MGAWANYO WA TANZU NA VIPERA VYA FASIHI SIMULIZI. M.M Mulokozi(1989)





 MGAWANYO WA TANZU NA VIPERA VYA FASIHI SIMULIZI.

 M.M Mulokozi(1989)


Katika makala hii tunaanza na kuelezea maana ya fasihi, fasihi fasihi simulizi kwa kutumia wataalam mbalimbali, baada ya kuelewa vizuri dhana hizi tutajadili vigezo vilivyotumika katika mgawanyo wa tanzu na vipera vya fasihi simulizi katika makala ya M.M Mulokozi (1989) na hatimaye tutaangalia ubora na udhaifu wa uainishaji wa tanzu hizo, na kumalizia na hitimisho, kielelezo na mwisho marejeo.
Fasihi ni sanaa itumiayo lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii bila kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa. Fasihi ambayo haijaandikwa ni fasihi simulizi na fasihi iliyoandikwa ni fasihi andishi.
Ama kuhusu Fasihi simulizi, Wamitila ( 2002) anaeleza kuwa Fasihi simulizi ni fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya mdomo kwa kusimuliwa, kuimbwa , kutongolewa au kughanwa.
Naye Mulokozi (1996) anaelezea kuwa fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo na vitendo bila maandalizi.
Kwa ujumla fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya masimulizi  ya mdomo na vitendo bila maandishi.
Katika makala ya M.M Mlokozi (1989) katika mulika ya 21 amejaribu kuzigawa tanzu za fasihi simulizi ya Tanzania katika tanzu zake mahususi kwa kuzingatia VIGEZO vifuatavyo;
Umbile na tabia ya kazi inayohusika;upande wa umbile na tabia ya kazi ya sanaa ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa na kuipa mwelekeo au mwenendo ilionao.Vipengele hivyo ni namna lugha inavyotumika(kishairi,kinathali,kimafumbo,kiwimbo, kighani nakadharika) pia muundo wa fani hiyo na wahusika kama wapo.
Kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira (hili linazingatia pia dhima yake kijamii) hapa Mulokozi amezingatia ukweli wa msingi kuwa fasihi simulizi ni sanaa inayo pita, isiyofungwa katika umbo maalum, wala matini maalum yasiyo badilika. Fasihi simulizi inatawaliwa na vitu muhimu vitatu yaani watu, wakati na mahali. Mwingiliano huu ndio muktadha, na muktadha ndio unaamua fani fulani ya fasihi simulizi ichukue umbo lipi? Iwasilishe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo.

Zifuatazo ni tanzu na vipera vya fasihi simulizi kama zilivyoainishwa na M.M.Mlokozi(1989) katika mulika 21 na jinsi alivyo ziainisha kwa kutumia vigezo hivi viwili, yaani kigezo cha umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishwaji kwa hadhira, na vipera vyake.
M.M.Mulokozi ameainisha tanzu sita ambazo ni; mazungumzo, masimulizi, maigizo (drama) ushairi semi na ngomezi (ngoma). Hivyo ufuatao ni uainishaji wa tanzu hizi za fasihi simulizi na vipera vyake kwa kutumia vigezo vya Mulokozi katika mulika ya 21.
Mazungumzo, ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida, juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi mazungumzo ili yawe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani, na uhalisia baada ya kuunakili.
Tanzu zinazoingia katika fungu la mazungumzo; Hotuba, Malumbano ya watani, Ulumbu, Soga na mawaidha. Katika kuainisha tanzu hizi ndani ya mazungumzo M.M.  Mulokozi ametumia vigezo vyote viwili; Hotuba, malumbano ya watani, ulumbu, soga na mawaidha. Kwa kuzingatia kigezo cha kwanza kinachozingatia msingi wa umbile na kazi inayohusika, tunaona tanzu hizi zote zina vipengele vya vinvyoumba sanaa na kuipa muelekeo au mwenendo ulionao, katika hotuba, malumbano ya watani, ulumbu, soga na mawaidha vyote vinavipegele vyake. Pia tanzu hizo zote zina maana ya lugha inayotumika. Mfano katika hotuba lugha rasmi ndiyo inayotumika, katika malumbano ya watani lugha ya kejeli mara nyingi ndio hutumika zaidi, mawaidha hutumia lugha rasmi au lugha za kikabila hutumika.
Pia katika kigezo umbile na tabia ya kazi inayohusika,katika kuainisha tanzu hizi mulokozi ametumia muundo wa fani na wahusika kama wapo.Tanzu zote hizo katika mazungumzo zina fani yake. Mfano katika malumbano ya watani ni tanzu inayozingatia fani zifuatazo; Kuna utani wa mababu, mabibi na wajukuu, utani wa mashemeji, utani wa kikabila na utanu wa marafiki. Kila kimojawapo kati ya fani hazi huwa na kanuni zake, miktadha yake na mipaka yake katika jamii zinazohusika.
Pia katika kuanisha tanzu za mazungumzo Mulokozi ametumia kigezo chake cha pili yaani kigezo kinachozingatia muktadha na namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira hili linazingatia pia dhima yake katika jamii kama ifuatavyo;

Ndani ya mazungumzo kuna hotuba, mawaidha, ulumbu, malumbano ya watani, soga; Tanzu hizi zote zinazingatia msingi wa fasihi kuwa ni sanaa inayopita, isiyofungiwa katika umbo maalum, wala matini yasiyobadilika. Mfano Hotuba ni sanaa inayopita, isiyofungwa katika umbo maaluma na matini yake hubadilika kulingana na matukio kama vile; matukio ya kidini, sherehe na kadharika. Hotuba hufuata wakati, watu na mahali. Katika kigezo hiki kinachozingatia muktadha na namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira huzingatia wakati, watu na mahali.Tunaona katika mazungumzo na tanzu zake zinazingatia wakati watu na mahali, mfano mawaidha huzingatia watu gani,wana umri gani, je ni vijana wa kiume au wa kike. Pia huzingatia mahali yaani tukio linapofanyika, mfano sebuleani au chumbani na pia wakati gani asubuhi, mchana au jioni.
Tanzu ya mazungumzo kwa ujumla imeainishwa kwa kutumia vigezo vyote viwili yaani kigezo cha umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo kinachozingatia muktadha na namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira.
Masimulizi; ni fasihi yenye kusimulia habari  fulani.  Mulokozi (1989) anasema kuwa masimulizi ni fasihi ya kihadithi na fani zake huwa na sifa zifuatazo; hueleza atukio katika mpangilio fulani mahsusi, huwa na wahusika yaani watendaji au watendwaji katika matukio yanayosimulia, hutumia lugha ya kimaelezo, utambaji wake au utoaji wake huweza kuambatana na vitendo au ishara, na huwa na maudhui ya kweli au ya kubuni na yenye mafunzo fulani katika jamii.

Katika mulika 21 Mulokozi amegawanya masimulizi katika tanzu zifuatazo; za kihadithi na Tanzu za Kisalua.
Katika tanzu za kihadithi amezigawa katika makundi yafuatayo;
Ngano  ni hadithi za kimapokeo zitumizo wahusika kama wanyama,miti na watu kuelezea au kuonya kuhusu maisha.Utanzu huu unajumuisha fani kadhaa kama vile; istiara,mbazi,na kisa.
Tanzu za kisalua zimegawanywa katika fani zifuatazo; visakale, tarihi, visasili,. Hivyo tunaona kuwa katika uainishaji wa tanzu hii ya masimulizi mulokozi ametumia vigezo vyote viwili kama ifuatavyo; katika msingi wa umbile na tabia ya kazi inayohusika Mulokozi ameonyesha vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa na kuipa mwenendo ulionao. Na vipengele hivyo ni kama; lugha ya kimaelezo, maudhui, matukio na wahusika.Pia ameonyesha namna lugha inavyotumika mfano. Ngano hutumia lugha ya kimaelezo na visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili. Vipera hivi vyote hutumia lugha ya kimaelezo.
Pia katika msingi wa umbile na kazi inayohusika, kigezo hiki huzingatia muundo wa fani na wahusika kama wapo.Tanzu ya masimulizi ina fani zifuatazo kutokana na Mulokozi. Hueleza matukio katika mpangilio fulani mahususi, huwa na wahusika yaani watendaji au watendwaji katika matukio yanayosimuliwa, utambaji au utoaji wake huweza kuambatana na vitendo au ishara, huwa na maudhui ya kweli au ya kubuni na yenye mafunzo fulani na hutumia lugha ya kimaelezo.   
Semi ni tungo au kauli fupifupi zenye kubeba maana fulani au mafunzo muhimu katika jamii, Mulokozi ameaimisha tanzu za semi kama ifuatavyo:-
Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa jamii. Methali huwa na sehemu mbili kwanza sehemu ambayo huanzisha wazo fulani sehemu ya pili ambayo hulikanusha au kulikamilisha wazo hilo. Methali ni utanzu tegemezi ambao kutokea kwake hutegemea fani nyingine mfano maongezi, majadiliano mazito, muktadha maalum katika methali Mulokozi ameainisha tanzu hii kwa kutumia kigezo cha umbile na tabia ya kazi inayohusika, katika kigezo hiki Mulokozi ameonyesha matumizi ya lugha. Mfano methali hutumia tamathali, sitiari na mafumbo. Pia methali huwa na wahusika wa fani zake zinazojitegemea. Mfano Haraka haraka / Haina Baraka. Wahusika kuna anayeuliza Haraka haraka na anayejibu Haina Baraka. Pia lugha aliyotumia katika methali hii ni lugha ya kinathari na kishairi.

Pia methali huwa na fani zake. Mulokozi anasema methali ni utanzu tegemezi ambao kutokea kwake hutegemea fani nyingine, fani hizo ni maongezi au majadiliano mazito, muktadha maalumu, huwa na sehemu mbili sehemu ya kwanza ambayo huanzisha wazo fulani na sehemu ya pili ambayo hulikamilisha au kukanusha wazo hilo.
Ndani ya kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishaji methali huwa na dhima ya kutoa mafunzo, kuadibisha, kuonya na kuhamasisha jamii. Methali huendana na wakati, watu na mahali kwa kuzingatia tukio pia huwa na matini yanayobadilika. Mfano Haraka haraka haina Baraka, methali hii inatoa onyo kuwa ukifanya jambo kwa haraka unaweza kukosea, hivyo polepole ndio mwendo.
Vitendawili; hizi ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili waifumbue. Fumbo hilo kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo na mara nyingi lina mafunzo muhimu kwa washiriki mbali na kuwachemsha akili zao.  Vitendawili hutegemea uwezo wa kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile, ni sanaa inayojitegemea, inayotendwa na ina jisimamia yenyewe.
Katika kigezo cha umbile na tabia inayohusika vitendawili hutumia lugha ya mafumbo na huwa na washiriki yaani wahusika ambao ni yule anayetoa kitendawili na anayejibu. Mfano  Mmoja huuliza Kitenawili na mwingine anajibu tega. Mfano; Kaa huku na mimi ni kae kule tumfinye mchawi (kula ugali), Mfano huu huhamasisha ushirikiano baina ya watu.
Pia vitendawili huwa na fani kama wahusika (pande mbili) wanaouliza na wanaojibu, muktadha maalumu (mazingira) katika muktadha na namna ya uwasilishaji Mulokozi amesema vitendawili huwa na mafunzo fulani zaidi ya chemsha bongo. Vitendawili huzingatia mazingira (mahali) watu na wakati maalum mfano watoto, mahali (shuleni au nyumbani) na huwa na wakati maalum.
Misimu, ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Msimu ukipata mashiko ya kutosha katika jamii hatimaye huingia katika kundi la methali za jamii hiyo. Mfano  Tamu tamu mahonda ukinila utakonda.

