NADHARIA ZA CHIMBUKO LA NGANO/MASIMULIZI
NADHARIA ZA CHIMBUKO LA NGANO/MASIMULIZI
Kazi
hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika sehemu
hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo
tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya
fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka
(1994/1999) na Finnegan (1970). Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Tukianza
na fasili ya Nadharia, Massamba (2009:63) anasema, nadharia ni taratibu
kanuni na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa
madhumuni ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea jambo. Sarantakos
(1997: 9) amefasili nadharia kama jambo linalofanywa na kuthibitishwa
kwa utaratibu maalum kwa njia ya utafiti kwa ajili ya kuelezea jambo
fulani katika jamii. Martin E. Amini (2005:10) anasema nadharia ni jumla
ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia kuelezea, kuchambua, kuelewa au
hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalum.
Hivyo
basi, nadharia huchukuliwa kama dira au muongozo wa kumuongoza
mtafiti/mchambuzi ili kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo
unaotarajiwa kuwa imara zaidi kuliko mtazamo mwingine. Hivyo tunaweza
kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi simulizi ni chombo kinachotoa
mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani.
Maana ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema, ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei
(2005:65) anasema ngano kuwa ni hadithi fupi na zenye
masimulizi yasiyo ya kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W.
(2003:165) anasema ngano ni hadithi ya kale ambayo ni moja kati ya
tanzu maarufu za fasili simulizi. Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya
hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na mwanzo wa hapo zamani za
kale.
Kwa
fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi
ambazo huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika
jamii husika na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Baada
ya kuangalia fasili mbalimbali za nadharia na ngano, sehemu inayofuata
ni kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi
simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na
Finnegan (1970). Tukianza na Okpewho (1992) ameanisha aina sita za
nadharia zinazoelezea asili ya fasihi simulizi/masimulizi ambazo ni,
nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya uamilifu,
nadharia ya urasimi, nadharia ya Saikochanganuzi na mwisho ni nadharia
ya Umuundo. Kwa upande wake, Miruka (1994) ameanisha aina tano za
nadharia ambazo ni, nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao,
nadharia ya urasimi, nadharia ya uamilifu na nadharia ya umuundo, wakati
Finnegan (1970) ameanisha aina tatu za nadharia ambazo ni nadharia ya
Mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya Umuundo.
Tukiangalia
uanishaji wa nadharia hizo za wataalamu hapo juu, tunaona kuwa,
wataalamu hao wanatofautiana katika idadi ya nadharia hizo, lakini
kimsingi wataalamu wote wanakubaliana kuhusu nadharia fulani fulani,
mathalani, wote wanakubaliana uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia
ya msambao na nadharia ya umuundo. Lakini Okpewho na Miruka
wanakubaliana juu ya uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya
msambao na nadharia ya umuundo, nadharia ya urasimi na nadharia ya
uamilifu. Okpewho anainisha aina nyingine ya nadharia ya Saikochanganuzi
ambayo haijitokezi kwa hao wataalamu wengine. Hivyo katika uwasilishaji
wetu, tutazigawa nadharia hizo katika aina sita kama ifuatavyo:
Nadharia ya wanamabadiliko,
nadharia hii iliasisiwa na Charles Darwin ambaye alikuwa mwana bailojia
karne ya 19, alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe ambao
waliishi miaka mamilioni iliyopita. Katika utafiti wake aligundua kuwa
viumbe walioendelea kuishi imewezekana tu kwa sababu ya kumudu
mapambano dhidi ya uhaba wa vyakula, hivyo Darwin aliita jambo hili kama
“Uhai kwa wanaofaa”. Pia aligundua viumbe walioendelea kuishi kwa
sababu ya maumbo yao na mazingira yaliyosababisha wao kuwepo.
Mawazo
ya utafiti wa Darwin yalishadadiwa na wanazuoni mbalimbali waliokuwa
wanachunguza utamaduni wa binadamu, katika utafiti wao walikusanya
simulizi kutoka jamii mbalimbali za Afrika, Asia na Amerika ambapo baada
ya kukusanya simulizi hizo waligundua zilikuwa na ufanano wa kimaudhui.
Wanamabadiliko wanaamini kuwa ngano/masimulizi tuliyonayo leo yana
asili moja isipokuwa zimekuwa zikibadilika kutokana na mabadiliko ya
wakati. Zaidi ya haya wanamabadiliko wanaamini kuwa viumbe wote
tumetokea kwenye asili moja hivyo tuna uwezo wa akili sawa na maendeleo
tutakuwa sawa.
