KWA KIASI KIKUBWA FASIHI HUTAWALIWA NA FANTASIA
ILI KUNOGESHA
USOMAJI. MAELEZO KWA KUTUMIA KITABU CHA MARIMBA YA MAJALIWA
Fasihi inafafanuliwa na Wamitila (2003)
kwa kueleza kuwa ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kwa usanii na inayowasilisha
suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusana kuacha athari fulani na
kuonyesha ubunilizi na ubunifu fulani na zinazomhusu binadamu. Kazi hizi za
fasihi huweza kuwasilishwa kwa njia ya mdomo yaani fasihi simulizi au kwa njia
ya maandishi yaani fasihi andishi. Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa fasihi ni
tawi la kisanaa litumialo lugha kama nyenzo kuu ili kufikisha ujumbe katika
jamii lengwa.
Pia Wamitila (2003) anaeleza kuwa
fasihi ya watoto kuwa hutumiwa kuelezea fasihi maalumu inayoandikwa kwa ajili
ya watoto.Hii ni fasihi ambayo ni tofauti na ngano na hurafa.Mifano ya kazi za
watoto ni kama vile Ngome ya Mianzi
ya M.Mulokozi, Yatima na Zimwi la leo ya Wamitila na Mwendo ya Lema.
Wamitila (kaishatajwa) anaeleza kuwa
fantasia ni sawa na njozi, njozi ni dhana inayotumiwa kuelezea kazi ya fasihi
ambayo ina sifa ambazo zinakiuka uhalisi.Anaendelea kufafanua kuwa ni kazi
yenye sifa za kindotondoto au kutaka kuamilisha hali isiyo ya kawaida. Njozi
hupatikana sana katika maandishi yanayolenga hadhira ya watoto.Sifa za kinjozi
huweza kupatikana katika fasihi inayohusishwa na matapo mbalimbali ya
kifasihi.Hutumiwa kueleza kazi za kinathari ambazo huwa na mandhari ya ajabu, matukio
magumu kukubalika katika hali ya kawaida na hata wahusika wasioweza kupatikana
katika uhalisi. Kutokana na fasili hiyo ya Wamitila tunaweza kusema kuwa
wahusika katika kazi zenye fantasia ni wahusika kama vile mazimwi, mashetani
,majini na vitu vingine ambavyo havidhaniwi kuwepo katika jamii, yaani haviwezi
kupatikana katika uhalisia .
Ifuatayo ni historia fupi ya kitabu
cha Marimba ya Majaliwa.
Marimba ya Majaliwa
ni kitabu kilichoandikwa na Edwin
Semzaba (2008), kinachoelezea harakati za kutafuta marimba ya Majaliwa
yenye nyuzi ishirini, iliyoporwa na Ngongoti aliyekuwa bingwa wa kupiga
marimba.Kitabu hiki kinahusisha msako wa marimba hiyo katika mikoa mbalimbali
ya Tanzania, na hatimaye Majaliwa alifanikiwa kupata marimba yake na
kushiririki katika mashindano ya kumtafuta bingwa wa kupiga marimba huko Dodoma
ambapo Majaliwa aliibuka mshindi wa shindano hilo.
Ufuatao ni uchambuzi wa baadhi ya fantasia zilizojitokeza katikakazi
ya fasihi kama katia kitabu cha Marimba ya Majaliwa. Katika uchambuzi wa
fantasia, tumejaribu kuziweka fantasia katika makundi tofauti tofauti.Makundi
hayo ni kama vile fantasia zinazohusu usafiri, fantasia zinazohusu utokeaji
tofauti tofauti wa bibi pamoja na umbo lake,fantasia zinazohusu jiwe la rubi,
fantasia zinazohusu utokeaji wa babu na nyinginezo.Kwa kuanza na fantasia
zinazohusu usafiri:-
Mwandishi Semzaba ameonyesha njia
mbalimbali alizokuwa akizitumia Majaliwa na bibi kusafiri kutoka sehemu moja
hadi nyingine ambazo hazikuwa za kawaida katika maisha halisi ya binadamu.Njia
hizo za ajabu alizokuwa akizitumia ni pamoja na :-
Kutumia
ufagio, mfano (uk.27) alitumia ufagio kueleka uwanja wa
kimataifa wa mifagio, (uk.103) alitumia ufagio kwenda mapango ya Amboni,(uk.
208) alitua uwanja wa Kigamboni kwa ufagio.
Kutumia
ungo, Bibi pamoja na Wajaliwa walitumia ungo kwenda
sehemu tofautitofauti kama inavyodhihirika katika (uk.77) kutoka Tanga kuelekea
Kilimanjaro.
Kutumia
njia ya kufumba na kufumbua.Katika njia hii, bibi alikuwa
akiwambia Majaliwa afumbe macho akifumbua wanakuwa wamefika sehemu au eneo
lingine.Aina hii ya usafiri inadhihirika katika (uk 77,107,107 na 209). Mfano
(uk 107) bibi alimwambia majaliwa afumbe macho baada ya Majaliwa kufumbua macho
akajikuta yumo ndani ya pango la Amboni.