Katika kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira misimu ni sanaa inayopita isiyofungiwa katika umbo maalum wala matini maalum yasiyobadilika. Misimu ina dhima ya kutoa mafunzo, kuonya, hutumika katika siasa pia misimu huenda na wakati, watu na mahali. Mfano Matteru (1987) anasema ‘tamu tamu mahonda ukinila utakonda’ . Katika  mfano huu unaonyesha madhara ya pombe iliyokuwa inatengenezwa na kiwanda cha mahonda (Zanzibar). Katika kigezo cha umbile na tabia ya kazi inayohusika misimu hutumia lugha isiyosanifu kwani huzuka na kutoweka mfano; mdebwedo, utajiju, yeboyebo,  buzi na kimeo.
Mafumbo ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake ni za ndani na zimefichika. Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalum hivyo ni tofauti na methali ambazo ni semi za kimapokeo. Katika kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishwaji mafumbo huwa na dhima ya kutoa maonyo na mawaidha kwa jamii kwani hubuniwa kwa hadhira maalum. Mfano  Mbele ya bata kuna bata na nyuma ya bata kuna bata, jumla nina bata wangapi’?  Fumbo hili huonyesha umakini katika katika kufanya kitu. Katika mafumbo ndani ya kigezo cha umbile na tabia ya kazi inayohisika huangalia namna lugha inavyotumika, katika mafumbo ambayo maana yake ya ndani imefichika mafumbo huundwa na wahusika na fani yake. Mfano yule anayetoa fumbo (anasema fumbo mfumbie mjinga ) Yule anayejibu (mwerevu ataling’amua) hapa anamainisha mjinga hawezi akalifumbua fumbo ila mwerevu hulifumbua pia mjinga anaweza akadanganywa ila mwerevu hawezi kudanganywa. Fumbo hili linahamasisha mtu afanye juhudi katika mambo ili afanikiwe kama mwerevu.
Lakabu ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au kujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina haya huwa ni sitiari. Majina haya huweza kumsifia mtu au kumkosoa. Mfano Mkuki uwakao – Jomo Kenyatta, Sakarani – mlevi, Simba wa yuda – Haile sellasie.
Katika kigezo cha umbile na tabia inayohusika Mulokozi ameonyesha lakabu hutumia maneno yenye maana iliyofungwa na sitiari, pia lakabu huwa na wahusika yule anayepewa sifa. Mfano mkuki uwakao – Jomo Kenyatta na anayetoa sifa.
Katika muktadha na namna ya uwasilishaji lakabu huwa na dhima mbalimbali kama kusifia, mfano baba wa taifa, inatoa sifa ya utendaji bora wa kazi, simba wa yuda inaonyesha mshupavu. Mkuki uwakao inaonyesha kiongozi  mchapa kazi. Pia lakabu hukosoa na kuonya mfano sakarani- ulevi hapa inaonyesha kuwa mtu mlevi hafai katika jamii. Lakabu huwa na matini yanayobadilika, hivyo ni sanaa inayopita, lakabu hufuata watu wakati na mahali.
Ushairi, ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo mashairi na tenzi. Zaidi ya kuw na vina ushairi una ufasaha wa kuwa na maneno machache au muhtasari mawazo na maono ya ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu. Mulokozi (1989) anasema ushairi hupambanuliwa na lugha ya kawaida kwa kutumia lugha na mbinu za kimuktadha. Kauli za kishairi hupangwa kwa kufuata wizani maalumu na mawimbi ya sauti na mara nyingi lugha ya mkato na mafumbo hutumika ushairi una fani zinazoambatana na muziki wa ala na wakati mwingine hupata wizani wake kutokana na mapigo ya muziki huo wa ala. Mulokozi (1989) amegawa ushairi katika mafungu mawili ambayo ni nyimbo na uwasilishaji.
Nyimbo ni kila kinachoimbwa hivyo hii ni dhana panainayojumuisha tanzu nyingi za kinathari kama vile hadithi huweza katika kundi la nyimbo pindi zinapoimbwa . Vipera  vya nyimbo ni tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
Katika kuainisha tanzu hiii ya nyimbo Mulokozi  ametumia vigezo vyote viwili, tukianza na kigezo cha kwanza ambacho ni umbile na tabia ya kazi inayohusika Mulokozi ameonyesha jinsi vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa na kuipa mwelekeo. Vipengele vilivyo katika nyimbo ni namna lugha inavyotumika .
Mfano: nyimbo za maombolezo hutumia lugha za maombolezo yenye maneno ya  Kufariji  tofauti na nyimbo za sherehe huwa na lugha ya furaha na  kuchangamsha.
Katika kigezo hiki pia cha umbile na tabia ya kazi inayohusika Mulokozi ameonyesha muundo wa fani na wahusika katika nyimbo.  Mfano: mambo muhimu yanayotambulisha nyimbo ( fani ya nyimbo) Muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji( wahusika), Muziki wa ala (kama ipo), Matini au maneno yanayoimbwa,Hadhira inayoimbiwa,Muktadha unaofungamana na wimbo huo mfano sherehe, ibada na kilio.
Pia Mulokozi katika kuainisha tanzu ya nyimbo ametumia kigezo cha pili yaani muktadha na namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira katika kuainisha tanzu hii ya nyimbo amezingatia wakati, watu (wahusika) na mahali. Pia nyimbo ina matini yanayobadilika, yasiyofungiwa katika umbo maalumu yaani ni sanaa inayopita.
Mfano: kuna nyimbo zinazoimbwa kwa kufuata wakati wake, mahali mahususi, na mahali maalumu, mfano wawe na vave hizi ni nyimbo za kilimo, mbolezi hizi ni nyimbo za kilio au maombolezi. Mbolezi huimbwa wakati maalumu, na waombolezaji ambao ni watu( wahusika) na mahali maalumu (mfano msibani)
Maghani ni ushairi unaotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Zipo maghani za aina mbili, kuna maghani ya kawaida, ambayo huundwa na fani mbalimbali za ushairi simulizi mfano mapenzi, siasa, maombolezo, kazi za dini na kadhalika. Maghani ya masimulizi hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au matukio fulani ambayo huambatana na nyimbo. Tanzu za maghani ni sifo, vivugo, tondozi, rara, ngano na tendi.
 Maghani ni tanzu iliyoanishwa kwa kutumia kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishwaji wake kwa hadhira. Molokozi ameonyesha maghani huwasilishwa kwa kalima badala ya kuimba, pia dhima za maghani ni kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa kuzingatia matukio
Mfano uhuru  kesi za mauaji
Mulokozi anasema maghani huundwa na fani mbalimbali za ushairi simulizi mfano mapenzi, siasa, maombolezo, kazi na dini. Zifuatazo ni fani za ushairi simulizi ambazo ni, Masimulizi hutolewa kishairi, huhusu matukio muhimu ya kihistoria au jamii, huelezea habari za ushujaa na mashujaa, huwasilishwa kwa kughanwa (ala ya muziki), hutungwa papo kwa papo.
Pia maghani huwa na wahusika, na huambatana na muziki wa ala. Mulokozi anasema mutambaji wa ghani hizi huitwa Yeli au Manju na kwa kawaida huwa ni bingwa wa kupiga ala fulani ya muziki (mtambaji huyu ndiye mhusika mkuu)
Maigizo, (drama) ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia au matendo ya watu na viumbe wengine ili kiburudisha na kutoa ujumbe fulani. Maigizo ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi. Mulokozi anasema drama (maigizo) ya kiafrika huambatana na ngoma mtambaji wa hadithi au matendo ya kimila. Kwa  mfano jando na unyago , yapo maigizo yanayofungana na michezo ya watoto, uwindaji , kilimo, na kadhalika. Drama hutumia maleba maalumu kama vizuizui (mask).
Katika kuainisha tanzu hii mulokozi ametumia vigezo viwili,kwa kuanza na kigezo cha kwanza Mlokozi ameainisha,mambo na vipengele vinavyopatikana ndani ya maigizo ambavyo ni maigizo yanayohusu matendo ya kimilana michezo ya watoto,matanga, uwindaji, kilimo na nyinginezo.
Kwa msingi wa umbile na tabia inyohusika vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa na kuipa muelekeo tanzu hii ya maigizo ni lugha inavyotumika katika kuigiza fani na wahusika mfano wahusika wa maigizo wapo na hawa ndio watendaji wakuu katika kufikisha ujumbe. Maigizo hutumia lugha mfano lugha ya kejeli na hata lugha rasmi pia maigizo huwa na fani inayotendwa.
Mulokozi Pia katika kuainisha tanzu hii ya maigizo ametumia kigezo cha pili kinachozingatia muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira, maigizo ni sanaa inayopita isiyofungiwa kaika umbo maalum wala matini yasiyobadilika ila maigizo hubadilika kutokana na tukio linaloigigwa na kuzingatia wakati, watu na mahali mfano maigizo huhitaji sehemu maalumu (jukwaa au uwanja wa kutendea) , wahusika ambao ndio waigizaji wakuu na pia maigizo huenda na wakati.
Ngomezi ni midundo Fulani ya ngoma kuwakilisha kauli Fulani katika lugha ya kabila hilo. Mara nyingi kauli hizo huwa ni za kishairi au kimafumbo
Mulokozi ametumia vigezo vyote viwili katika kuainisha tanzu hii, kwa kuanza na umbile na tabia ya kazi inayohusika ameangalia vipengele ndani vinavyoiumba sanaa na kuipa mielekeo na mienendo ulionao.Vipengele hivyo ni namna lugha inayotumika, kishairi, kinathari, kimafumbo, kiwimbo au kighani. Mfano, katika ngomezi hutumia lugha na kauli za kishairi au kimafumbo.
Pia kigezo hiki huangalia fani na wahusika kama wapo, katika ngomezi huwa na wahusika ambao hupiga na kuandaa ngoma hizo.hii hujionyesha katika  utofauti wa upigaji wa ngoma hizi kutokana lengo lake  ambapo inaweza kutoa taarifa, tahadhari au ngomezi za uhusiano.
Katika kigezo cha pili muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira Mulokozi ameonyesha jinsi ngomezi ilivyo ni sanaa ambayo huandaliwa kwa matukio maalum. Pia ngomezi hutawaliwa na vitu vitatu muhimu katika kigezo hiki ambavyo ni watu, wakati na mahali.
M.M Mulokozi katika mulika amejitahidi kuelezea na kuzigawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kwa kuzingatia vigezo vyote viwili, yaani umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.
Pamoja na kujitahidi huko, kuna baadhi ya mapungufu ambayo yamejitokeza kama;
Mulokozi ameonyesha utenzi wa ngomezi, ila hajayuonyesha vipera au vitanzu vinavyojitokeza au kupatikana katika utanzu huu.
Mulokozi ameainisha na vipera vya fasihi simulizi lakini yeye mwenyewe anakiri kuwa bado hakuna wataalamu walioshughulikia suala hili undani zaidi kwani tanzu za fasihi simulizi hutifautiana kati ya jamii na jamii, Hivyo Mulokozi ameonyesha udhaifu wa kitaaluma
Mulokozi ameshindwa kutofautisha istilahi ya Tanzu na Vipera. Badala ya kutumia vipera yeye ametumia tanzu: vipera vya hadithi yeye anasema fungu au tanzu za kihadithi.
Mulokozi pia ameonyesha udhaifu pale anaposema misimu ikipata mashiko huingia kwenye methali, wakati misimu ikipata mashiko ya kutosha si lazima kuingizwa kwenye methali tu bali huingizwa kwenye msamiati wa lugha sanifu mfano: ngunguli, ngangali na ulanguzi
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, uainishaji wa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kama vilivyoainishwa na Mulokozi vinaingiliana kifani na  kimaudhui.
KIELELEZO KINACHOONYESHA TANZU NA VIPERA VYA FASIHI SIMULIZI.
MAREJEO
Mulokozi, M.M. (1989) Tanzu za Fasihi Simulizi Mulika 21:1-24, Dar es salaam: TUKI.
Mulokozi, M.M. (1996) Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Dar es salaam
Wamitila, K.W.(2002) Uhakiki wa Fasihi Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi, Phoenix, 
                         Publishers Ltd.