Ubora wa nadharia hii, nadharia
hii ndiyo msingi wa nadharia nyingine zilizofuata kama nadharia ya
msambao, urasimi na uamilifu. Vilevile imesaidia kuelezea asili ya
ngano/masimulizi hasa ngano zinazofanana kimaudhui, na mwisho nadharia
imesaidia kuonesha kuwa ngano zina asili moja isipokuwa zinabadilika
kutokana na mabadiliko ya wakati na mazingira.
Mapungufu ya nadharia hii, wanamabadiliko
waliamini kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi kilihesabika kama
masalia ya zamani/mabaki ya fasihi zilizotangulia, kwa maana kwamba
kila kitu kilichosalia kitakuwa na dosari hakiwezi kuwa kitu halisi.
Wanamabadiliko pia wameangalia tu upande wa maudhui na kuacha kipengele
cha fani kama vile muundo na mitindo ya fani husika. Mwisho, pamoja na
ufanano wa huo wa kimaudhui kuwa ngano zina asili moja lakini kuna
tofauti kubwa hasa katika utendaji wa fanani hivyo fanani hutofautiana.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia
hii inahusiana na ngano za Kiswahili katika sanaa za jadi ambayo ni
elimu inayohusu asili ya binadamu pamoja na umuhimu wake ambao
ilihusishwa na usimulizi wa ngano ambayo ilitokana na jamii husika
katika shughuli mbalimbali za jamii kama vile jando na unyago, miviga,
vyanzo vya vyakula, sherehe, matambiko kwa kutaja kwa uchache.
Nadharia ya msambao, nadharia
hii imeasisiwa na wataalamu kama Jacob na Wilhem Grimm, baadaye mawazo
yao yaliendelezwa na Maxmuller na Mmarekani Stere Thomson. Pamoja na
kwamba kulikuwa na tofauti ndogondogo lakini wataalamu wa nadharia hii
wanamwelekeo mmoja ambao wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni
moja lakini kutokana na maingiliano ya kijamii ndiyo yaliyosababisha
kusambaa kwa hii ngano hasa kutoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya)
kuja katika jamii zisizostaarabika (Afrika).
Okpewho
anasema, wanamsambao walijishughulisha na kuhusianisha ngano za jamii
mbalimbali na kugundua kuwa ngano zina ufanano unaokaribiana sana.
Uhusiano huu unahusishwa na kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na
mawasiliano baina ya jamii moja hadi nyingine. Katika utafiti wao
wanamsambao wamegawanywa katika shule mbili, kwanza ni kundi la shule ya
India, kundi hili lilianzishwa na Jacob na Wilhelm ambapo walikusanya
hadithi mbalimbali huko ujerumani na kwingineko barani Ulaya na kugundua
kuwa ngano hizo zilikuwa na uhusiano na kuhitimisha kuwa ngano za Ulaya
kama zilivyo lugha za Ulaya zimeonekana na rangi ya nasaba bora
iliyopata kuishi huko kati ya kaskazini na Asia, rangi ya nasaba bora si
rangi ya ngozi bali ni familia ya lugha ambayo lugha zote za Ulaya
zinahusishwa nayo. Hivyo aligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa na
makundi ya wahamiaji. Wao waliona chimbuko la ngano ni huko India na
zikafika huko Magharibi kwa njia ya msambao.
Kundi
la pili ni kundi la shule ya Kifini, shule hii ilianzishwa na Eliasi
Lonnrot ambaye mwaka 1825 alianza kukusanya ngano za mashujaa katika
nchi ya Finland, kupitia maudhui yanayohusiana na kuziweka katika kundi
moja.
Ubora wa nadharia hii,
wanamsambao waliipa hadhi fasihi simulizi kwa kuchunguza muktadha kwa
undani, vilevile, nadharia hii ilionekana kuwa ni ya kisayansi zaidi,
hivyo inaweza kuchunguzika tofauti na wanamabadiliko kwani akili ya mtu
haiwezi kuchunguzika.
