ACT waahidi kuzalisha umeme wa upepo
Mgombea urais wa ACT- Wazalendo Anna Mghwira akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni .
-
Singida. Mgombea urais wa ACT- Wazalendo Anna Mghwira, ameahidi kuutumia upepo wa Mkoa wa Singida kuzalisha umeme wa uhakika.
Mghwira
alisema hayo jana alipozungumza na wakazi wa Singida Mjini na kuongeza
kuwa ni ndoto kuwa na nchi ya viwanda bila ya umeme na maji ya uhakika.
Alisema
badala ya kutegemea umeme wa maji ambao umeonyesha kushindwa,
inahitajika nguvu ya ziada kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa
kutumia vitu mbadala ukiwamo upepo wa Singida unaopotea bure.
“Nakumbuka
miaka ya 1980, kulikuwa na mradi wa umeme wa upepo, kutokana na
kutokuwa na mipango endelevu ya maendeleo, ilikufa. Sasa ACT- Wazalendo
itahakikisha inaifufua ili iende sambamba na upatikanaji wa umeme wa
uhakika,” alisema Mghwira.
Alisema mbali ya viwanda
watahakikisha kunakuwa na kilimo shirikishi kwa maana ya kusaidia
maendeleo na siyo kwa ajili ya chakula pekee.
Mghwira alisema kilimo hicho kitamuhusisha mkulima wa
kawaida na Serikali kwa utaratibu maalumu kupitia sera na kanuni za ACT
-Wazalendo.
“Kinachowatesa na kuwapa hasira wananchi ni
uwazi, vitu vingi vinafanywa kwa siri na kuwanufaisha wachache.
Serikali ya itaweka kila kitu bayana ili kuondoa ukakasi huo unaokatisha
tamaa kwa kuwakandamiza wengi,” alisema Mghwira.
Kuhusu
elimu, alisema wamejipanga kuwajali zaidi walimu kwa sababu wao ndiyo
chimbuko la kuwapo shule na wasomi wanaoisaidia nchi katika masuala
mbalimbali. Alisema bila kuwajali walimu kwa kuzingatia madai yao
ikiwamo nyumba, kulipwa kwa wakati na kupata vitendea kazi, haitakuwa
rahisi kuwa na wahitimu wanaoweza kupambana katika soko la ajira.
“Walimu
watakuwa na nafasi nzuri ya kujadili, kuwasilisha maoni yao na
kusikilizwa, huku mahitaji yao muhimu yakipewa kipaumbele,” alisema
Mghwira.
Mgombea mwenza wa ACT-Wazalendo, Hamad Yusuph
aliwaomba wananchi kumpigia kura Mghwira ili alete mabadiliko ya kweli.
Alisema wananchi wamechoka kudanganywa na huu ndiyo wakati wa kufanya
uamuzi sahihi.