NADHARIA ZA UCHAMBUZI WA FASIHI


Wataalamu mbalimbali wameainisha nadharia mbalimbali za uchambuzi wa kazi yoyote ya fasihi. Miongoni mwa nadharia hizo ni pamoja na;
Nadharia ya umuundo (structuralism)
Umuundo ni nadharia inayojibainisha kwa kuangalia Ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu kizima. Kwa mfano muungano wa maneno hufanya sentensi na sentensi zikiungana zinaunda aya au onesho na onesho kuunda tamthiliya.
Ntarangwi (2004) anasema kuwa umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi.
Mwasisi anayetajwa sana katika nadharia hii ni Ferdinard De saussure aliyependekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole' na `langue' kueleza maoni yake: `Parole' au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa kinadharia unaounda lugha zote au `Langue' - yaani masharti au kaida zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi.
Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii . Hasa alichotaka kuendeleza kidhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep).
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na Sasiolojia.
Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake.
Katika kupata maana lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna DHANA, ALAMA na KITAJWA.
UMUUNDO NA FASIHI
Kama vile muundo wa lugha ulivyo mfumo, muundo wa fasihi pia una vipengele vinavyotegemeana na vinavyoelezwa katika muktadha wa vipengele vingine. Katika kazi ya fasihi kuna kitengo cha kisanaa kama vile maudhui, ploti, wahusika, muktadha na lugha. Hakuna kipengele cha fasihi kati ya hivi kitakachoelezwa katika upekee wake. Lazima kielezwe kwa kuzingatia kuwepo kwa jukumu la vipengele vingine. Kwa mfano katika kueleza au kuzungumzia ploti, wahusika watashirikishwa na lugha yao kuzingatiwa.
Kwa hiyo nadharia ya umuundo husisitiza vipengele vya kazi ya sanaa, jinsi vinavyohusiana hadi kuikamilisha kazi hiyo. Huangalia namna sehemu mbalimbali za kazi za sanaa zilivyofungamana. Yaani Neno halihitaji urejelezi ili lipate maana, na Kazi yenyewe ilivyoundwa ndivyo hutoa maana. Yaani maana inavyoumbwa ina dhima kubwa kuliko maana yenyewe.
Wafula na Njogu (2007) wanasema kuwa Umuundo unapinga wazo la kijadi linalodai kwamba fasihi ni tokeo la mchango wa maudhui na fani. Dhana ya kimapokeo kuhusu fasihi inadai kwamba fasihi ni umbo lenye viungo viwili, maudhui na fani na kwamba viungo hivi vyaweza kutenganishwa.
Wahakiki wanoegemea mkondo wa Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. Wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili kinachoweza kuhakikwa kivyake. Hivyo basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za jinsi matini hiyo hufanya kazi.
Mhakiki anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki wake. Kwa hivyo wahakiki wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini peke yake huku wakiepuka kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanya kazi.
Hata hivyo, huenda njia hii isiwe ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe haiwezi kabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile mazingira yake (Ntarangwi 2004).
Nadharia ya umarx (marxism)
Kwa maana rahisi kabisa, tunapoongelea kuhusu nadharia ya U-Marx tuna maana ya kurejelea mikabala mbalimbali ambayo misingi yake mikuu ni mawazo yanayohusishwa na Carl Marx na Friedrich Engels.  Katika kitabu cha The Germany Ideology, Marx na Engels walisema kuwa kitu cha msingi katika maisha ya binadamu ni kula na kunywa, kupata malazi na mavazi na mambo mengine. Tendo la kwanza la kihistoria kwa hiyo ni kutafuta njia ya kuyakidhi mahitaji haya ya msingi. Ili kufanikiwa katika lengo hilo, binadamu hulazimika kujiunga pamoja au kuunda umoja ili kuimarisha umoja na wepesi wa kuizalisha mali ya kukidhi mahitaji hayo. Muungano huo huwa na ugawaji wa majukumu au kazi ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa matabaka katika jamii. Hatua ya juu ya mwendelezo huu ni uzukaji wa mfumo wa ubepari. Katika mfumo huu, mali inamilikiwa na idadi ndogo ya watu. Watu hao wanaipata mali yao kutokana na unyonyaji wa umma na hasa wafanya kazi (Wamitila 2002:).
Kwa mawazo ya Marx,  maendeleo ya jamii huthibitika katika vipindi vya maisha ambavyo kizazi cha binadamu kimepitia. Kutokana na Marx tabaka la jamii hutoweka na lingine huchipuka kwa sababu ya mgongano wa kitabaka. Mgongano huu hutokea kwa sababu kuna tabaka la wanyonyaji na wanaonyonywa. Hivyo, inabidi kuwa na mapinduzi dhidi ya mifumo ya kuzalisha mali inayohimili unyonyaji. Mapinduzi yanayotokea baadaye yanaongeza tumaini la ujenzi na uimarishwaji wa jamii inayozingatia usawa. Marx anamwona binadamu kuwa kiini cha historia yote na matendo yote yanayotendeka humu duniani. Umarx unamwabudu binadamu, hivyo humpa tumaini binadamu la kung’oa mizizi yote ya unyonyaji na unyanyasaji na kujenga ulimwengu wa kinjozi usiokuwa na madhila (Wafula na Njogu 2007). Vidato ambavyo jamii ilipaswa kupitia kabla ya kufikia ukamilifu wa kinjozi ni vifuatavyo: Ujima, Utumwa, Umwinyi, Ubepari, Ujamaa na Ukomunisti
Kwa jumla, twaweza kusema kwamba mhakiki wa Ki-marx hukita nadharia yake kwenye itikadi za Karl Marx na Fredrick Engels, na hasa kwenye madai ya hao wawili kuwa, katika tathimini ya mwisho kabisa maendeleo ya historia ya binadamu pamoja na taasisi zake, yatakuwa ni tokeo la mabadiliko katika njia za kimsingi za uzalishaji mali. Kwamba mabadiliko kama hayo husababisha mageuko katika muundo wa matabaka ya kijamii ambayo katika kila kipindi huendeleza kung'anga'aniwa kwa uwezo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii; na kwamba dini, fikra na utamaduni wa jumuiya yoyote (zikiwemo sanaa na fasihi kwa kiwango fulani) huwa ni `itikadi' na miundo maalum ya `kitabaka' ambayo ni zao la miundo na matabaka ya kijamii yaliyomo wakati huo.
Umarx huchukulia kwamba jamii zote za kitabaka huzalisha mkururo wa miundo ya urazini inayokinzana na kushindana. Katika jamii ya kikapitolisti, kwa mfano, aina tofauti za mitizamo kuhusu maisha huwakilisha haja tofauti za kitabaka ambazo hutegemea hasa mikinzano kati ya mapato na nguvu za kutenda kazi. Kwa hivyo Umarx huhusisha itikadi na uzalishaji mali na jukumu lake katika mivutano ya kisiasa katika jamii. Jinsi watu binafsi wanavyoelewa msingi wa maisha yao hutokea kuwa kamba ya mvutano ambapo wanaweza ama kubadilika au kuendelezwa.
HOJA ZA UMARX KWA UFUPI
i/ Katika historia ya mwanadamu, jamii na mahusiano yake, taasisi zake namna yake ya kufikiri; mambo yote hayo hutegemea mabadiliko ya mfumo wa uzalishaji mali. Yaani jinsi uchumi, uzalishaji, mgawanyo na umilikaji mali unavyoendeshwa.
ii/ Mabadiliko ya kihistoria katika msingi wa uzalishaji mali yanaathiri mabadiliko ya muundo wa matabaka ya jamii, na hivyo hutokeza (kwa kila wakati) tabaka tawala na tawaliwa ambayo huwamo katika mapambano na harakati za kugombea uchumi, siasa na faida za kijamii.
iii/ Urazini wa mwanadamu umeundwa na itikadi. Imani, thamani ya kitu, namna za kufikiri na kuhisi. Ni kupitia hivi, mwanadamu huuona ulimwengu wake, na huelezea yale yaliyomzunguka na yale anayoyaona kuwa kweli.
Kwa hiyo wazo kuu la U-Marx ni kwamba hata waandishi wa mkondo huo huandika kwa kutumia falsafa ya Marx jinsi alivyoiona historia ambapo wazo kuu ni kuwa: harakati za matabaka ndio msingi mkuu unaofanya mambo yawe kama yalivyo.
Umarx katika Fasihi
§  Usanii ni uumbaji wa Ukweli katika maisha.
§  Ukweli unaooneshwa katika kazi za fasihi hiyo ni usahihi wa mambo katika jamii? Kama ni Riwaya, Tamthilia, Ushairi na kadhalika inawakilishaje ukweli?
§  Kazi za kisanaa zinatakiwa kuonesha mivutano iliyopo katika jamii hasa kati ya wanyonyaji na manyonywaji.
Nadharia ya urasimi
Kwa mujibu wa Njogu na Wafula (2007) Urasimi ni wakati maalumu ambapo misingi ya kazi za sanaa huwekwa na kukubalika kuwa vipimo bora kwa kazi nyingine. Hii ina maana kwamba kila jamii ina urasimi wake. Urasimi katika Kiswahili ulikuwepo kati ya karne ya 18 na karne ya 18. Nao urasimi wa Kigiriki ulikuwepo baina ya karne ya nne (KK) na takriban karne ya nne (BK). Ieleweke kuwa si sahihi kuamini kama baadhi wanavyodhani kuwa unapozungumzia urasimi, huwa na maana ya msingi ya kitaaluma iliyowekwa na Wagiriki na Waroma wa kale.
Sifa za urasimi kwa ujumla
Pamoja na kwamba imeshatajwa hapo mwanzo kuwa kila jamii ina urasimi wake, lakini bado tunaweza kutoa sifa za jumla za urasimi mahali popote ulipo. Kwa mfano:
  • Kazi ya kirasimi huwasilishwa katika lugha inayoeleweka  kwa urahisi. Hii ina maana kuwa wazo linaelezwa moja kwa moja. Mitindo ya Kinjozi (mf. Nagona, Mzingile, Bina-Adamu, Walenisi)  haitumiwi. Uhalisia unasisitizwa.
  • Kazi nyingi za kirasimi hazichoshi kusoma. Hii ni kwa sababu kazi hizi ni kazi bora. Husomwa mara nyingi na watu wengi na kila unapoisoma wazo jipya hupatikana.
  • Fani na maudhui katika kazi za kirasimi ni mambo yaliyofinyangwa kwa kutumia mbinu kamilifu na teule. Daima kuna ufungamano uliokamilika kati ya kinachoelezwa na jinsi kinachoelezwa.
Katika urasimi wa Kigiriki watu mashuhuri ambao walikuwa wanarejelewa sana ni kama Plato, Aristotle, Horace na Longino. Kazi maarufu kwa upande wa Tamthilia inayoweza kutumika kama mfano wa urasimi wa enzi hizo ni kama ile ya Sofokile iitwayo Mfalme Edipode (1971) iliyotafsiriwa na Samuel Sateven Mushi.
URASIMI WA KISWAHILI
Njogu na Wafula (2007) wanasema kuwa kazi za kirasimi katika fasihi ya Kiswahili zipo.  Hata hivyo uhakiki wa kirasimi kuhusu kazi hizo ni nadra kupatikana. Msomaji wa kazi za kirasimi katika fasihi ya Kiswahili anapaswa kuhitamidi uhakiki wake kutokana na utunzi wenyewe. Urasimi wa Kiswahili ulifikia kilele chake katika karne ya 18 na 19. Kazi zinazodhaniwa kuhusishwa na urasimi wa Kiswahili ni pamoja na hizi: Utenzi wa Al-Inkshafi, Utenzi wa Hamziyya, Utenzi wa Mwanakupona. Kazi za watunzi wa mashairi ya unne (tarbia) kama Muyaka wa Muhaji, Mohammed Mataka na Ali Koti, “Sheria za kutunga mashairi na Diwani ya Amri” (1954) (Amri Abeid).
Kazi zingine za kirasimi kwa mujibu wa Njogu na Wafula (2007:21) ni kama vile riwaya za; Kiu (M.S.Mohamed, 1972), Utengano (S.A. Mohamed, 1980), Harusi za Buldoza na Hadithi nyingine (S.A. Mohamed, 2005)
Pia tamthilia kama: Kinjeketile, Mashetani (E.N. Hussein, 1969, 1971), Kilio cha Haki (A.M Mazrui, 1982), Sauti ya Dhiki (A.Abdalla, 1973).
Sifa ya fasihi ya Kiswahili katika misingi ya Kirasimi
·         Huu ni wakati ambapo misingi ya ushairi andishi wa Kiswahili ilipowekwa.
·         Mengi ya mashairi ya kirasimi yalipokezwa kwa mdomo na uhakiki pia ulifanywa kwa njia ya kimasimulizi.
·         Mashairi yalitumia lugha teule
·         Warasimi wa Kiswahili walitumia lugha rahisi iliyoeleweka na ujirani wao bila shida yoyote.
·         Masimulizi marefu kama vile utenzi yana mwazo, katikati na hatimayake.

