NEC: Wanasiasa acheni kutumia majukwaa vibaya
Kamishna wa Tume Jaji mstaafu, Mary Longway
Iringa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
imewataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kutumia majukwaa vibaya
katika muda uliobaki badala yake wanadi sera zao.
Kamishna
wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mary Longway alisema hayo kwenye mkutano
uliowakutanisha maofisa wa NEC na viongozi wa vyama vya siasa mkoani
hapa juzi.
“Tume imekuwa ikifuatilia kampeni za vyama
vyenu vya siasa, tumieni nafasi zenu kueleza sera ili kuwasaidia
wananchi kufanya uamuzi sahihi,” alisema Longway.
Aliwaasa
viongozi hao kuwasilisha malalamiko yao katika kamati za maadili
zilizopo kisheria pindi wanapoona maadili na kanuni za uchaguzi
zinakiukwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia Tume kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika kampeni kwa wakati.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Iringa, Mustapher Msowela aliitaka Tume kukutana na
viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kujadiliana
kuhusu wananchi kukaa umbali wa mita 200.
Mwakilishi wa
Chama cha SAU Iringa, Selemani Rajabu alisema katika suala la watu
kulinda kura busara inapaswa kutumika ili kuepuka vurugu.
“Watu wanaosimama umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura waachwe wasubiri endapo hawatafanya vurugu ,” alisema Rajabu.