa Pemba kuacha jazba za siasa na kuweka mbele maslahi yao na maendeleo ya nchi yao.
Aliahidi kudumisha Muungano akimtaja mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan kuwa suluhisho la kero za Muungano.
“Msifanye makosa Oktoba 25,” alisema Dk Magufuli.
Katika mkutano huo ambao umevunja rekodi kwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, Dk Magufuli alipokea wanachama wapya 80 kutoka CUF.
Alisema kwa kushirikiana na Dk Shein ataongeza kasi ya kuimarisha huduma za kijamii, kama barabara, afya, elimu pamoja na mawasiliano.
Kwa upande wake Balozi Seif Ally Idd aliwataka wananchi wa Pemba kuwachagua wagombea wa CCM ili waendeleze kasi ya maendeleo.
-
Powered by Blogger.