JE ONTOLOJIA YA KIAFRIKA INAWEZA KUTUMIKA KAMA NADHARIA YA KUCHAMBULIA KAZI ZA FASIHI ZA KIAFRIKA?.


Katika kueleza mada hii tutaanza na ufafanuzi wa maana ya falsafa.
Wikipedia kamusi elezo huru wanasema,falsafa ni neno linalotokana na neno la kigiriki lenye maana ya upendo na hekima,wanaendelea kusema kuwa falsafa ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili inayafuata njia ya mantiki .Falsafa huchunguza mambo kama vile kuweko,au kutokuweko,ukweli,ujuzi ,uzuri,mema, na mabaya,lugha na haki.
Kwa mujibu wa Wamitila (2003 ) anasema, falsafa ni mawazo anayoyaamini mtu au mwandishi  kuwa yana ukweli unaotawala misingi ya maisha.
Hivyo, Falsafa ni taaluma au mtazamo unaochunguza matumizi ya dhana,kupima hoja,mbinu za ujengaji hoja,kufanya uhakiki au tathimini,kuthibitisha au kutoa ushahidi wa hoja zinazozungumzwana nadharia mbalimbali zinazohusu maisha.Mfano,kuua ni tendo zuri au sio zuri?
Pia fasihi ya Fasihi ya Afrika, tunaweza kusema inamaanisha maandiko kuhusu na kutoka Afrika. Kama George Joseph anavyodokeza katika ukurasa wa kwanza wa sura yake katika kitabu chake cha ‘understanding contemporary Afrika’ wakati mtazamo wa fasihi ya ulaya kwa ujumla inahusu herufi zilizoandikwa, dhana ya Afrika inahusu fasihi simulizi.Pia ansema fasihi inaweza kuashiria matumizi ya maneno kisanaa kwa ajili ya sanaa pekee.
Kwa ujumla Fasihi ya Afrika ni sanaa yoyote, au fashi yoyote ile inayopatikana katika bara la Afrika.
Pia istilahi Nadharia, Kwa mujibu wa TUKI (2004), Wanasema nadharia ni mawazo, maelezo, mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza,kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Nao Njogu na Rocha (2008), wanasema nadharia ni kioo cha kumulika kila jambo au tendo limuhusulo binadamu ulimwenguni  inakuwa ngumu gizani.
Pia Wamitila (1996), Anasema kuwa, nadharia ni maarifa ya kitaalamu ambayo msomaji au mhakiki anapaswa kuyajua na kuyafahamu kabla ya kuanza kazi zake.
Hivyo basi sisi tunakubaliana na TUKI, kwa kusema nadharia ni mawazo, maelezo,mwongozo uliopagwa ili kusaidia kueleza,kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Ama kuhusu Ontologia huu ni moyo wa falsafa. Ontologia ni tawi la falsafa ambalo huchunguza asili ya vitu, (binadamu ametoka wapi?,dunia imetoke wapi?,shetani ni nini?) Pia huchunguza uwepo wa vitu mbalimbali,vitu vilivyo hai na vitu visivyokuwa hai, vinavyoonekana na visivyoonekana.
Maana ya Ontologia tunaweza kusema ni falsafa ya utafiti wa asili nya kuwa wakati wa kuwepo au ukweli.wanaendelea kusema neno ontolojia asili yake ni kigiriki.
Ontolojia, pia ni nadharia ya vitu na mahusiano yao,inatoa vigezovya kubainisha aina tofauti ya vitu (halisi na kufikirika,uwepo na haipo,kweli na bora,kujitegemea na tegemezi) na mahusiano yao.
Naye Mihanjo A, (2010) akimnukuu Anselm katika nadharia yake ya kiontolojia,anselmamethibisha ontolojia kwa kuonyesha uishi wa Mungu.Anselm ameelezea na kuonyesha asili na uishi wa Mungu.
Kwaujumla Ontolojia  ni tawi la falsafa ambalo huchunguza asili ya vitu,(binadamu ametoka wapi?,dunia imetoke wapi?,shetani ni nini?)pia huchunguza uwepo wa vitu mbalimbali,vitu vilivyo hai na vitu visivyokuwa hai,vinavyoonekana na visivyoonekana.
Mkondo tulioutumia ni mkondo wa falsafa za kijamii na kisiasa . Mkondo huu unazingatia na kuangalia falsafa za jamii na siasa. Mkondo huu umefafanuliwa na kuelezwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Keneth  Kaunda na Kwame Nkurumah.
Tukianza na ; Mwalimu Julius Kambalage Nyerere ambaye anatetea mkondo huu kwa vigezo vifuatavyo;
Anadai kuwa ujamaa wa kiafrika ni kama Afrika pana ujamaa ambao unakuwa mwendelezo wa kifamilia na kuishi vizuri na watu vilevile anadai kuwa si ujamaa wa kimax ambao unatetea mgogoro wa kitabaka.Yeye anaona asili ya ujamaa ni jamii za kiafrika.
Sera ya mipango inajadiliwa na kurekebishwa na watu wote.Kila mtu alifanya kazi  katika ardhi ya jamii nzima na kila mtu alipata matunda kulingana na kazi yake.
Anaendelea kusema, ujamaa ni tofauti na ubepari unaolenga kumnyonya mtu.Hivyo wito wake ni kuishi katika umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.
Mtaalamu mwininge ni Kwame Nkurumah ambaye ametumia vigezo vifuatavyo;
Anadai kuwa ujamaa ulikuwa msingi  wa jamii za kiafrika kuliko ubinafsi hivyo ubepari utaiharibu Afrika, Afrika haita kuwa huru ikiwa itaendelea kuwa chini ya ubepari wa kimagharibi.
Huyu aliathiriwa na falsafa ya kimarx na renin lakini hakutaka kuitumia kama ilivyo alitaka uimalishwe ujamaa wenye asili ya kiafrika na vipengele vya kiislam na kikristo vya ulaya.
Keneth Kaunda alisema waafrika walifanikiwa  kuushinda ukoloni kwa sababu ya utu na sio nguvu katika kufikia ukamilifu wa utu binadamu lazima alenge kufanana na mungu. Mungu ni usawa wa kila kitu,mungu ni amani,upendo na utu,utu unavileta pamoja dini na siasa na kuzaa taifa la watu wanaopendana.
Anamalizia kwa kusema kuwa nguvu katika kujikomba si mbinu sahihi ya ukombozi bali nguvu inaweza kutumika katika kujilinda  aliandika  African humanism.
Baada ya kueleza mkondo na vigezo vya wataalam wa falsafa za kijamii na siasa ,tunachambua riwaya ya kufikirika ambayo ni kazi ya fasihi ya kiafrika kwa kutumia mkondo wa falsafa za kijamii  na kisiasa.
Riwaya ya kufirika ameandikwa na Shahban Robert chapa ya nne mwaka (2008) kufikirika ni riwaya inayohusu maisha na maswaibu yaliyo mkuta mfalme na malkia wa kufikirika kwa kuchelewa kupata mototo.
Uchambuzi wetu unaanza kama ifuatavyo;
Suala la imani, imani ni kuwa uhakika wa mambo yatarajiwayo. Nyerere anasema kuwa kila mtu alifanya kazi katika ardhi ya jamii nzima na kila mtu alipata matunda ya kazi yake. Katika riwaya hii( uk3-4), unaonyesha jinsi ,mfalme anavyoamini kuwa na watoto wengi ndio nguvu ya ufalme wake pia mfalme aliamini waganga, kafara,ramli,hirizi,mazinguo,mashetani na watabiri.(Uk 8-11), ndio maana mfalme aliwaita waganga wote wafike kwake ili waweze kuagua na kutabiri juu ya utasa na ugumba wao.
Utawala, katika riwaya hii mwandishi ameeleza suala la utawala kwa kumtumia mfalme kama mfano wa mtawala mwenye uongozi mbovu wenye mabavu “(uk 4) mfalme alipoamua waitwe waganga wote wa jadi mfano waganga wa mashetani,makafara,watabiri,hirizi,wa mizizi,mazinguo na mashetani asiye hudhulia apewe adhabu pia katika uk(23-25) mfalme anamfukuza mwalimu kazi.
Suala la ukombozi,ukombozi ni hali ya kujitoa kutoka hali  fulani kwenda hali nyingine .Katika riwaya hii kuna ukombozi wa kisiasa,mwandishi amemtumia mjinga,ameonyesha jinsi mjinga alivyosimama kisheria dhidi ya kifo kilichokuwa kinawakabili,kifo  ambacho hakikuzingatia utu wa binadamu (uk38.)KenethKaunda ansema, waafrika walifanikiwa kuushinda ukoloni kwa sababu ya utu sio nguvu,katika kuufikia ikamilifu wa utu binadamu lazima alenge kufanana na Mungu.
Matabaka katika jamii, matabaka ni mgawanyiko wa makundi ya watu  (kiuchumi,kisiasa,kielimu na kijamii) katika jamii. Katika riwaya hii kuna matabaka makuu mawili,tabaka la kwanza ni tabaka tawala,ambalo liliundwa na viongozi wa serikali, wanasheria,mahatibu na wafanya biashara,tabaka tawaliwa lilikuwa ni wakulima,(tabaka la mwisho),(uk 35-36).Matabaka katika jamii hayafai kwani huondoa umoja,Nyerere anapinga matabaka hivyo wito wake ni kuishi katika umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.
Athari za uongozi mbaya, huu ni uongozi usiofuata haki za raia wake, baada ya maamuzi ya mfalme kuwaruhusu waganga mfano;waganga wa mizizi walichimba mzizi ya mti,walitoa magome na kukata matawi ya miti,hali iiliyopelekea ukame wa  nchi na uharibifu wa mazingira na makazi ya wanyama,waganga wa kafara walitumia pia kwa moto na walihitaji damu za wanyama kwa ajili ya kafara,hivyo wanyama wengi walikufa.Ni vizuri kufikiri jambo kabla ya kutenda.
Umuhimu wa uzazi, katika riwaya hii mfalme aliona fahari yake yote si kitu kwani alikosa kuwa na mtoto (uk 1-3) anasema, “Nina majeshi ya askari walioshujaa, waongozi hodari raia wema,watii ambao hawalingani na Taifa lolote jingine katika maisha yake yote nashukuru kwa Bwana vitu vya faraja,visivyokwisha lakini nina sikitiko kubwa kwa kukosa mtoto”. Jamii ya kufikirika waliamini kuwa na watoto wengi ndio ujenzi wa nguvu wa Taifa lao. (uk 3) Mfalme anaamini watoto ndio nguvu ya ufalme wake.
Mapinduzi ya kisiasa,na kiutamaduni,mapinduzi ni kufanya mabadiliko, yaani kuondoa utawala au siasa ya kwanza na kuingia siasa mpya.katikas riwaya hii mjinga alitumia utu wake kufanya mapinduzi kwa kumsaidia mototo wa mfalme kupata dawa hospitalini,na kupona,wanakijiji wa kufikirika walizoea utamaduni wa kuwaamini waganga wa jadi na sio hospitali.Pia katika siasa mjinga alijaribu kutetea haki na sheria ya utu,kwa kuzuia kafara ya watu kutalewa kwani haina umuhimu.
Kazi nyingine ya fasihi  ipatikanayo Afrika ni ushairi wa fungate ya uhuru.Fungate ya uhuru ni diwani iliyoandikwa na Mohamed S. khatibu mwaka (1988). Diwani hii inajadili mambo yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya katika nchi zetu za Afrika. Katika diwani hii tutachambua mambo hayo kwa kutumia mkondo wa jamii na siasa. Uchambuzi wetu unaanza  kama  ifuatavyo;
Kuwa na uongozi bora ,uongozi mbaya ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya.Katika diwani hii inaonyesha jinsi viongozi wanavyotumia  madaraka yao vibaya kuwanyonya wananchi wa kawaida.Nyerere anasema sera ya mipango inajadiliwa nakurekebishwa na watu wote.Pia ujamaa ni tofauti na ubepari unaolenga kumnyonya mtu,hivyo yeye anasisitiza kuishi katika umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.Diwani inaonyesha kuwa uongozi mbaya ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya(uk15-16) shairi la “Viongozi wa Afrika”,hapa mwandishi amekemea viongozi wanaotumia madaraka vibaya.Mashari mengine yanayozungumzia uongozi mbaya ni “Fungate”, “Waja wa Mungu”, “Wizi”, “Utawala”, “Njama”, “ujamaa”.
Kupinga vita ukoloni mamboleo,ukoloni mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru kisiasa lakini njia nyingine za uchumi hutawaliwa au hubaki mikononi mwa mabepari aunyingine.Kwame Nkurumah anasema ujamaa ni msingi wajamii za kiafrika kuliko ubinafsi,hivyo ubepari utaiharibu Afrika,Afrika haitakuwa huru ikiwa itaendelea kuwa chini ya ubepari wa kimagharibi.Katika shairi la “Ruya”,anonyesha kuwa wazungu ndio waliondoka katika ardhi ya Afrika lakini unyoyaji bado upo.Pia katika shairi la “kunguru”,mwandishi ameonyesha athari za ukoloni mamboleo.
Kufanya mageuzi,mageuzi huleta mafanikio katika ujenzi wa jamii mpya.Keneth Kaunda anasema waafrika walifanikiwakuushinda ukoloni kwa sababu ya utu na sio nguvu,pia nguvu katika kujikomboa si mbinu sahihi ya ukombozi bali nguvu inaweza kutumika katika kujilinda.Mwandishi naye ametoa njia mbalimbali ili kufanikisha ukombozi katika shairi la “Unganeni”,pia mwandishi anapendekeza kutumia silaha katika mageuzi ikiwa unyonyaji hautaondoka kwa njia ya amanimfano katika shairi la “Siku itafika” (uk 30) na “Nikizipata bunduki).

Umoja na Ushirikiano, hii ni mbinu mojawapo ambayo mwandishi amependekeza  kama mojawapo ya njia ya ujenzi wa jamii mpya.Nyerere asisitiza watu kuishi katika umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.Katika shairi la “unganeni” (uk 1) mwandishi anawataka waafrka wote tuungane ili kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa.

Kujenga nchi itayofuata mfumo wa ujamaa, Nyerere anasema,ujamaa wa kiafrika ni kama Afrika pana, ujamaa ambao unakuwa mwendelezo wa kifamilia na kuishi vizuri na watu na sio ujamaa wa kimax unaotetea migogoro yakitabaka,mwandishi anashauri ujamaa kuwa ni sululisho la wanyonge,shairi la “Ujamaa” shairi hili linajadili wapinzani wa ujamaa.Mwandishi ansema ujamaa umeumbuliwa,umethiliwa,umekashifiwa na umesalitiwa.

Kupiga vita wizi wa mali ya umma,sehemu nyingi zimeoza kwa wizi,ikulu na viongozi wamejiunga na wahalifu.Katika shairi la “Wizi” na “Kunguru” (uk19) ameeleza wezi waliotimuliwa na kutawanywa, shairi la “Joka la mdimu” mwandishi anatanabaisha watu kuhusu uwezekano wa wakoloni kurudi kwa umbotofauti lakini athari ni zile zile,pia katika shairi la “Naona” (uk 33) anoonyesha taabu wazozipata wakulima na malipo duni wanayopewa kwa mazao yao.

Kitabu cha tamthiliya ya “Nguzo mama” iliyoandikwa na Penina Mhando(1982).Tamthiliya hii inasawiri na kuyaelezea matatizo mbalimbali yanayowakabili na kuwaelemea wanawake wengi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.Kwa kutumia mkondo wa kisiasa na kijamii tumechambua tamthiliya hii kama ifuatavyo;

Uongozi mbaya, katika tamthiliya hii mwandishi ameonyesha umuhimu wa uongozi bora, na kiongozi bora. Nyerere anasema ujamaa ni tofauti na ubepari unaolenga kumnyonya mtu, anasisitiza kuwa kuishi katika umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni.Katika kijiji cha patata kulikuwa hakuna ujamaa. Katika jamii kiongozi anaweza kuipeleka jamii yake kwenye neema au kwenye mdomo wa simba kutegemeana na uongozi wake anavyoupeleka (uk 22), kijiji cha patata kilikuwa na uongozi mbaya wa kidikteta, mfano; Mwenyekiti, kamati ya halmashauri,wanatumia vitisho kumlazimisha Bi nane kusema asichokijua (uk24).