Upungufu wa wa nadharia hii, kufikiria
kuwa ngano zimeenea toka kundi moja la watu hadi kundi jingine,
inaonesha kuwa jamii ya Kiafrika haikuwa na ngano. Nadharia hii inaona
kuwa Afrika haikuwa na ngano kwani ngano zilitoka katika jamii
zilizostaarabika (Ulaya) jambo ambalo si kweli kwani hata kabla ya ujio
wa wakoloni Waafrika walikuwa na ngano zao. Vilevile, licha ya kuipa
fasihi simulizi upekee katika kipengele cha muktadha lakini
hawakuchunguza kwa undani vipengele vya kisanaa vya fasihi simulizi,
mfano hawakuangalia vipengele muhimu vya fasihi simulizi ya Kiafrika
hususani sanaa ya jadi kama vile, miviga, jando na unyago, matambiko,
n.k.
Nafasi ya nadharia hii
katika ngano za Kiswahili, ukiangalia kwa jicho la ndani nadharia hii
inasaidia kutambua kuwa mfanano wa ngano katika jamii nyingi za kiafrika
ulitokana na maingiliano ya shughuli za kijamii kama vile, biashara,
kilimo,ufugaji, uwindaji na kazi mbalimbali za jamii.
Nadharia ya umuundo,
nadharia hii iliasisiwa na Claude Levis Strauses, alidai kuwa utamaduni
unajumuisha vitu mbalimbali vinavyofanana, alichunguza visasili na
kusema kuwa visasili hivyo vinatumika katika kuelezea na kutatua
matatizo katika jamii. Hadithi hizo zilikuwa zinaelezea falsafa ya jamii
husika, alidai kuwa visasili hivyo vilisaidia jamii katika kuyaelewa na
kutatua matatizo ambayo yalileta mtanziko katika maisha ya binadamu,
matatizo hayo ni kama vile, uhai na kifo.
Strauses,
alidai kuwa muhusika wa ngano anajengwa katika kupambana na tatiziko
ambalo anashindwa kulipatia majibu. Dominique Zahen aliongeza kuwa
ngano zinahusu uhai na kifo na ziishie kwa kuona kuwa uhai na kifo
vimetoka kwa mungu (mfano: ngano inayoelezea namna kifo kilivyoingia
duniani) (rejea Miruka 1994:138)
Ngano
zinatakiwa kutazamwa kama mfumo wenye kanuni zake ambazo kila msanii
anatakiwa kuelewa pia aelewe mfumo unavyoweza kutumiwa katika
mawasiliano na hata kimuundo. Mfano katika ngano lazima kuangalia
matumizi ya lugha na kaida zinazotawala utunzi huo.
Ubora wa nadharia hii,
nadharia hii inasisitiza kuwepo kwa kanuni/kaida maalumu za kiutambaji,
kiutunzi na matumizi ya lugha. Hapa wanaona kuwa ngano zisichukuliwe
kama kitu pekepeke bali ni utanzu unaoongozwa na kaida maalumu katika
uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha. Hivyo kutakuwa na sifa
zinazofanana katika ngano zote. Vilevile, inasaidia kujua chimbuko la
ngano katika jamii fulani.
Udhaifu wa nadharia hii, kwanza
kwa kutumia nadharia hii hatuwezi kupata kanuni rasmi ya kiutambaji,
kiutunzi na matumizi ya lugha toka jamii moja hadi nyingine. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba kila jamii ina namna yake ya kuwasilisha ngano
zao, kuziumba ngano zao na matumizi ya tofauti ya lugha. Mfano; maumbo
ya ngano yanatofautiana toka jamii moja hadi nyingine, mfano,
muingiliano wa tanzu moja katika nyingine, utambaji pia hutofautiana,
mfano watambaji na tabaka tawala na watambaji na tabaka duni. Hata
wahusika wa ngano pia hutofautina mhusika anaweza kuwa mtu duni kwenda
bora au mtu bora kuwa mtu duni. Nadharia hii pia inatalia mkazo muundo
kuliko dhima ya ngano katika jamii.
Nafasi ya nadharia hii
katika ngano za Kiswahili, nadhairia inasaidia wanafasihi
kutambua/kuelewa ngano kama utanzu wa fasihi una muundo wake rasmi
katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha kiulemwengu lakini
muundo huo si wa kimajumui kwa maana huweza kutofautiana kutoka jamii
moja hadi nyingine.
Nadharia ya urasimi, nadharia hii iliasisiwa na mwanazuoni wa Kinesi Vladimir Propp (1928,1968) katika chake cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia
hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji
wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini
kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vema kuanza kuchunguza aina za
ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili
ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika.
