Chopa inayosadikiwa kubeba makada wa CCM yaanguka
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
-
Dar es Salaam. Chopa inayosadikiwa kubeba makada wa CCM imezua utata baada ya kudaiwa kudondoka katika eneo la Msolwa, Hifadhi ya Selous.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alilithibitishia Mwananchi kuwa
kuna chopa imedondoka katika hifadhi hiyo Kitalu R3 na watu waliompa
taarifa hizo walikuwa Kitalu R2.
Akizungumza na
Mwananchi saa sita usiku, Nyalandu alisema eneo hilo lipo karibu na Mto
Ruaha ambao ni mpana sana. “Mashuhuda waliona helkopta ikianguka na
tunafanya kila kitu kuhakikisha tunapata ufumbuzi wa suala hili,”
alisema Nyalandu.
Katika ukurasa wa twitter, Nyalandu
aliandika, “Mashuhuda wa ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa
Kitalu R2 walishuhudia ikianguka na kulipuka ng’ambo ya Mto Ruaha Kitalu
R3,”
Hata hivyo, kulikuwa na utata wa hali ya abiria
wanne na rubani waliokuwa ndani ya chopa hiyo iliyokuwa inatoka Dar es
Salaam kwenda Iringa na Njombe.
Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii jana usiku zilieleza kuwa helkopta hiyo ilikuwa na watu wanne na rubani mmoja.
Kutokana
na taarifa hizo kuzagaa, msemaji wa Kampeni za CCM, January Makamba
aliandika katika akaunti yake ya twitter kuwa: “Tumesikia habari za
Chopa kuanguka huko Selous. Mungu aepushe kusiwe na majeruhi. Chopa zote
zinazotumiwa na CCM kwenye kampeni ziko salama.”
Inadaiwa kuwa awali Chopa hiyo ilikuwa inatumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe.
Mwananchi
ilifanya juhudi za kumtafuta Filikunjombe jana usiku, lakini simu yake
muda wote ilikuwa inatumika na wakati mwingine kutopatikana kabisa.
Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema wamepata taarifa za ajali lakini hakuna aliyefika eneo la tukio mpaka leo.
Aidha
Meya wa Ilala, Jerry Silaa asubuhi hii aliandika kwenye kurasa yake ya
Instagram kuwa: “Baba yangu Capt.William Silaa akiwa na Mhe.Deo
Filikunjombe na abiria wengine walipata matatizo ya engine ya helicopter
5Y-DKK jana jioni wakitokea Dar kuelekea Ludewa. Taarifa za mwisho
ilionekana imeanguka kwenye msitu wa Selous. Hakuna mawasiliano ya simu.
Usiku kucha vyombo vyote vya serikali vimeendelea na jitihada za kufika
eneo la tukio na jitihada kubwa zaidi zinaendelea asubuhi hii. Nawaomba
wote kuwa watulivu kwani jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu
na ushirikiano wa taasisi nyingi za wizara tofauti. Tuwaombee wote Mungu
awanusuru."