Uvivu na Uzembe, huwa haufai katika jamii,katika mkondo huu Nyerere anasema kila mtu alifanya kazi katika ardhi na kila mtu alikula matunda ya kazi  yake hivyo mtu akiwa mzembe atakula matunda ya uvivu na uzembe ambayo si mema.katika kijiji cha patata watu hawa walikuwa ni wavivu na wazembe,ndio maana ilipekea kufifia na kushindwa kuinua  Nguzo mama”. Wanawake hawa walikuwa hawawajibiki, mfano;(uk 34)

Mapenzi na ndoa, katika “Nguzo mama”kuna mapenzi yasiyokuwa ya kweli,yanayoyojali pesa na usaliti kati ya wanandoa.Mapenzi haya hayana utu kwani ndani ya utu kuna amani na upendo wa kweli.Usaliti huleta hali ngumu katika familia mfano;familia ya Bi tano wanalala njaa kwa kukosa chakula na mahitaji muhimu kwa kuwa Maganga baba yao anamaliza pesa zote kwa wanawake.mfano ;

“Wee Bi sita mshenzi unanichukulia mume wangu hivihivi kimachomacho”(uk 39)
Umoja na ushirikiano, hiki ni kitu muhimu sana katika jamii Nyerere anasisitiza kuwa na umoja kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni .Asili ya ujamaa ni Afrika na si ujamaa wa kimarx unaotetea matabaka.Kijiji cha patata watu wake walikosa umoja na ushirikiano ndio maana walishindwa kuinua nguzo mama kwani kila mtu anajali mambo yake Bi moja anaacha kazi anaenda kuangalia khanga (uk 34
Dhuluma, hii imeghubika jamii yetu ya leo,katika tamthiliya hii ya Nguzo mama mwandishi amejaribu kutuonyesha jinsi jamii ya Patata kama zilivyo jamii iliyooza kwa dhuluma hasa pindi wanawake wanapofiwa na waume zao,mfano Bi saba anaoonyesha jinsi gani wanawake wengi wa kiafrikawanavyodhulumiwa mali na ndugu wa mwanaume zao pindi wanapofariki.Bi saba  baada ya kufiwa tu shemeji  walikuja kugawana vitu.mfano( uk 43);
.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kumba riwaya hii ya kufikirika,tamthiliya ya nguzo mama na ushairi wa fungate ya uhuru zimeweza kuchambuliwa vizuri na tawi hili la ontolojia.Tumeweza kuona ni jinsi gani vitu halisi na vingine vya kufikirika vikitendeka katika kazi hizi,vilevile suala zima la falsafa za kijamii na siasa kama zilivyokwisha elezewa hapo mwanzo.Ujamaa unaonekana kuwa ni hali inayopelekea maendeleo katika jamii,ontolojia ya kiafrika hutumika kuchambulia kazi za fasihi za kiafrika.
MAREJEO
1.Mihanjo A,(2010)Falsafa na ufunuo wa maarifa.Toriam.Morogoro Tanzania.
2.Mohamed S.k (1988)Fungate ya uhuru.Dar-es-salaam university place(DUP).
3.Muhando p (1982) Nguzo mama. Dar-es-salaam university place(DUP).
4.Njogu na Chimera R(1999)Ufundishaji wa fasihi,Nadharia na Mbinu.Jomo Kenyatta.Nairobi
5.Tuki(2004)Kamusi ya Kiswahili sanifu.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.Dar-es-salaam.
6.Robert,S.(2008) Kufikirika.Mkuki na nyota:Dar-es-salaam Tanzania.
7.Wamitila K.W (1996) Utangulizi wa Kiswahili.Chuo kikuu cha Dar-es-salaam.Dar-es-salaam.

                      CHIMBUKO LA RIWAYA YA KISWAHILI.

