Kikwete aongoza mamia kumzika Kigoda
Mufti
wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi (mbele) akiongoza swala ya mazishi
ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda mjini Handeni,
mkoani Tanga jana. Picha na Burhani Yakub
Handeni/Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete
na mkewe Mama Salma Kikwete jana, waliwaongoza mamia ya wananchi kwenye
mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.
Dk Kigoda alifariki dunia Oktoba 12, kwenye Hospitali ya Apollo, India alikokuwa akitibiwa.
Akisoma
wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mussa Uledi alisema Dk
Kigoda alijikita zaidi katika kazi na ndicho chanzo cha kuchelewa kwenda
kupata matibabu India.
Katika salamu zake kwa wafiwa
na wakazi wa Tanga, Spika Anne Makinda alisema Bunge limepoteza mshauri
mzuri wa mambo ya uchumi ambaye alikuwa hasukumwi kufanya kazi tangu
alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge hadi
alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa waziri.
Viongozi wa
kada tofauti walitoa salamu za rambirambi akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Salum Mwalimu aliyesema wanasiasa wamepoteza mpambanaji na mtu
ambaye hakujikweza katika nafasi zote alizozishika.
Mtoto wa Kigoda, Omar Kigoda pamoja na kutoa shukran kwa Serikali, pia aliwashukuru wakazi wa Handeni kuifariji familia hiyo.
Kabla
ya mazishi hayo, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliwaongoza
mamia ya waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mwanasiasa
huyo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Sambamba
na Makamu wa Rais, viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, mawaziri, wabunge na marais wa wastaafu Ali Hassan
Mwinyi na Benjamin Mkapa walishiriki kuaga mwili huo.
Akisoma
salamu kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe alisema kifo cha Dk Kigoda kimeacha pengo kubwa serikalini
kutokana na umahiri aliokuwa nao katika masuala ya uchumi. “Daima
tutamkumbuka Kigoda kwa utumishi wake uliotukuka, alijitoa kwa dhati
kutumia taaluma yake katika kuliletea maendeleo taifa,”alisema.
Shughuli
ya kuaga mwili huo ilimalizika saa 3,30 asubuhi na safari ya kwenda
Handeni kwa mazishi ilianza. Imeandikwa na Elizabeth Edward, Rajabu
Athuman na Burhani Yakub.