Pia
msanii ameonyesha jinsi bibi Majaliwa alivyokuwa akipaa hewani kutoka sehemu
moja kwenda nyingine. Mfano uk.
(182)…. alimwacha sehemu ya Mwandege halafu akapaa.Hivyo usafiri aliokuwa
akitumia bibi na Majaliwa kwa hali ya kawaida katika jamii ni mambo ya kinjozi
yaani hayapo katika maisha ya kiuhalisia na wala hayatarajiwi kuwepo.
Kundi lingine la fantasia ni namna
ya utokeaji na uondokaji wa bibi pamoja na umbo lake
Msanii ameonesha hali isiyokuwa ya
kawaida katika maisha ya binadamu kwa kumtumia mhusika ambaye ni bibi yake
Majaliwa na kufanikiwa kuonyesha hali hiyo ya kinjozi.
Utokeaji wa bibi pamoja na umbo lake
unadhihirika kama ifuatavyo:-
Katika uk. (5-7) tunaona bibi
anajitokeza katika umbo la samaki na
kumbeba Majaliwa na kuondoka naye hadi Unguja kusini.Bibi yake Majaliwa alijitokeza
kama papa na kubadilika na kuwa nguva .Hili si jambo la kawaida kwa binadamu
kubadilika badilika bali ni mambo ya kinjozi tu.
Katika uk. (143) mwandishi ameonesha jinsi bibi alivyogeuka na kuwa tai mkubwa na kuruka,
hali hii pia sio hali ya kawaida kwa binadamu bali ni dhana ya ufantasia
aliyoitumia msaniii ili kukamilisha lengo lake.
Pia mwandishi amefanikiwa kuonesha
matukio mbalimbali ya kifantasia aliyokuwa akifanya bibi yake Majaliwa na
Majaliwa. Mfano nyoka kutoka mdomoni kwa
mtu uk. (58) msanii anasema, “Bibi alipanua mdomo na kutoa nyoka ambao
waliwameza wale vibwanga wote”.
Kumvisha
Majaliwa nguo uk. (58) bibi alichukua kijani
akakichomeka kichwani kwa Majaliwa na Majaliwa akajiona amevaa koti,suruali na
viatu vya baridi.
Kuna
ufantasia unaojitokeza katika hadithi ambazo bibi alikuwa akimsimulia Majaliwa
mfano uk. (169) Bibi anamsimulia Majaliwa hadithi ya mvuvi
aliyevua chupa, na ndani ya chupa akatoka ndege mkubwa na kuanza kuongea.
Pia
michezo ya wanyama wakali, imeoneshwa na msanii katika
uk.(78 na 79) ambapo ameonesha jinsi Majaliwa na bibi yake walivyokuwa
wakicheza na wanyama wakali kama vile simba na tembo huko mbugani Arusha .Dhana
hii ni ya kifantasia kwani haiwezekani kabisa katika hali halisi kwa wanyama
wakali kucheza na binadamu.
Kwa upande mwingine msanii ameonesha
dhana ya ufantasia pale ambapo walikuwa wakiingia katika sehemu tofauti tofauti
kama vile hotelini mfano waliingia hoteli ya ngurudoto huko Arusha uk.(80), na
hoteli ya Seventy seven uk.(88)
Hivyo mwandishi ametuonesha hali
zisizokuwa za kawaida katika maisha halisi ya binadamu kama vile kubadilika badilika kutoka binadamu na kuwa
samaki,bibi kuja kwa umbo la mama yake Majaliwa, bibi kuja kwa umbo la binti mdogo na vitu vinginevyo kama ndege sio
jambo la kawaida katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Kundi lingine la fantasia
lililooneshwa na msanii katika kitabu hiki ni uwepo wa jiwe la rubi, hili
ni jiwe ambalo Majaliwa alipewa na bibi yake kwa masharti. Jiwe hili
lilimsaidia Majaliwa kula chakula katika
sehemu mbalimbali alizokuwa akisafiri
akitafuta marimba yake ingawa jiwe hili lilikuwa na masharti.Masharti aliyopewa
Majaliwa ni kutokula kitu kwa kupitia mdomo.Mwandishi ameonesha jinsi Majaliwa
alivyotumia jiwe hilo, hata alipokiuka masharti bibi yake alimpa tena jiwe kama
lile.Uwepo wa jiwe hili unadhihirika katika kurasa kama vile
(21,102,110,143).Majaliwa alitumia jiwe hili kwa kula pale tu alipotamka maneno
kadhaa na akujikuta tayari ameshiba bila kutumia mdomo na kinywa.
Kundi linguine la mambo ya ajabu
ajabu ni nmna ya utokeaji wa babu.Mwandishi ameonesha kuwa mpinzani wa
Majalia, Ngongoti alikuwa akipata nguvu za kusafiri kwenda mbali pamoja na
kumtoroka Majaliwa kwa kutumia nguvu za kimiujiza alizokuwa akisaidiwa na
babu.Nguvu za babu zilikuwa kipingamizi kilichomfanya Majaliwa kushindwa
kufanikisha haraka zoezi la kupata Marimba yake.Msanii ameonesha jinsi babu
alivyokuwa akijitokeza na kutuma vikwazo kama vile:-
Vibwengo
uk.(53).