Katika kujadili mada hii, mjadala huu, utajikita zaidi kutoa maana ya riwaya kutoka kwa wataalamu mbalimbali, maana ya riwaya ya Kiswahili, maana ya chimbuko, Kisha mjadala huu utaelekea zaidi katika kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili kutokana na wataalamu mbalimbali waliopata kueleza asili ya riwaya hiyo ya Kiswahili, na hicho ndio kitakachokuwa ni kiini cha swali. Mwisho tutahitimisha mjadala wetu.
Kwa kuanza na maana ya riwaya imejadiliwa kama ifuatavyo:
Wamitila (2003), anasema riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina, yenye kuchukua muda mwingi katika maandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Muhando na Balisidya (1976), wanaeleza riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake.Wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35000 hivi na kuendelea.
Nkwera (1978), anasema riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza kutosha kufanya kitabu kimoja au zaidi. Ni hadithi ya kubuniwa iliyojengwa juu ya tukio la kihistoria na kuandikwa kwa mtindo wa ushairi iendayo mfululizo kwa kinaganaga katika kuelezea maisha ya mtu au watu na hata taifa. Anaendelea kusema kuwa riwaya ina mhusika mkuu mmoja au hata wawili.
Senkoro, anasema riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake. Anaendelea kusema kuwa ni hadithi ndefu ya kubuni, yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatiwa kwa undani na upana wa maisha ya jamii.
Hivyo inaonyesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi, na mambo hayo ni; lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari, isawiri maisha ya jamii, iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu, wahusika zaidi ya mmoja, iwe na mpangilio na msuko wa matukio, lazima na maneno kuanzia elfu thelathini na tano na kuendelea, na mwisho riwaya ni lazima ifungamane na wakati yaani visa na matukio ni lazima viendane na matukio.
Baada ya kuangalia maana ya riwaya kutokana na wataalamu mbalimbali sasa ni vyema kutoa maana ya riwaya ya Kiswahili kabla ya kujadili chimbuko la riwaya.
Riwaya ya Kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili katika lugha ya kiswahili ambao hupatikanakatika nchi ya Afrika mashariki. Pia ni ile riwaya ambayo inawahusu waswahili wenyewe.
TUKI (2004) inasema chimbuko la maana yake ni mwanzo au asili.
Tanzu za asili zinaonyesha kuwa ndio zilichangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuibua riwaya za Kiswahili.Na yafuatayo ni mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya chimbuko la riwaya ya Kiswahili.
Madumulla (2009), ameeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, na ngano inayosimuliwa kwa mdomo. Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na maandiko ya fani ya ushairi hususan ni tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndiyo maanadishi yaliyotamba katika pwani ya afrika mashariki. Wazungu na waarabu hawakubadilishana maarifa kwa urahisi na hivyo pakapelekea kuwa na majilio ya taratibu za maandiko ya kinathari. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa Kiswahili toka katika lugha za ulaya na kufanya riwaya za Kiswahili kutokea. Mfano wa riwaya hizo ni kama vile; Habari za mlima iliyoandikwa na Sheikh Ali Bin Hemed (1980).
Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi. Anaendelea kusema kuwa riwaya za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za Kiswahili. Anasema riwaya mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa. Ndiyo riwaya ya kwanza kutafsiriwa kwa Kiswahili. Pia anaeleza kuwa  riwaya ni utanzu uliozuka  kutokana na hali mahususi za kijamii. Riwaya kama ile ya kiingereza ya Robinson  Crusoe iliyoandikwa na Daniel Defoe  ni miongoni mwa riwaya za mwanzo. Anasema riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni na viwanda.Suala la ukoloni  na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa mawanda mapana zaidi  ya yale ya ngano na hadithi fupi. Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya mapinduzi ya viwanda huko ulaya kilifanya waandishi waandike maandiko marefu kwani wakati huo ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi.
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo; ni fani za kijadi za fasihi pamoja na mazingira ya kijamii.
Fani za kijadi za fasihi, Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haikuzuka hivihivi tu bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi, na ndipo zikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo. Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile; riwaya za kingano, tendi, hekaya, visakale, historia, sira, masimulizi ya wasafiri, insha na tafsiri.
Ngano, Mulokozi anasema, kuwa ni hadithi fupi simulizi pia huwa ni hadithi za kubuni na nyinga hasa zinawahusu wanyama wakali, pia zinahusu malaika, binadamu, mazimwi na majini. Anasema kuwa mara nyingi ngano huwa na msuko sahihi na wahisika wake ni bapa na wahisika hao ni mchanganyiko wa wanyama, mazimwi na binadamu. Anatolea mfano wa ngano zilizo chukua visa vya kingano kuwa ni kama vile riwaya ya Adili na Nduguze ya Shaban Robart (1952), Lila na Fila ya Kiimbila (1966), Kusadikika ya Sharban Robart (1951) na baadaye yakafuata machapisho mengine kama vile; Mfalme wa Nyoka ya  R.K. Watts. Dhamira za riwaya za kingano ni kama vile choyo, mgongano wa kimawazo na tama.
Hekaya,ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabu yaani yasiyokuwa ya kawaida. Mara nyingi masaibu hayo hufungamanishwa na mapenzi. Pia hekaya ni ndefu kiasi yaani sio ndefu kiasi cha kama riwaya. Katika jamii ya waswahili hekaya zilikuwa zimeenea sana kipindi cha kabla ya ukoloni.Mifano ya hekaya ni kama vile; Hekaya za Abunuasi ya C.M.C.A. 1915, Sultan Darai (1884), Kibaraka ya (1896) na hekaya ya Jonson, F. na Brenn, E.W. Katika hekaya ya Alfa-Lela-Ulela ya kuanzia 1929. Hizo ndizo baadhi ya hekaya za mwanzo lakini baadaye ziliathili riwaya za Kiswahili kama vile; Hekaya ya Adili na Nduguze ya Sharban Robart (1952), hekaya ya Ueberu Utashindwa ya Kiimbila (1971), na Hekaya ya A.J.Amiri, ya Nahodha Fikirini, (1972).
Tendi (utendi), ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, ambao waweza kuwa ni wa kijamii au kitaifa. Kwa kawaida baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya ila tu badala ya kuwa na umbo la kinathari zenyewe zina umbo la kishairi. Kuna tendi za aina mbili ambazo ni tendi andishi na tendi simulizi. Riwaya pevu kama tendi husawiri mawanda mapana ya kijamii na kihistoria. Huwa na wahusika wababe yaani mashujaa wenye kuwakilisha pande zinazopingana. Mfano wa tendi ni kama vile; Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mlima ya Hemedi Abdallah, (1895), Utendi war as (Ghuli), utenzi wa Fumo liyongo wa Mohamed Kijumwa K. (1913).Tendi katika riwaya za Kiswahili imetumia wahusika wawili tu ambao ni wahusika wa kubuni na wale wa kijadi wa kiafrika.
Visasili, hizi ni hadithi zinazohusu asili na hatima ya watu, vitu, viumbe, ulimwengu na mataifa, na pia huangalia uhusiano wa wanadamu na mizimwi pamoja na miungu. Hadithi za kivisasili zinapoonyeswa huaminika kuwa yakweli tupu hasa kwa kusimulia matukio mengi ya kiulumwengu.
Mfano wa visasili; Lila na Fila ya Kiimbila (1966) ambayo imekopa motifu ya asili ya ziwa ikimba huko Bukoba. Hadithi ya Mungu wa Kikuyu huko Kenya. Roza Mistika ya Kezilahabi (1971), Nagona (1987) na Mzingile (1991), Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robart.
Visakale, ni hadithi ya kale kuhusu mashujaa wa taifa,kabila au dini. Mara nyingi visa kale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni, na hadithi hizi hupatikana karibu katika kila kabila kila lugha.Baadhi ya visakale vya Kiswahili masimulizi huhusu chimbuko la miji ya pwani, mijikenda, mwinyi mkuu huko Zanzibar.Visa kama hivi ndivyo vinavyopelekea kuandikwa kwa riwaya za kiswahili. Mfano wake ni riwaya ya Abdalla Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972) katika kitabu cha Habari za Wakilindi, Kisima cha na Giningi ya M.S.Abdulla (1968) na ile Hadithi ya Myombekela na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buhliwali (1980) ya A. Kitereza.