Ubora wa nadhairia hii,
nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake,
mfano ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki,
(Alan Dunde’s)
Udhaifu wa nadharia,
nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya
ngano yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji
wake.
Nafasi
ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia
kuziweka ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata
ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na wahusika
wasiowaelevu/wajinga mfano fisi.
Nadharia ya saiko-changanuzi, muasisi
wa Nadharia hii ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu
alikuwa tabibu wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia,
alichunguza hasa sehemu ya nafsi iliyofichika yaani sehemu ya ung’amuzi
bwete ili kujua asili ya tatizo la mgonjwa husika, alieleza kuwa
ung’amuzi bwete ni sehemu ya akili ya binadamu ambayo huhodhi fikra,
mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo haiwezi kukubalika na jamii. Hofu
na mawazo hayo hujitokeza kwa ndoto. Pia ung’amuzi bwete huhusisha
matukio yaliyotendeka zamani lakini mgonjwa huyaingiza katika maongezi
yake kama yanatendeka muda huo. Kutokana na utafiti wake aligundua
kwamba ndoto zote husheheni ukweli kuhusu maisha ya mgonjwa.
Freud
anaifananisha kazi ya fasihi na ndoto kwa kuwa visasili huwa ni hadithi
za kubuni basi ubunifu huo unashabihi ndoto kwani wahusika wake na
maudhui yake kwa ujumla huwa katika ulimwengu wa kufikirika ambao ni
kama ndoto katika ulimwengu halisi sawa sawa na mgonjwa wa akili
anayeumba ulimwengu wake.
Freud
alisisitiza mambo yote katika akili ya binadamu yanatawaliwa na ngono
(libido). Mawazo yake yaliungwa mkono na mwanafunzi wake Carl Gustav
Jung ambaye pia alifanya kazi pamoja na Freud katika kuwatibu wagonjwa
wa akili kwa kutafsiri ndoto ingawa Gustav alitofautiana na Freud kwa
msimamo wake kuwa akili ya binadamu inatawaliwa na ngono.
Carl
Gustav Jung alifanya utafiti na kuunda dhana ya kikale ambayo ni
mtiririko au picha kongwe inayojitokeza mara kwa mara katika tajriba
anayopitia mwanadamu , alisema kuna sehemu ndani ya akili isiyokuwa na
fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa juu ya mawazo na matendo
yake. Alitofautisha sehemu hiyo kama, sehemu ya kwanza ni sehemu binafsi
inayofunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake na
sehemu ya pili ni sehemu ya kijamii inayofunza maarifa ya kibinadamu
yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa kwa karne
nyingi. Anasema sehemu hii husika na matambiko muhimu ambayo mtu
anapitia kama sherehe za kumpa mtu jina, sherehe za kuingia jandoni na
unyagoni, sherehe zinazoigizwa wakati wa ndoa na hatimaye sherehe
zinazohusu maziko ambazo sherehe zote hii ndizo huibua ngano.
Gustav
alifafanua kwa undani masuala ya ngano katika tamaduni mbalimbali za
dunia. Hivyo Freud na Gustav wanasema masimulizi ni kama ndoto au
mvurugiko wa akili kwani picha, taswira na maudhui vyote ni vya kubuni
havitoki katika ulimwengu halisi.
Ubora wa Nadharia hii,
Nadharia hii inaonesha utofauti wa msimulizi mmoja hadi mwingine
hutokana na historia ya mtu binafsi na uwezo wake binafsi hata kama kisa
kitakachosimuliwa ni kimoja, hii imedhihirishwa kwa wagonjwa waliokuwa
wanasimulia mambo yao kwa utofauti kutokana na historia zao. Lakini pia
imesaidia kutuonesha chimbuko la ngano kwa miktadha tofauti tofauti kama
sherehe za jando na unyago, sherehe za kutoa jina, n.k.
Upungufu wa Nadharia hii,
Nadharia hii imesisitiza zaidi masuala ya hisia za kingono katika
ubunifu wa masimulizi kitu ambacho hakina ushahidi wa kutosha kwani siyo
kila hadithi inatarajia kujiridhisha kutoka hali ya ngono iliyofifizwa
katika ung’amuzi bwete kama anavyosema Freud.
Nadharia ya kiuamilifu,
Nadharia hii iliasisiwa karne ya 20 na Poland Bronislav Malinowsk.