Mwandishi anaeleza, Majaliwa aliona kundi kubwa la vibwengo likwaajia kutoka
kushoto, kulia na mbele yao.Pia uk. (27,58 ,93 na194) unaonesha jinsi babu
alivyotuma vibwengo kumkabili bibi na Majaliwa.
Pia babu alimtokea Majaliwa katika umbo la Mamba akiwa na nia ya
kumuangamiza lakini bibi alimsaidia, haya yanajitokeza katika uk.wa (49). Zote
hivi ni fantasia kwani si hali ya kawaida kwa vitu kama hivi kujitokeza kwa
umbo la binadamu na binadamu kujibadilisha na kujitokeza katika hali
tofautitofauti katika maisha halisi ya binadamu.
Fantasia nyingine alizozionesha msanii
ni kama vile, Majaliwa alipofika Ukerewe
aliona mawe mawili makubwa juu ya
mlima ambapo jiwe moja la juu lilikuwa linazungukazunguka. uk.(146).Hali
hii katika mazingira ya kawaida si halisi na wala hatutegemei kuona jiwe
likizunguka lenyewe bila mtu kuligusa.
Baada ya kupitia baadhi ya fantasia
katika kitabu ch Marimba ya Majaliwa , ufuatao
ni mchango wa fantasia katika kazi hiyo;
Kujenga
dhamira : Msanii ametumia dhana ya fantasia kama vile
uwepo wa jiwe la rubi kujenga dhamira tofauti tofauti kama vile kuwafanya
watoto wawe na adabu na utii, kuwafanya watoto wafikiri zaidi mazingira ya
uwezekano katika jamii . Vilevle fantasia za utokeaji wa babu huwafanya watoto wawe na woga juu ya mambo
mbalimbali na wawe na mawazo juu ya tamaduni mbalimbali za watu wa kale.
Kujega
taharuki: hapa fantasia hujenga shauku kwa watoto au
msomaji kutaka kujua nini kitaendelea baada ya kukutana na kikwazo fulani.Mfano
fantasia ya kuingia hoteli ya Ngurudoto na hoteli ya Seventy seven kimiujiza
inajenga taharuki ya kutaka kujua kwamba, je baada ya kupambazuka Majaliwa
atashikwa au la.Pia hali ya utokeaji wa babu kama mamba pale mtoni alipokuwa
akinawa majaliwa,msomaji hupata taharuki ya kutaka kujua kama Majaliwa atamezwa
na yule mamba au la.Fantasia ya kupaa kwa ungo na kutua juu ya mlima
Kilimanjaro, msomaji hupata taharuki ya kutaka kujua kuwa Majaliwa atasalimika
kwenye barafu au la.
Pia kutua na kucheza na wanyama wakali
mbugani, huzua shauku kwa msomaji ya kutaka kujua wataliwa na wanyama hao au la
na watasalimikaje na wanyama hao.
Fantasia humjengea mtoto au msomaji
taswira tofauti tofauti juu ya mambo yasiyokuwa ya kawaida. Mfano fantasia ya
utokeaji wa bibi katika sura tofautitofauti,utokeaji wa babu,uwepo wa jiwe
la rubi na usafiri uliotumika hujenga taswira ya mambo kama hayo kutokea katika
jamii. .Mtoto hujenga taswira juu ya uwepo wa vitu kama hivyo katika maisha ya
kila siku ya jamii.
Fantasia
huamilisha uwepo wa mambo fulani fulani katika jamii ili kutaka kuthibitisha
mambo hayo.
Mfano fantasia za utokeaji wa bibi na babu na upinzani kati yao, hutaka
kuamilisha kuwa suala la ugomvi kati ya watu waliokufa yanaweza kuwapata watoto
au watu wao wa karibu waliobaki duniani kwa namna tofauti tofauti za ajabu.
Hivyo tunaweza kupata funzo kuwa ugomvi si kitu chema katika jamii.
Fantasia
huibua migogoro : msanii ametumia dhana hii ya
fantasia katika kitabu hiki ili kuibua na kukuza migogoro.Hali hii ya kukuza
migogoro au kisa ni namna ambayo mtunzi hutumia ili kukifanya kisa chake kiwe
na mawanda mapana.Mfano fantasia za upinzani wa babu dhidi ya bibi kwa maumbo
tofauti kama vile umbo la vibwengo na umbo la mamba, hali hii imekuza kisa cha
msanii na kuwa na mawanda mapana kwani humlazimu msanii kubuni zaidi namna ya
kumuepusha muhusika wake asiangamie.Pia fantasia ya usafiri kama vile kutumia
ungo,ufagio na nyinginezo, msanii amezitumia ili kujenga na kukuza migogoro
katika kazi yake ili uwe na mawanda mapana zaidi.