Visasuli, hizi ni hadithi zozote ambazo huelezea chimbuko au asili ya kitu chochote, na maranyingi visasuli havina uzito wowote kulinganisha na visasili.mfano wake ni; kwanini paka anapenda kukaa jikoni (mekoni), Kwa nini mbuni hana mabawa yaani hapai angani, kwa nini kima anamuogopa mamba, kwanini mbwa kuishi na binadamu, kwa nini fisi hupenda kula mifupa. Katika hadithi hizi watu huwa hawaamini sana bali wanachukulia kuwa ni utani tu.
Masimulizi ya kihistoria, haya ni masimulizi ya matendo ya, mwanadamu katika muktadha wa wakati, na ni fani muhimu sana katika jamii yeyote ile. Masimulizi halisi ya kihistoria yaweza kuwa ni ya mdomo au hata maandishi na yote huwa ni chemichemi nzuri ya riwaya. Mfano wa riwya hizo ni; Habari za pate za Fumo Omari Nabhany (1913) ambayo yalikuwa ni maandishi ya masimulizi na uchambuzi. Riwaya zingine zilizoathiriwa na matukio ya kihistoria ni; Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934), Kifo cha Ugenini ya O. Msewa (1977), Kwa Heri Iselamagazi ya B. Mapalala (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika (1992).
Sira, ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu au watu. Sira huweza kuwa wasifu yaani zinazohusu habari za maisha ya mtu zikisimuliwa na mtu mwingine au zaweza kuwa tawasifu yaani habari za maisha ya mtu zikisimuliwa nayeye mwenyewe. Sira iliathiri kuchipuka kwa riwaya hasa kwa kuonyesha masilimulizi ya maisha ya mtu toka utotoni mpaka uzeeni. Masimuliza ya riwaya hizi yalikuwa katika masimulizi na hata katika maandishi pia kwa maana kabla ya ukoloni yalikuwepo maandishi yaliyohusu maisha ya mitume na masahaba.Mifano ya hadithi hizi ni; Kurwa na Doto ya M. S.Farsy (1960),Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971),Kichwa Maji ya Kezilahabi (1974) pamoja na Dunia Uwanja wa Fujo (1975),Mzimu wa Baba wa Kale ya Nkwera (1967),na riwaya ya Maisha Yangu baada ya Miaka Hamsini ya Sharban Robart (1951).
Msimulizi ya wasafiri, hizi ni habari zinazosimulia masibu nya wasafiri katika nchi mbalimbali. Hekaya za riwaya chuku za kale zilisaidia kukuza riwaya. Mfano Alfa Lela –Ulela na hadithi ya Robinson Kruso huko 1719 ilihusu safari ya baharini ya mhusika mkuu ambaye baadaye merikebu aliyokuwemo ilizama, ndipo akalazimika kuishi peke yake katika kisiwa kidogo. Na katika riwaya za Kiswahili kuna baadhi ya riwaya za masimulizi kama vile; Mwaka katika Minyororo ya Samweli Sehoza (1921), Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932)  ya Martin Kayamba. Na  uhure wa Watumwa na Kwa Heri Eselamagazi.
Insha,  ni maandiko ya kinathari yenye kuelezea, kuchambua au kuarifu kuhusu mada Fulani.Zipo insha za zina nyingi kama vile, makala, hotuba, tasnifu, michapo, barua, sira  maelezo n.k insha nyingi ni fupi mfano kuanzia maneno kama 500 na 10000 japo zingine zaweza kuwa ni ndefu kiasi cha kuwa tasnifu za kufikia kiwango cha kuwa kitabu. Mfano wa insha ni Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robert na Kichwa Mji ya Kezilahabi.
Shajara, ni kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku. Uandishi wa shajara ulianzia huko Asia na baadaye ndio ulipopata kuibuka ulimwenguni kote.Jadi hii ya kiasia iliathiri utunzi wa riwaya hasa zile za kisira. Mfano wa shajara ni ile iliyotungwa na Lu Shun iitwayo Shajara ya Mwendawazimu (1918).
Romansia (chuku) hii ni hadithi ya mapenzi na masaibu ya ajabu.Zikua maarufu sana huko Uingereza hasa karne ya 6 na 12 na Ufaransa pia zilikuwepo na pamoja na China ambapo hadithi zilizofanana na riwaya zilitungwa.mfano hadithi za Hsiao-shuo .Watunzi wa riwaya za kisasa zimekuwa na mafanikio makubwa sana kutokana na riwaya hizo za chuku hii ni kwa sababu watunzi wengi wlikuwa wamesoma kazi nyingi za riwaya za wakati ule.
Drama, maigizo mengi hasa ya tamthiliya yaliathiri sana riwaya hasa kwa upande wa usukaji wa matukio na uchanganyaji wa ubunifu na uhalisia. Mfano ni riwaya nyingi za Charles Dickens zina msuko uliosanifiwa kwa uangalifu kama msuko wa tamthiliya.
Baada ya kujadili fani za kijamii hatuna budi sasa ya kujadili mazingira ya kijamii kama yalivyopatwa kuelezwa na Mulokozi. Anaeleza kuwa, kufikia karne ya 16 fani za kijamii zilikuwa zimekwisha enea na kufahamika katika maeneo mengi, hivyo kulihitajika kuwe na msukumo wa kijamii, kiteknolojia na kiuchuni. Msukumo huo wa kundeleza fani za kijadi ulikuwa ni wa aina tatu ambao ni;
Ukuaji mkubwa wa shughuri za kiuchumi huko ulaya, ukuaji huo ulifungamana na biashara ya baharini ya mashariki ya mbali na kuvumbuliwa kwa mabara mawili ya amerika na ukuaji wa viwanda hasa vya nguo huko ulaya. Mabadiliko haya yalizua tabaka jipya la mabwanyenye waliomiliki viwanda na nyenzo nyingine za kichumi.Tabaka hilo lilihitaji fani mpya za fasihi, lilikuwa na wakati wa ziada wa kujisomea, uwezo wa kifedha wa kujinunulia vitabu na magazeti. Hivyo tangu mwanzo ilitawaliwa na ubinafsi uliojidhihirisha kiitikadi. Kwa mfano Robinson Kruso ni riwaya ilyosawili ulimbikizaji wa mwanzo wa kibepari. Ilimhusidhs muhusika asiye staarabika aitwaye Fraiday au Juma. Ubinafsi huu ulijitokeza pia katika utungaji wake, na haikusomwa hadharani bali kila mtu alijisomea mwenyewe chumbani mwake.
Mageuzi ya kijamii na kisiasa, mabadiliko haya yalifungamana na mabadiliko ya kiuchumi. Mataifa ya ulaya yalianza kujipambanua kiutamaduni na kisiasa yaliyojitenga na dola takatifu ya kirumi. Mabadiliko hayo yalianza kujenga utamaduni wa kitaifa na mifumo ya elimu iliyo hiyaji maandishi katika lugha zao wenyewe. Mfano wa mageuzi ya kijamii na kisiasa iliyofanyika ni kama vile; Misahafu ya Dini Kama Biblia ilanza kutafsiriwa kwa lugha za ulaya, Martin Lther alichapisha  Biblia kwa lugha za kidachi miaka ya 1534. Hivyo basi inaonyesha kuwa kadiri elimu ilivyopanuka na nduvyo wasomaji wa vitabu walivyoongezeka na kufanya kuwe hadhira kubwa nzuri ya wasomaji na watunzi wa riwaya.
Ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa vitabu, yaani kwa kutumia herufi iliyoshikamanishika.Ugunduzi huu uliofanywa na Johnnes Gutenberg huko ujerumani mwaka 1450 uliorahisisha kazi ya uchapaji vitabu katika nakala nyingi nakuondoa kabisa haja ya kunakili miswada kwa mikono. Bila ugunduzi huo kufanyika haingewezekana kuchapisha riwaya nyingi na kuzieneza kwa bei nafuu.Nmifano ya riwaya hizo ni kama vile; Pamela ya Samwel Richardson (1740).
Kutokana na wataalamu mbalimbali kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili, inaonekana kuwa, riwaya ni utanzu wa fasihi ambao kuzuka kwake kulifungamana na fani za kijadi pamoja na mazingira ya kijamii. Fani za kijamii kama vile, ngano, visasili, visasuli, visakale, insha, na nyinginezo zizosimuliwa bila ya kuandikwa kabla ya karne ya 16, zilichochewa na kupewa mwendelezo baada ya kukua kwa sayansi na teknolojia huko ulaya,hasa baada ya ugunduzi wa mitambo ya kupiga chapa kazi za fasihi.
MAREJEO
Madumulla, J.S. (2009), Riwaya ya Kiswahili, Historian a Misingi ya Uchambuzi. Nairobi:                                           Sitima Printer and stations L.td.
Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. TUKI.
Mhando, P. na Balisidya, (1976), Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania                                                                  Publishing House.
Nkwera, F.V. (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Tanzani Publishing                                            House.
TUKI,(2004),Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Nairobi.Kenya:Oxford University Press.
Senkoro,F.E.M.K.(2011), Fasihi Andishi.Dar es Salaam.Kauttu L.t.d.
Wamitila,K.W.(2003),Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication. 

