Mbegu za kiume huhifadhi virusi vya ebola
Freetown, Sierra Leone. Utafiti umeonyesha
virusi vya ebola vinaweza kudumu kwenye mbegu za kiume kwa baadhi ya
watu waliopona ugonjwa huo kwa takriban miezi tisa.
Hayo
yamo kwenye utafiti wa awali uliofanywa kwa pamoja na Wizara ya Afya na
Usafi wa Mazingira ya Sierra Leone, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo,
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa
cha Marekani.
Matokeo ya ufatifi huo yalitangazwa juzi
nchini humo baada ya kukamilika kwake na kubaini siyo kila mbegu za
mwanaume zinaambukiza bali ni baadhi ya watu waliopona ugonjwa huo kwa
takriban miezi tisa.
Taarifa hiyo ilisema, awali virusi
vilionekana kwenye mbegu za uzazi za wanaume baada ya kupona, hata
hivyo kuna taarifa chache tu kuhusu muda wa virusi hivyo kudumu katika
mbegu hizo.
Kwa mujibu wa utafiti wanaume wanapaswa
kujizuia na aina zozote za ngono au kutumia mipira hadi wapimwe mara
mbili na kuonekana hawana virusi vya ebola.
Wakati
huohuo, China na Umoja wa Mataifa wamesaini makubaliano kuhusu China
kuchangia Dola 5 milioni za Marekani kusaidia mapambano dhidi ya ebola.
Mchango huo utaingizwa kwenye mfuko wa fedha wa kushughulikia ebola ili kusaidia Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti na Ebola.
Ugonjwa
huo ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama homa za
virusi zinaazosababisha kutokwa na damu mwilini (Viral Haemorrhagic
Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huo hakijulikani.
Tafiti
zinaonyesha kwamba katika orodha ya watu 10 waliopata kirusi cha ebola,
wastani kati ya watu watano au tisa hufariki dunia.