Fantasia
hufanikisha msuko wa vitushi,mfano msanii ameweza kuhusianisha fantasia kama vile usafiri wa
kutumia njia mbalimbali na hadithi mbalimbali alizokuwa akimsimulia Majaliwa na
inaonesha wazi kuwa kutokana na kutumia fantasia kumemsaidia kukamilisha msuko
wa vitushi kama vile alivyomsimulia majaliwa hadithi tofati wakiwa safarini.
Mfano wakiwa juu ya mlima Kilimanjaro.
Pia fantasia huburudisha, husisimua na kutia watoto hamasa.Mwandishi
amefanikiwa kuonesha fantasia tofauti tofauti za kusisimua na kutia hamasa kama
vile bibi alivyokuwa akimtokea Majaliwa, bibi na Majaliwa kucheza na wanyama na
nyinginezo. Hali hii huburudisha na kumsisimua mtu aisomapo.Pia wasomaji
huburudika kutokana na matukio ya ajabu ajabu yaliyojitikeza na namna yanavyoendelezwa na msanii.
Hivyo tunaweza kuhitimisha kuwa
mwandishi wa kitabu cha Marimba ya Majaliwa, amefanikiwa kuonesha jinsi
fantasia zinavyojitokeza katika fasihi.Msanii ameonesha fantasia hizo
zilivyotumika katika usakaji au utafutaji wa Marimba katika sehemu mbalimbali
nchini Tanzania.Utokeaji wa fantasia katika kazi ya fasihi huwa ni ubunifu wa
mtunzi kwa lengo la kuifanya hadhira anayoiandikia, mathalani ya watoto ihamaki na kufikiri zaidi sababu za
uwezekano wa mambo kama hayo katika jamii.
MAREJEO
Semzaba, E. (2008), Marimba ya Majaliwa.
E&D Publishers Limited:Dar es Salaam
Wamitila, K. W. (2003) Kamusi ya
Fasihi: Istilahi na Nadharia,Nairobi :English Press
MAANA
YA RIWAYA NA AINA ZA RIWAYA
Katika
kuandika makala hii hili, sehemu ya kwanza tutaangalia maana ya riwaya kwa
mujibu wa wataalamu, historia ya riwaya kwa ufupi na sifa za zake. Sehemu ya
pili tutaangalia kiini cha swali yaani aina za riwaya kwa mujibu wa wataalamu
wa fasihi. Sehemu ya tatu tutaangalia hitimisho na kumalizia na marejeo.
Riwaya
imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwao ni kama vile,
Encyclopedia Americana (EA), Jz. 20 (1982:510f)
wakinukuliwa na Mulokozi (1996) wanasema, riwaya kuwa ni hadithi ya kubuni
inayotosha kuwa kitabu. Maelezo haya yanaibua utata kwani hayafafanui kitabu
kinapaswa kuwa na urefu kiasi gani. Matharani kwa mujibu wa UNESCO katika
Mulokozi (1996) kitabu ni chapisho lolote lenye kurasa 48 au zaidi. Ama urefu
wa kitabu hautegemei idadi ya kurasa tu pia unategemea ukubwa wa kurasa (upana
na kina) ukubwa wa maandishi na mpangilio wake.
Encyclopedia
Britanica EB, Jz.8, (1985:810) wakinukuliwa na Mulokozi (1996) wanaeleza kuwa,
riwaya ni masimulizi marefu ya kinathari yaliyochangamana kiasi, yenye
kuzungumzia tajriba ya maisha ya binadamu kwa ubunifu. Udhaifu wa hoja hii ni
kwamba wamejikita katika kigezo cha urefu, lakini hatujui urefu huo ni wapaswa
kuwa kiasi gani. Lakini Mphahelele (1976:45) akinukuliwa na Mulokozi (1996) anaeleza kuwa riwaya fupi
huwa na maneno kati ya (35,000 hadi 50,000) na riwaya ndefu huwa na maneno kati
ya (50,000 hadi 75,000).
Pamoja
namaelezo hayo ya Mphahelele (1976) imeonekana bado kuna utata katika kigezo
cha urefu. Hivyo Wamitila (2002) Senkoro
(2011) na hawakubaliani na kigezo cha
kufasili riwaya kwa kutumia kigezo cha urefu. Mfano Senkoro anaeleza kuwa ,
“Ikiwa tutakichukua kipimo cha jumla ya
maneno (75,000)
kuwa kielelezo cha riwaya basi
itaonekana kuwa tuna
riwaya chache
mno katika fasihi kwa hali hii
nadhani sifa
ya mchangamano ni nzuri zaidi kuelezea
maana ya riwaya” (uk. 56)
Naye
Wamitila anendelea kuelezea kuhusiana na suala urefu kuwa,
“Kigezo hiki cha urefu hakifai
tunapoziangalia kazi
za
fasihi ya Kiswahili...Mfano kazi mbili za E. Kezilahabi,
“Nagona
naMizingile” hazina idadi kubwa ya maneno lakini
ni
riwaya”.