DHANA  NA DHIMA  YA USHAIRI WA KISWAHILI

Katika makala hii tutaeleza historia fupi ya ushairi na mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya ushairi.
Tukianza na Mulokozi (1996) anasema, wataalamu wengi wamekubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi, hasa ngoma na nyimbo zinazofungamana na ngoma.
Kabla ya karne ya 10 BK ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa  kwa ghibu bila kuandikwa.  Wataalamu hao waliojadili historia ya ushairi ni kama (Chiraghdin 1971: 7:10, Massir 1977:1  Ohly 1985:467).
Dhana ya ushairi imejadiliwa kwa kuangalia makundi mawili ya waandishi wa mashairi ya Kiswahili, makundi hayo ni kundi la wanamapokeo, na kundi la wanausasa.
Tukianza na kundi la wanamapokeo.  Wataalamu mbalimbali wamejadili dhana ya ushairi kama ifuatavyo:
Kwa mujibu wa Shaaban Robert (1968) anasema kuwa Ushairi ni Sanaa ya vina  inavyopambanuliwa,  kama nyimbo, mashairi na tenzi  zaidi ya kuwa sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache  au muhtasari, uliza  swali wimbo, shairi na tenzi ni nini?  Wimbo ni shairi dogo na shairi ni wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi pia anauliza kina na ufasaha huweza kuwa nini?  Anasema  kina ni mlingano wa sauti za herufi, na kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti, na ufasaha ni uzuri wa lugha, mawazo, maono na fikra za ndani  zinapoelezwa kwa muhtasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu.  Hivyo  katika ufafanuzi wake wa ushairi inaonesha dhahiri kuwa Shaaban Robert anagusia vipengele viwili maalumu yaani fani ya ushairi na maudhui ya ushairi.
Naye Mnyampala (1970) kama alivyonukuliwa na Massamba D.P.B. katika  Makala ya Semina ya Kimataifa  ya waandishi wa Kiswahili (2003) anasema ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale.  Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongezi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalumu kwa shairi.
Hapo tunaona dhahiri kuwa Mnyampala anauona ushairi ukiwa umejengwa na vitu viwili mahususi, ambavyo ni maneno ya hekima na sanaa yenyewe.  Tena Mnyampala katika dibaji hiyo hiyo anasisitiza juu ya sanaa ya ushairi kwa kusema:
(i)                   Shairi liwe na “poetical Swahili”  yaani Kiswahili kinachohusu mwendo wa mashairi bora.                                                                                                       
(ii)                 Shairi liwe na urari wa mizani kamili zinazohusika na ushairi wa kawaida waka lugha ya Kiswahili kisichokuwa na kashfa au matusi  ndani yake.
(iii)                Shairi liwe  na vina vinavyopatana hususani mwishoni mwa kila ubeti kwa shairi lolote zima ingawa vina vya katikati vikosane kwa utenzi wake.
(iv)               Shairi lazima liwe na muwala
(v)                 Lisizidi mno maneno ya kurudia rudia.
Kwa mujibu wa Abdilatifu Abdalla (1973) katika makala ya semina  ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili anasema maana ya ushari ni utungo ufaao kupewa jina  la ushairi ni utungo wowote tu bali ni utungo ambao katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada  ya chenziye,  wenye vipande vilivyoona ulinganifu wa mizani zisizo pungufu wala kuzidi na vipande hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalumu  na yenye lugha nyofu, tamu na laini, lugha ambayo ni telezi kwa ulimi wa kutamka, lugha ambayo ina uzito wa kifikra, tamu kwa mdomo wa kuisema, tambuzi kwa masikio ya kuisikia, na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa na kama ilivyokusudiwa.
Kutokana na hayo yaliyokwishasemwa, tunaona kuwa dhana ya ushairi ya wana jadi imefinywa kwenye umbo maalumu lenye utaratibu wa vina na urari wa mizani ambayo kwa kweli ni dhana ya kimaandishi.
Kundi la pili ambalo limefafanua dhana ya ushairi   ni kundi la wanausasa.  Hawa wamejadili dhana ya ushairi kama ifuatavyo:
Kwa mujibu wa Wamitila (2010) anasema ushairi ni sanaa inayotambulishwa na mpangilio maalumu wa sentensi au vifungu, mpangilio ambao una mdundo maalumu  au ruwaza fulani inayounda wizani, lugha ya mkato na mafumbo pamoja na mpangilio usio wa kawaida wa vifungu fulani.
Mulokozi, (1989) anasema ushairi ni sanaa ya lugha inayoonesha au kueleza jambo, wazo  au tukio kwa namna inayovuta hisia kutokana na mpangilio  maalum wa maneno yaliyoteuliwa, kauli za mkato, picha na tamathali  na inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya nyimbo au maandishi.  Kwa mujibu wa ufafanuzi huo ushairi hueleza tu, bali hudhihirisha, au huonyesha kusawiri,  anaendelea kusema ushairi huwajumuisha watu wawili au zaidi.  Kihisia katika tukio linalowagusa wote,  ukawatosa katika dimbwi la uchungu, au furaha, hasira au ridhaa, na kuwatoa tena wakiwa wameburudika na kuelimika.
Kwa sababu hii ushairi  ndiyo sanaa ya fasihi inayokaribiana  zaidi na muziki na  mara nyingi sanaa hizi mbili hufungamana.
Mulokozi na Kahigi (1979) wanamnukuu Kezilahabi kwa kusema kuwa ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno  fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha  jambo ambalo halikutiliwa maanani katika fafanuzi la wataalamu hawa ni dhima ya fasihi na ushairi kama vyombo vya kuburudisha na kustarehesha watu.
Wataalamu hawa wanaendelea kusema kuwa ushairi lazima uguse hisi, lazima umsisimue yule anayeusema, kusoma au kuimba na  yule ausikilizaye.  Hivyo shairi lisilogusa hisi ni  kavu na butu hata  kama limetafsiriwa katika vina na urari wa midhani, shairi hilo litaishia kuhubiri tu.
Kwa ujumla wanausasa wanadai kuwa ushairi  ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha  na yenye muwala, kwa  lugha   ya mkato, picha au stiari  au ishara.  Katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbi ili kueleza wazo au mawazo, kujifunza au kueleza tukio au hisi fulani.  Kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.
Kutokana na mawazo hayo ya washairi mbalimbali wa kimapokeo na wana usasa wote wameonesha  mambo fulani ambayo yamefanana kwa  namna moja ua nyingine.
Wote wanakubaliana kwamba katika ushairi fani na maudhui ni vitu vya muhimu kabisa na kwamba kila kimoja  kati ya vitu hivyo kina wajibu maalumu.
Pia washairi wengi huamini kwamba lugha ya ushairi lazima iwe ya mkato, yaani iweze kusema mambo mengi kwa kutumia maneno  machache.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa ushairi ni  sanaa ya lugha yenye ughunaji na yosawiri, kueneza au kuonesha jambo lenye  hisi au hali fulani kwa namna  ya kuvutia hisia katika mpangilio  mahususi wenye urari wa vizani na sauti.
Baada ya kuangalia  wataalamu mbalimbali walioelezea dhana ya ushairi, zifuatazo ni dhima za ushairi wa Kiswahili.
Ushairi husaidia kurithisha  maarifa kwa jamii, kupitia ushairi jamii inaweza kujifunza mambo mbalimbali kama vile namna ya kuepukana na magonjwa, umuhimu wa kutunza mazingira.                                                                                                           
Mfano:  shairi la Binti katika diwani ya dhifa iliyoandikwa na Kezilahabi e, Mwandishi anarithisha jamii maarifa kwa kusisitiza jamii izingatie umuhimu wa elimu: anasema
                        Soma soma kwa kujiamini.
                        Elimu ni kikata kiu,
                        Huondoa pia ukungu,
                        Pasipo njia pakawa
                        Fanya kazi utayopata,
                        Kazi ni kinga ya  heba
                        Sasa umekuwa na uwe,
                        Huu usinga na kupa
                        Na unyoya nakuchomekea nyweleni.
Ushairi husaidia kuhamasisha jamii, ushairi hutumiwa kama njia ya kuwahamasisha wanajamii katika shughuli mbalimbali. Mfano: katika utendi wa Fumo Loyongo ubeti wa kumi na tatu, anahamasisha wanajamii kuwa na nguvu kama simba, anasema:
                        “Ni mwanaume Swahili
                        Kama simba unazihi
                        Usiku na asubuhi
                        Kutembea ni mamoya.
Pia katika diwani ya Wasakatonge, shairi la Wanawake wa Afrika, mwandishi anawahamasisha wanawake kujikomboa, anasema:
                        Wanawake wa Afrika
                        Wakati wenu umefika,
                        Ungeneni
                        Shikaneni
                        Mjitoe utumwani,
                        Nguvu moja!                                                                                                                 
Ushairi husaidia kudumisha na kuendeleza utamaduni katika jamii, kupitia ushairi wanajamii wanadumisha na kuendeleza utamaduni wao na  kwa njia hii  huhakikisha kuwa unabaki hai. Mfano katika  tohara huwa kunakuwa na nyimbo zenye mafunzo kwa vijana wanaofanyiwa jando na unyago, kama vile kuandaa wanaohusika kwa majukumu ya utu uzima.
Ushairi huburudisha  hadhira, ushairi ni nyenzo kuu ya burudani, katika jamii licha ya majukumu mengine ya nyimbo, msingi mkuu ni uwezo wake wa kuweza  kuathiri hisia za wasikilizaji au washiriki wake na kuwaburudisha.  Mfano katika shairi la watoto wawili kutoka kwa mwandishi Kezilahabi Kichomi (1974 uk. 62):
            Mtoto wa tajiri akilia  hupewa mkate,
            Mtoto wa tajiri akilia hupewa picha ya kuchezea,
            Akilia mtoto wa tajiri huletewa kigari akapanda,
            Akiendelea kulia hupanda mgongo wa yaya,
            Akikataa kunyamaza ulimwengu mzima hulaumiwa.
Ushairi husaidia kukuza lugha kwa kawaida ushairi hutungwa kwa lugha nzito yenye ishara  na jazada zinazoeleweka na wanajamii wanaohusika, na kwa njia hii  hutusaidia kukuza hisia za kujitambua kwao kama watu wa kundi fulani lenye mtazamo, imani na mwelekeo fulani.
Hivyo kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba aidha ushairi uwe wa kimapokeo au  wa kisasa unaonesha mambo muhimu yanayoilenga jamii husika.  Mfano katika mambo ya kidini, kisiana na kiutamaduni.                                                                                                                        
MAREJEO
Abdilatifu, a (1973), Sauti ya Dhiki, Oxford London.
Kezilahabi, E (1974), Kichomi, Heinemann; London.
Massamba, D.P.B. (2003), Utunzi wa Ushairi wa Kiswahili katika makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili (III).  Fasihi.  Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M na Kahigi K.K. (1979), Kunga za Ushairi na Diwani Yetu, TPH, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1989) Uchambuzi wa Mashairi:  Mulika Namba 21; TUKI, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1996), Fasihi ya Kiswahili, chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dar es Salaam.
Robert, S (1968) Kielelezo cha Insha.  Nelson London.
TUKI, (2003), Makala za Semina ya  Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III : Utunzi wa Ushairi wa Kiswahili, TUKI Dar es Salaam.
Wamitila, K.W.  (2010) Kichoche cha Fasihi Simulizi na Andishi, English Press.  Nairob
Powered by Blogger.