‘Vichinjio’ vinavyobeba uhalali, haki
Wakati Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika Oktoba 25,
ukiwa ni wa tano tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini
mwaka 1992, safari hii Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), imetoa
vitambulisho vya mpiga kura vyenye alama za utambulisho za kibaiolojia.
Licha ya hatua hiyo, kuna madai ya kusambaa na kukamatwa kwa vitambulisho bandia vya kupigia kura.
Vitambulisho
hivyo vilitolewa wakati wa uandikishaji wananchi kwenye daftari hilo
ulioanza Machi 23 mwaka huu mkoani Njombe na kuhitimishwa Dar es Salaam,
Agosti 4.
Kupitia mfumo huo, Watanzania 22,751,292
wenye sifa wameandikishwa kwa ajili ya kupiga kura siku tisa zijazo kwa
ajili ya kumchagua rais, wabunge na madiwani. Katika uchaguzi
unaohusisha ya vyama vya siasa 22.
Walioandikishwa ni
wale waliokuwapo kwenye daftari lililotumika katika Uchaguzi Mkuu mwaka
2010, wapigakura wenye sifa ambao hawakuandikishwa awali na wote
waliotimiza umri wa miaka 18 mpaka siku ya uchaguzi.
Baada
ya NEC kufanikisha hatua hiyo ukafuata mchakato wa kuhakiki na
kuhamisha taarifa kwa wananchi waliobadilisha makazi na maeneo ya
kupigia kura na ulitengwa mwezi mmoja kwa ajili ya kazi hiyo.
Muda
huo ulimalizika Septemba, hivyo kutoa fursa kwa wataalamu wa Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka tume hiyo kuendelea na
uchakataji wa taarifa za wapiga kura zilizokusanywa.
NEC
licha ya kukiri ugumu katika utekelezaji jukumu hilo, uliochangiwa na
sababu mbalimbali ikiwamo za kiutawala na uwezeshaji kitambulisho cha
mpigakura ndicho kithibitisho kinachobeba haki ya Mtanzania kuwa
mpigakura halali.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu
Damian Lubuva anasema walijifunga kibwebwe kuhakikisha wanakamilisha
uandikishaji kwa BVR, huku akiainisha baadhi ya changamoto walizokumbana
nazo.
Anataja changamoto zilizoibuka wakati wa
uboreshaji wa daftari hilo kuwa ni pamoja na ugumu wa kuchukua alama za
vidole kutoka kwa baadhi ya wananchi, hali iliyosababishwa na kazi za
kiuchumi wanazozifanya kila siku.
Nyingine ni mashine
za uchapaji kuhitaji kusafishwa mara kwa mara kutokana na mazingira ya
vumbi kwenye vituo vya uandikishaji na maombi mengi ya kuanzishwa vituo
vingine vya kazi hiyo wakati kazi hiyo imekwisha kuanza, pamoja na dhana
potofu kwamba mfumo wa BVR utasaidia kuchakachua matokeo.
“Pamoja
na changamoto hizo Tume imefanikisha uandikishaji kwa muda mfupi.
Tulikuwa na mashine 8,000 pekee, lakini tukaandikisha watu wengi zaidi
kuliko nchini nyingi zilizowahi kutumia teknolojia hiyo. Tumepongezwa
kwa hili…Umoja wa Tume za Uchaguzi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC), wamevutiwa na ufanisi wetu,” anasema Jaji Lubuva.
Kadi feki
Lubuva
anasema licha ya kuzaga uvumi wa kuwapo kwa kadi za kughushi miongoni
mwa wapigakura wanaotarajiwa kujitokeza siku ya uchaguzi, tishio
linalotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini NEC wenye
dhamana na kusimamia Uchaguzi Mkuu imejipanga kukabiliana nalo.
Tangu
kuundwa kwake Januari 1993, NEC imepewa mamlaka ya kusimamia na
kuendesha uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ni. Imefanya kazi hiyo
pia tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na
uchaguzi wa kwanza kwa mfumo huo kufanyika mwaka 1995.
Mkurugenzi
wa Tehama wa NEC, Dk Modestus Kipilimba anasema hakuna yeyote asiye na
utambulisho halali atakayepiga kura na atakayekamatwa, atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
“Hairuhusiwi kutumia kadi isiyo
ya NEC. Orodha ya wanaostahili kupiga kura tunayo na elimu imeshatolewa
kwa wananchi kujiepusha na suala hilo, yeyote atakayekaidi atachukuliwa
hatua za kisheria. Lakini kwa uhakika, hakuna uwezekano kwa mtu yeyote
wa nje kufanikisha azma hiyo,” anasema Dk Kipilimba.