Hivyo,
Wamitila (2002) na Senkoro (2011) wanaelekeana kufanana katika kufasili maana
ya riwaya ambapo wanaeleza kuwa, riwaya ni kisa mchangamano ambacho huweza
kuchambuliwa kupimwa kwa mapana na marefu kifani na kimaudhui. Riwaya ni kisa
au mkusanyiko wa visa, nyenye urefu unaoviruhusu vitambe na kutambaa mahali
pengi na kuambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake.
Riwaya basi ni hadithi ndefu ya kubuni, yenye visa vingi, wahusika zaidi ya
mmoja, na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana,
maisha ya jamii. Riwaya hutoa picha ya jumla ya maisha ya mtu toka nyumbani
hadi katika kiwango cha taifa na dunia nzima. Senkoro (2011).
Hivyo
kutokana na fasili za wataalamu hawa tunaweza kufasili riwaya kuwa ni
masimulizi ya kubuni ya kinathari yenye msuko au mpangilio fulani wa matukio au
ploti inayofungamana na wakati au kusawili wakati na yenye visa vingi
vivavyotendeka katika wakati fulani na yenye mawanda mapana yenye mchangamano
wa dhamira, visa na wahusika.
Baada
ya kutoa fasili mbalimbali za wataalamu wa fasihi kuhusu maana ya riwaya, sasa
tuangalie kwa ufupi chimbuko la riwaya;
Riwaya
ilizuka kutokana na maendeleo ya mageuzi ya kiutamaduni. Suala la ukoloni na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo
zilihitaji kuelezwa kwa mawanda zaidi ya
yale ya ngano na hatithi fupi. Hapo hapo kuzuka kwa miji na viwanda
pamoja na maendeleo ya wasomaji yalifanya riwaya nyingi ziandikwe. Uchangamano
wa maisha ya jamii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wenyewe ulizusha haja ya kuwa na utanzu wa
fasihi ulio na uchangamano kifani na kimaudhui. Kupanuka kwa usomaji, hasa
wakati wa mapinduzi ya viwanda huko Ulaya, kuliwafanya waandishi waandike
waandiko marefu kwani sasa walikuwapo wasomaji hasa wanawake waliobaki
majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani, wasomaji ambao muda wao
uliwaruhusu kusoma maandiko marefu marefu ijapokuwa hii lilikuwa jambo la
baadaye sana wakati wa kina Charles Dickens. Hii historia fupi ya
chimbuko. Senkoro (2011:55)
Baada
ya kuangalia historia fupi ya chimbuko la riwaya ni vyema tukaangalia nduni
bainifu za riwaya kwa kuziainisha katika aya moja. Kwa mujibu wa Wamitila (2002) sifa
hizo ni kama zifuatazo;
Uwazi
na uangavu, kazi husika ya fasihi isiwasumbue na kuwatatiza wasomaji kuzielewa,
muwala na muumano, kazi ya riwaya lazima iwe na mshikamano au mtiririko mzuri
wa visa au matukio kuijenga kazi ya kifasihi, uchangamano wa visa yaani kutokea
kisa zaidi kimoja, wingi wa maana kuhusiana na sifa ya uchangamano na ukamilifu
ni kule kuwako kwa elemeti zote muhumiu na za kimsingi katika kazi ya fasihi.
Baada
ya kuangakulia sifa au nduni bainifu za riwaya tuangalie aina za riwaya kwa
mujibu wa watalamu mbalimbali;
Katika
uainishaji wa aina za riwaya, wataalamu wametumia vigezo mbalimbali vya
uainishaji kama vile msingi wa kidhamira ambao kwa kiasi kikumbwa sifa za
kimaudhui, kifani, kihistoria na kiitikadi. Katika uainishaji wa aina za riwaya
kwa kutumia vigezo hivyo wataalamu wamefanana kuainisha baadhi ya aina za
riwaya. Mfano Mulokozi (1996), Wamitila (2003) na Madumulla (2009) aina walizofanana kuainisha ni kama
zifuatazo;
Riwaya
saikolojia
ni aina ya riwaya inayododosa nafsi ya
mhusika, fikra, hisia mawazo, imani, hofu, mashaka, matumaini na athari ya
mambo hayo kwake binafsi na labda kwa jamii mfano “Kichwa Maji” ya E.Kezilahabi, “Kipimo cha Mianzi” ya Feud na
“Kiu” ya M.S. Mohammed.
Riwaya
ya kisosholojia au jamii ni riwaya ambayo inasawiri maisha ya kawaida ya jamii kwa
kuchunguza matatizo yake, yawe kifamilia kitabaka, kiuchumi, kisiasa au hata
kiutamaduni mfano “Titi la Mkwe” ya A.
Banzi, “Kurwa na Doto” ya M.S. Farsi na “Rosa Mistika” ya E. Kezilahabi.