Uamilifu uliibuka kama njia yal kuyatazama maisha na utamaduni wa jamii,
kwa kuchunguza dhima za vipengele vya kijamii pamoja na njia ambazo
kwazo dhima hizi zinahakikisha uwepo wa jamii. Malinowsk alifanya
utafiti Australia na kugundua kuwa ngano ni kumbukumbu za kweli za mila
na desturi za jamii zilizopita, unyago, jando, mazishi, harusi, tohara,
matambiko, kusalia miungu, n.k.
Ubora wa Nadharia hii,
Nadharia hii imesaidia kuondoa mawazo kuwa chimbuko la fasihi
mbalimbali zikiwemo ngano ni mahali fulani bali ni kila jamii imekuwa na
simulizi ambazo zinasawiri tajriba (uzoefu) wao wa kila siku katika
Nyanja mbalimbali kama vile, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Vilevile Nadharia hii, inatusaidia kujielewa na kuzielewa jamii zetu
vizuri, kwa kuyaelewa mazingira ya mila na desturi zetu katika jimii.
Nafasi ya Nadharia hii
katika ngano za Kiswahili, inatusaidia kujua tamaduni zetu katika somo
la ngano, pia inatusaidia kujua kuwa kila jamii ilikuwa na tamaduni zao
zenye kuwaongoza katika maisha yao ya kila siku kama vile, jando na
unyago, harusi, matambiko, mazishi, miviga, kusalia miungu kuwa ndiyo
chimbuko la ngano.
Hitimisho,
kila nadharia tuliyoiangalia ina umuhimu wake katika kujifunza chimbuko
la ngano, hivyo ni muhimu kila mwanataaluma wa ngano kuzisoma na
kuzielewa nadharia zote zinazozungumzia chimbuko la ngano kwa sababu
kila nadharia ina misingi yake ambayo kwa namna moja ama nyingine
inatusaidia kujua na kuelewa chimbuko la ngano, Nadharia hizi ni muhimu
pia kujifunza kwa sababu kuanzishwa kwa nadharia inategemea na upungufu
unaojitokeza katika nadharia nyingine. Kwa ujumla licha ya mtenguo wa
nadharia moja dhidi ya nyingine tunaona kuwa Nadharia hizi
zinakamilisha, Nadharia moja inakamilisha Nadharia nyingine. Kwa maana
hiyo, hatuwezi kujua au kuthibitisha chimbuka la ngano kwa kutumia
nadharia moja.
MAREJEO
Finnegan, R. (1976) Oral Literature in Africa. Oxford University Press. Nairobi.
Kingei, K na Kisovi, C (2005), Msingi wa Fasihi simulizi. Nairobi: Kenya Literature
Bureau.
Martin E.Amin (2005),Social Science Researc Conception,Methodology and
Analysis.Makerere University
Massamba (2009:63) Kamusi ya isimu na lugha, Falsafa ya Lugha. Dar es salaam.TUKI.
Mhando,J. na Balisidya, N. (1976) Fasihi , Tanzania Publishing House, Dar es salaam.
Miruka, O.S. (1994) Encounter with Oral Literature, East African Educational
Publisher.Nairobi. Kenya.
Muhando, P & Balisidya, N (1976) Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Tanzania Publishing
House(TPH) Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1989:5) “Tanzu za Fasihi Simulizi” Katika MULIKA Na. 21, D.SM. TUKI
Nkwera, F.V. (xx) Tamrini za Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo, Dar es Salaam: Business Printers Limited
Okpewho, I. (1992) African Oral Literature. Backgrounds, Character, and Continuity.
Indiana University Press: USA.
Sarantakos. S.(1997), Social Research. (2nd Edition) Palgrave Publisher Ltd (Formerly
Macmillan Press Ltd)
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi. KAUTITU Limited. Dar es salaam.