Katika
uandikishaji huo, NEC ilitumia teknolojia ya kisasa ya BVR na kila
mapigakura alipatiwa kadi mpya aina ya PVC yenye alama za kiusalama,
kuongeza uwezekano wa kukamatwa kwa atakayejaribu kughushi.
Licha ya tume hiyo kukabidhi kwa Jeshi la Polisi majina
ya watu 52,078 waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la
Kudumu la Wapigakura ili hatua stahiki zifuate, NEC imebainisha pia
maofisa watakaojihusisha na udanganyifu aina yoyote, nao watasombwa na
dhoruba hiyo.
Wakati wa ziara ya waandishi wa habari
katika Kituo cha Taarifa za Wapigakura cha NEC, ilielezwa kwamba
mtumishi yeyote atakayejihusisha na uchakachuaji wa daftari hilo,
atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka saba jela.
Sheria
hiyo imewekwa ili kuondoa uwezekano kwa watumishi 74,502 waliotumika
katika uandikishaji nchini kujihusisha na vitendo hivyo.
“Si
rahisi kuingiza maelezo ya mtu ambaye hakuwapo kituoni kwenye taarifa
za NEC. Licha ya kulindwa, utaratibu uliopo unashirikisha zaidi ya mtu
mmoja. Endapo kutakuwa na ‘mjanja’ yeyote, lazima tutambaini na sheria
itamalizana naye,” anasema Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Ramadhan.
Haki ya mpigakura
Siku
tisa zimebaki Watanzania kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua
rais, wabunge na madiwani watakaongoza kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo.
Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzanania katika Kifungu cha 61(3)(a) na (b) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi, vinampa kila mpigakura haki ya kupata elimu na taarifa sahihi
kwa wakati, kuhusu mchakato wa uchaguzi ikiwa pamoja na kushiriki
mikutano ya kampeni bila woga na kutoa maoni kwa uhuru na amani.
Sheria
pia, inamruhusu kumpigia kura kwa siri mgombea anayemtaka bila bugudha,
vitisho au woga na kulalamika juu ya mwenendo mbaya wa uchaguzi.
Kwa
watu wenye ulemavu, wagonjwa au wazee, sheria hiyo inatoa haki ya
kusaidiwa kupiga kura. Vilevile, NEC imeandaa vifaa ili kuwawezesha
walemavu hasa wasioona kutimiza wajibu huo wa kidemokrasia bila msaada
wowote.
Hata hivyo, ni vema mpigakura akajilinda dhidi ya matukio ya uvunjifu wa sheria, taratibu na kanuni siku ya uchaguzi huo.
Matukio
hayo ni pamoja na kufanya kampeni ya aina yoyote siku hiyo na kupokea
rushwa kwa ajili ya kupiga au kuacha kupiga kura. Wananchi pia
wanakumbushwa kuepuka kupokea chakula, vinywaji au takrima kwa ajili ya
kupiga au kutopiga kura.
“Ni kosa kupiga au kujaribu
kupiga kura zaidi ya mara moja, kununua, kuuza, kutoa kadi kwa mtu
mwingine au kumshawishi mtu asiye na sifa kupiga kura. Haitoruhusiwa
kutumia jina la aliyefariki au jina la uongo na kufanya kampeni au kuvaa
alama za chama cha siasa ndani ya mita 200 kutoka kituo cha kupigia
kura,” anasema Ramadhan na kuongeza:
“Tuliandikisha
watu zaidi ya watu milioni 23.7 na baada ya uhakiki na uchakataji wa
taarifa zote wamebaki milioni 22.75, hao ndiyo watakaoshiriki uchaguzi
huu. Mtu asiyependa matatizo ni vema akajiepusha na watu wenye dhamira
mbaya kama kughushi kadi.”
Ni jinai
Ili
ufurahie ushindi wa mgombea utakayemchagua na kuendelea kuwa salama
hata baada ya Oktoba 25 ni busara na hekima kuepuka kuvunja sheria kwani
ulinzi utakuwa wa kutosha maeneo yote wakati mchakato wa upigaji kura
ukitekelezwa.
Maelekezo ya NEC kuhusu upigaji kura kila
mpiga kura kukumbuka kituo alichopangiwa kupigia kura kulingana na
alikojiandikisha, ni mahali ambako jina lake litabandikwa na kuruhusiwa
kupiga kura.
Ikiwa siku ya kupiga kura jina
halitaonekani katika orodha iliyobandikwa kituoni, kuna uwezekano
mpigakura huyo amekwenda kituo ambacho hakujiandikisha wakati wa
uboreshaji wa BVR, hivyo ndiyo sababu NEC hubandika orodha kituoni kabla
ya uchaguzi ili kuondoa utata huo na kila mwananchi kujihakikishia yumo
kwenye orodha ya wapigakura.