Riwaya historia ni aina ya riwaya ambayo msingi wake
kuhusu matukio fulani katika jamii ya mwandishi, tukio hili huwa ni kubwa na la muhimu kijamii, laweza
kuwa la kikabila au la kitaifa mfano “Uhuru wa Watumwa” ya J. Mbotela,
“Miradi Bubu ya Wazalendo” ya Luhumbika na “Zawadi ya Ushindi” ya B. Mtombwa.
Riwaya ya uhalifu ni riwaya ambayo hujihusisha na
uhalifu wa aina mbalimbali kama vile ujambazi, uuaji, magendo na utapeli. Mfano
“Kwa sababu ya Pesa” ya Simbamwene na “Sanda ya Jambazi” ya H. Jajab.
Riwaya ya upelelezi ni aina ya riwaya ambayo huwa na vitu
viwili yaani kosa /uhalifu na upelelezi wa uhalifu huo hadi mhalifu
anapopatikana, hivyo wahusika wake ni wahalifu, wadhurumiwa na wapelelezi
wakiwemo polisi “Mzimu wa Watu wa Kale” ya M.S. Abdallah na “Duniani kuna Watu”
ya M.S. Abdulla.
Baada
ya kuonesha aina za riwaya ambazo zimeainishwa na wataalamu hawa wote sasa tuangalie aina za riwaya ambazo wanafanana Wamitila na Mulokozi aina hizo ni kama zifuatazo;
Riwaya
barua
ni riwaya ambayo huwa na muundo wa barua kuanzia mwanzo hadi mwisho mfano “Pamela” ya S.Richardson na “ Barua
Ndefu kama Hii”
Riwaya ya vitisho ni riwaya yenye visa vya kusisimua
damu na mara nyingi visa hivyo huambatana na matukio ya ajabu na miujiza mfano “Mirathi ya Hatari”
ya Mung’ong’o na “Vipuli vya Figo” ya E.
Mbogo.
Riwaya teti ni riwaya ambayo huathiriwa na
kuchimbuka kutegemea jinsi mhusika mkuu anavyosawiriwa. Mhusika huyu huukejeli
mfumo wa kiutawala uliopo katika jamii yake. Riwaya hii huonesha vituko ambavyo
ni vigumu kukubalika vinavyotokea katika jamii mfano “Unfortune Traveler”
ya Daniel Defoi.
Riwaya ya majaribio, ni riwaya inayojadili mkondo wa
nafasi na riwaya kweli. Riwaya ya mjadara nafsi hutungwa bila kuzingatia kanuni
za kawaida za uandishi wa riwaya, watunzi wa riwaya hii hudai kuwa kumbo la
kawaida ya riwaya hii haitoshelezi mahitaji ya karne hii huwakilisha ukweli wa
maisha. Mfano, “Mtunzi wa Hukumu” ya Kasri na “Bina-Adamu” na Musaleo” za
Wamitila.
Baada
ya kuonesha aina za riwaya ambazo zimeainishwa na Mulokozi pamoja na Wamitila
sasa tuangalie aina za riwaya ambazo zimeainishwa na Wamitila na Madumulla.
Riwaya hizo ni kama zifuatazo;
Riwaya ya kitawasifu, ni riwaya ambayo ina muundo unafanana
na muundo wa tawasifu kwa kuyachunguza maisha ya mtu fulani na kwa nafsi ya
kwanza. Mfano riwaya ya “Uhuru wa watumwa” J. Mbotela na “Maisha Yangu baada ya
Miaka Hamsini” ya S.Robert.
Riwaya ya wasifu, ni riwaya ambayo mwandishi huandika
kwa lengo la kumhusu mtu fulani, mfano “Wasifu wa Siti Binti Saad” ya S.
Robert.
Riwaya ya kifalsafa, ni riwaya ambayo inashughulikia
masuala ya kifalsafa. Mada ya kifalsafa huchukua sehemu muhimu katika riwaya ya
aina hii kuliko wahusika, mandhari, msuko au mtukio. Mfano, “Nagona na
Mzingile” ya E kezilahabi na “Umleavyo” ya Haji Gorra Haji.
Baada
ya kuonesha aina za riwaya ambazo zimeainishwa na Wamitila na Madumulla,
tuangalie zile ambazo zimejadiliwa na Mulokozi na Madumulla ambazo
hazijaainishwa na Wamitila.
Riwaya
ya mapenzi ni riwaya yenye kusawiri uhusiano wa kimapenzi kati mvulana na
msichana. Mfano “Kweli Unanipenda”
“Mwisho wa Mapenzi” za Simbamwene.
Riwaya ya ujasusi ni wa upelelezi wa kimataifa. Majasusi
ni wapelelezi wanaotumwa na; nchi, serikali au waajiri wao kwenda katika nchi
nyingine kuchunguza siri zao hasa siri za kijeshi, kiuchumi na kisayansi ili
taarifa hizo ziwanufaishe wale waliotumwa mfano “The thirty nine steps” ya E.
Msiba. “Mzimu wa Watu wa Kale”.