Wamitila. K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia. Focus Books.Nairobi.Kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848) kuthibitisha kuwa, hadi kufikia miaka 800 BK hadi 900 BK mijongeo ya wabantu ilikwashafika maeneo ya mito ya juba na tana
Na. Furaha Venance
M.A.KISWAHILI (UDSM)
2015
Ikisiri
Mijongeo
ya Wabantu na kutamakani katika upwa wa Afrika Mashariki ni suala
ambalo limewashughulisha wataalamu mbalimbali. Ama kwa hakika wataalamu
walio wengi wanaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia miaka 800 BK na
900 BK mijongeo ya Wabantu ilikuwa tayari imekwishafika maeneo ya Mto
Juba na Mto Tana. Hivyo basi, katika makala haya tunakusudia kutumia
nadharia ya Barker (1848) na nadharia ya Turton (1975) kuafiki kuwa,
mpaka kufikia miaka 800BK na 900BK wabantu walishafika na kutamakani
maeneo tajwa hapo juu. Ili kufikia lengo hilo, makala haya yamegwanyika
katika sehemu tatu sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo kwa kifupi
tutaeleza maana ya Wabantu, sehemu ya pili ambapo ndiyo kiini cha makala
haya itakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza tutaanza kutalii mawazo
ya baadhi ya wataalamu yanayodai kuwa mpaka kufikia miaka hiyo Wabantu
walishajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana na sehemu ya
pili ya sehemu hii ndipo tutatumia nadharia ya Barker na Turton
kuthibitisha ama kuafiki kuwa mpaka kufikia miaka ya 800 na 900BK
Wabantu walishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Sehemu
ya tatu ambao ndiyo sehemu ya mwisho itakuwa ni hitimisho la makala
haya.
1.0 Utangulizi
Katika lugha nyingi za kibantu neno bantu1 lina
maana ya watu Mapunda (1980: 26). Neno Bantu kwa mara ya kwanza
lilianza kutumiwa na Dkt. Wilhelm Bleek (1827-1875) katika kitabu chake
kilichochapishwa mwaka 1862 kilichopewa jina la Comparative Grammar of South African Languages Collins
(1968), Massamba (2002). Bleek alitumia neno Bantu kurejea kundi la
lugha alizozilinganisha sarufi za lugha husika hususani kwa kuangalia
mfumo wa ngeli za majina na vitenzi na kugundua kuwa lugha hizo
zinafanana Massamba (2002:36). Mapunda (keshatajwa, 26-27) anaeleza
kuwa, wanahistoria wanaelekea kukubaliana kuwa Wabantu ni jamii ya watu
ambao huzungumza lugha zenye asili moja. Aidha, Nurse na Spear (1985:37)
wanaeleza kuwa Wabantu ni watu walio na nasaba moja ya Proto-Bantu,
waliosambaa labda katika milenia ya pili. Watu hawa wanasadikika kutokea
katika kitovu kimoja asili yake ni huko Kameruni na Nigeria ya
mashariki. Ama kuhusu madai lao kwamba chimbuko la Wabantu ni huko
Kameruni na Nigeria bado wataalamu wanatofautiana kuhusiana na chimbuko
la Wabantu.
Aidha, Johnson (1919)
katika nadharia yake inayojulikana kama nadharia ya Johnson kuhusu
chimbuko la Wabantu na mijongeo yao anaeleza kuwa, mtawanyiko wa
Wabantu-Azali ulichukua mwelekeo wa mashariki kuelekea maeneo ya
kaskazini ya Maziwa ya Albert na Nyanza ambayo yapo kusini magharibi ya
Sudan na kaskazini ya Uganda. Kwa mujibu wa maelezo yake, Maziwa ya
Albert na Nyanza kwa maana ya Uganda-Albert-Nile ndiyo kitovu cha
chimbuko la Wabantu. Kwa upande wake Greenberg (1955) anatofautiana na
Johnson anayedai kuwa, chimbuko la Wabantu ni Uganda-Albert-Nile, kwa
maoni yake anadai [1]chimbuko
la Wabantu ni mpakani mwa Kameruni na Nigeria na baada ya kutoka maeneo
hayo wakaanza kushuka kuelekea kusini mwa Jangwa la Sahara Massamba
(2002). Tukiyatazama madai haya tutaona kuwa ndiyo yanayoelekea kuungwa
mkono na Nurse na Spear katika fasili yao kuhusu Wabantu na chimbuko lao
kama tuliyoitazama hapo juu.
Nadharia nyingine
inayozungumzia chimbuko na mtawanyiko wa Wabantu ni nadharia ya Malcom
Guthrie (1970). Mtaalamu huyo anaonekana kupinga mawazo yote ya
watangulizi wake wanaodai kuwa, chimbuko la wabantu ni
Uganda-Albert-Nile (Johnson) na chimbuko la Wabantu kuwa ni mpakani mwa
Kameruni na Nigeria (Greenberg). Guthrie anadai kuwa Wazungumzaji wa
Kibantu wa mwanzo walikuwa eneo lenye pori kusini mwa msitu wa Ikweta
kati ya makutano ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantiki. Kwa mujibu
wa ramani ya sasa eneo hilo linalotajwa yanasemekana kuwa lipo nchini
Zambia Massamba (2007:43-44).