Baada
ya kuonesha ufanano wa uainishaji wa aina za riwaya kwa mujibu wataalamu hawa tuangalie aina za riwaya ambazo
zimeainishwa na mtaalamu mmoja mmoja bila wengine kuziainisha aina
hizo.Tukianza na Wamitila ameainisha aina za ruiwaya kama zifuatazo;
Riwaya changamano; ni riwaya ambayo ina muundo mgumu na
inayohitaji umakini kuielewa. Kwa kawaida msuko wa riwaya hii huwa tata.
Inawezekana pakawepo na matumizi mapana ya mbinu rejeshi, upana mkubwa wa
wahusika na mandhari, matumizi mengi ya lugha ya kitamathali, mfano; “Mzingile”
ya E. kezilahabi, “Zirail na Zirani” ya W.E Mkufya.
Riwaya sahili; ni dhana inayotumiwa kuelezea aina za
riwaya ambayo ina muundo rahisi na inaweza kueleweka kwa urahisi. Kwa mfano;
riwaya ya “Kaburi Bila Msalaba” ya P . Kureithi.
Riwaya tatizo; ni riwaya ambayo inajishughulisha na
tatizo au mgogoro fulani katika jamii. Huweza pia kuelezea aina ya riwaya
ambayo inachunguza tasnifu au swala fulani la kisaikolojia. Mfano; “Kuli” ya
Shafi A.shafi na “Mafuta” ya K. Mkangi.
Riwaya kampasi; ni riwaya ambayo mandhari yake ni
chuo kikuu. Hata hivyo hii imepanuliwa na kuhusishwa na kazi za kuchekesha au
zenye mwelemeo wa kitashititi. Kazi za aina hii hukusudia kufichua udhaifu
uliopo katika tabia za wanachuo. Mfano; “Small world” ya David Lorge.
Riwaya ya kiambo; ni riwaya ambayo inatilia mkazo
kwenye mandhari, usemi au muundo wa kijamii na desturi za mahali maalumu.
Mandhari na mahali huathiri njia mbalimbali za kuhisi na kuwaza kwa wahusika
wanaopatikana kazi ya aina hii.
Riwaya ya kidastopia hii husawili jamii isiyokuwa ya kawaida na isiyokuako kwa
wakati maalumu bali inafikirika tu. Katika jamii hiyo sheria za kawaida za
kijamii zimebadilishwa kwa namna inayowafanya watu wengi waishie kutaabika na
kuteseka sana. Mfano wa riwaya hizi ni kama vile “ Kusadikika” ya Shabani
Robert na “Walenisi” ya Katama Mkangi.
Riwaya ya kimonolojia
ni riwaya ambayo sauti inayotawala ni moja. Sauti hiyo ni ya mwandishi.
Wahusika wanaopatikana katika riwaya hii hudhibitiwa kwa kiasi kikubwa na sauti
ya mwandishi. Mfano “Walenesi” na “Mafula” za Katama Mkangi.
Riwaya ya kipolifoni; ni riwaya ambayo inahusishwa na
urejeleaji ambapo kila wahusika
wanapozungumza au kuongea sauti zao mbalimbali zinawakilisha mikabala
mbalimbali kiitikadi. Mfano “Dunia mti mkavu” ya S.A Mohamed.
Riwaya ya kisasa; ni riwaya inayohusu wanasiasa na
maisha yao wanasiasa. Hudhamiria kuyafichua mambo yanayotendeka kinyume na
picha inayoonekakana waziwazi. Mfano; “Nyota ya Huzuni” ya George Liwenga na
“Njozi Iliyopotea” ya C.G. Mng’ong’o.
Riwaya ya kitarihi ni riwaya ambayo inajihusisha na
mawanda makubwa ya kiwakati na kimandhari.Wahusika wengi walioteuliwa kuakisi
hali mbalimbali za kijamii na kiuchumi za wakati maalumu. Mfano;Riwaya ya “Habari za Wakilindi”
Riwaya ya Kitasnifu ni riwaya inayojihusisha na tatizo
fulani la kijamii hasa kwa nia ya kuwahusisha
wasomaji. Katika hali fulani inayowapata wahusika na kwa njia hiyo
huwachochea kuwazia njia ya kusuluhisha tatizo hilo Mfano; “Njozi Iliyopotea”
ya M.Mng’ong’o na “Nyota ya Huzuni” ya G.Liwenga.
Riwaya ya kiutopia hii ni riwaya ambayo inasawiri jamii
anayoiona mwandishi kama jamii kielelezo na aghalabu huhusisha sifa za
Kifantasia au kinjozi. Mfano wa riwaya hii ni kama, “Siku ya Watenzi Wote” ya
Shaaban Robert
Riwaya ya kiurejelevu hii ni riwaya inayojirejelea. Aghalabu
katika usimulizi wake, riwaya ya aina
hii huishia kutoa maoni kuhusu usimulizi wake na njia za kubuni na kutunga
riwaya.Tunaweza kusema hii ni riwaya inayofichua mbinu zake za kiutunzi. Mfano
“Musaleo” ya K.W.Wamitila
Riwaya kinzani ni riwaya inayotumiwa kuelezea ambayo
imekwenda kinyume na matarajio au kaida za uandishi wa riwaya. Mfano, kuwa na
muundo wa kimajaribio wahusika kukosa motisha, kuwako kwa matendo yasiyoweza
kuungwa kimantiki.
Riwaya ya utetezi
hii hutumiwa kuielezea riwaya ambayo inahusu matatizo ya kijami,
kiuchumi pamoja na dhuluma inayowapata wanyonge au wasiokuwa na uwezo katika
jamii fulani. Hivyo riwaya hii hukusudia kurekebisha hali iliyopo katika jamii.
Mfano “Walenisi” na “Mafuta” ya Katama
Mkangi na “Kuli’ na “Vuta
n’kuvute” za Shafi A.Shafi.
Pia
kuna baadhi ya aina za riwaya ambazo
zimejadiliwa na Mulokozi ambazo
hazijajadiliwa na Wamitila na Madumulla. Aina hizo za riwaya ni kama zifuatazo;
Riwaya chuku
ni riwaya ambayo hueleza vituko na masahibu yasiyo kuwa ya kawaida, ni
riwaya ambayo haizingatii uhalisia na
mara nyingi masahibu yake huambatanana mapenzi.Mfano “Alfu lela Ulela” ya G.
Bocci ccio na “Kusadikika” ya S.Robert”
Riwaya ya kingano, ni riwaya yenye umbo na mtindo wa ngano
mathalani huweza kuwa na wahusika wanyama,visa vyenye kutendeka nje ya wakati
wa kihistoriA.Mfano “Lila na Fila” ya Longman na “Adili na Nduguze” ya S.Robert
Riwaya istiara ni riwaya mafumbo ambayo umbo lake la
nje ni ishara au kiwakilishi tu cha jambo jingine. Mfano “Kusadikika” ya S.Robert ambayo inasawili utwala wa mabavu na “Shamba la Wanyama” ya Kawegere.
Riwaya tendi ni riwaya yenye mawanda mapana kama
tendi aghalabu riwaya hii husawili matendo ya ushujaa na masuala mazito ya
kijamii yenye kuathiri historia ya taifa husika. Mfano “Vita na Amani” ya Leo
Tolstoi na “Chaka Mtemi wa Wazuru” ya Thomas M.
Riwaya ya kisayansi ni riwaya inayotumia taaluma ya sayansi kama msingi wa matukio, masahibu
na maudhui, mathalani riwaya hii hubashiri namna sayansi itakavyo athiri
maendeeo ya mwanadamu katika karne zijazo. Mfano “Safari Kiini cha Dunia” ya
Jules Vernes.
Kuna
baadhi ya aina ya riwaya ambazo zimejadiliwa na Madumulla ambazo hazijadiliwa
na Mulokozi na Wamitila. Ambazo ni kama zifuatazo;
Riwaya ya kimaadili ni riwaya ambayo ina nia ya kufundisha
maadili fulani mfano “Kufikirika” ya S Robert.
Ni riwaya inayotoa maadili kwa jamii.
Riwaya ya kimapinduzi ni riwaya ambayo inajadili migogoro na
maisha ya binadamu kwa kutafakari kwa mantiki na kina kuhusu mambo ambayo
urazini wake hauonekani kwa urahisi. Mfano “Umleavyo” ya Haji na Kichwa Maji”
ya E.Kezilahabi.
Hivyo
kutokana na uainishaji huu wa aina mbalimbali za riwaya kutoka kwa wataalamu
hawa tumeona kuwa wanatofautiana katika vigezo vya uainishaji ambapo tunaona
wanaainisha aina mbambali za riwaya. Kutokana na uainishaji huo tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa aina hizo zote za riwaya zinaweza kuangukia katika
aina kuu mbili za riwaya ambazo ni riwaya ya dhati na riwaya pendwa. Riwaya
pendwa ni riwaya ni riwaya ambazo hutungwa kwa lengo la kuburudisha na
kumstarehesha msomaji mfano, riwaya za kimapenzi, kimahaba, kiuharifu,
kiupelelezi na kijasusi. Wakati riwaya ya dhati ni riwaya ambazo huchimbua na
kuchambua masuala mbalimbali ya kijamii, yaani hutafuta chanzo chake sababu
zake mpaka kikatokea athari na suluhisho lake. Hivyo tunaweza kusema kuwa aina
za riwaya ambazo hukosekana katika aina mojawapo ya riwaya dhati huwa
katika riwaya pendwa.
MALEJEO.
Madumulla,
S.J. (2009) Riwaya ya Kiswahili: Nadharia Historia na Misingi ya Uchambuzi.
Dar es Salaam:
Mture Educational Publishers Ltd.
Mulokozi,
M.M. (1996) Utangulizi wa Fasihi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Senkoro,
F.E.M.K. (2011) Fasihi. Dar es
Salaam: KAUTTU.
Wamitila,
K.W. (2002) Uhakiki wa Fasihi: Misingi na
Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix
Publishers Ltd.
Wamitila,
K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publicatins
Ltd.