Kwa kuwa lengo letu si
kuzijadili nadharia hizi katika makala haya, itoshe kusema kuwa kwa
hakika hatuwezi kupinga ama kukubaliana na akina Nurse na Spear ama
nadharia hizo kuhusu hasa chimbuko la Wabantu kwani suala bado
linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi ingawa wanahistoria wengi
wanakubaliana kuwa, chimbuko la Wabantu ni huko Afrika Magharibi
inakadiriwa miaka 2500 hadi miaka 3000 iliyopita, Wabantu walianza
kusambaa maeneo mbalimbali kutokea Afrika Magharibi hususani mashariki
ya Nigeria na Kameruni. Wabantu hao waliingia Afrika Mashariki
wakitokea huko Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mapunda
(keshatajwa: 27)
Kwa maana hiyo
tunaweza sema kuwa, Wabantu ni jamii ya Waafrika wenye nasaba moja na
huzungumza lugha zenye asili moja ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusiana,
wanapatikana kuanzia Afrika Magharibi, Afrika ya Kati hadi kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Mtawanyiko wa Wabantu
kwa kutumia nadharia inayodai kuwa, chimbuko lao ni Afrika Magharibi
hususani maeneo ya Kameruni na Nigeria unaweza kuonekana vizuri katika
ramani ifuatayo:
2.0 Kiini cha Makala
2.1 Madai
kwamba hadi kufikia miaka 800 BK na 900 BK mijongeo ya Wabantu
ilikwishafika maeneo ya mto Juba na Tana kwa mujibu wa wataalamu
mbalimbali.
Kama tulivyokwisha
dokeza hapo awali. Katika sehemu tutayatalii mawazo ya baadhi ya
wataalamu ambayo kwa hakika yaelekeana kukubaliana na hoja hii kuwa
mpaka kufikia miaka hiyo mjongeo wa Wabantu ilikwishafika maeneo ya mto
Juba na mto Tana.
Tukiitazama ramani ya
sasa ya Afrika Mashariki mto Juba unapatika kusini ya Somalia unakaribia
mpakani mwa Kenya upande wa kaskazini na Somalia upande wa kusini
(Tazama kielelezo na. 2, uk. 7) wakati mto Tana unapatikana katika nchi
ya Kenya. Ama kuhusu mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia maeneo hayo
yanazungumzwa kwa namna tofauti na wataalamu mbalimbali. Mathalani,
Christopher Eheret anatueleza kuwa kufikia karne ya 7 yawezekana Wabantu
walifika maeneo ya Mto Tana Massamba (2002:80 ). Kwa
maelezo haya ya Eheret ina maana kuwa, mpaka kufikia miaka 600 BK ndiyo
kipindi ambacho wabantu walikuwa wamefika mto tana. (karne ya 7 = miaka
ya 600 BK).
Aidha, Nurse na Spaer
(1985) wanaeleza kuwa hadi kufikia miaka ya 500BK Wabantu walikwisha
fika pwani ya kaskazini katika eneo ambalo leo hii ni mpakani mwa pwani
ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia kusini Massamba (2002:80).
Tukiyachunguza madai haya ya Nurse na Spear bila shaka utaona kuwa,
yanawiana na yale ya Eheret tuliyoangalia hapo awali, wakati Nurse na
Spear wanataja kuwa kati ya mwaka 500 BK. Wabantu walikuwa
wameshatamakani katika pwani ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia
kusini ingawa hawataji hasa ni eneo gani, Eheret anatueleza kuwa ni
karne ya 7 (miaka ya 600 BK) ndiyo Wabantu walikuwa wameshafika eneo la
kaskazini mwa Kenya na anatutajia eneo hilo kuwa ni maeneo ya Mto Tana.
Kwa upande wake,
Gonzales (2008) anaeleza kuwa, kwa kutumia ushahidi wa kiisimu kufikia
karne 4 BK ( sawa na miaka ya 300 BK) Wabantu walishatamakani katika
eneo la pwani ya Afrika Mashariki. Aidha, Jenkins2 anabainisha
kuwa Wabantu wa Afrika Mashariki na Somalia inaelekea walihamia maeneo
hayo wakitokea Afrika ya kati, anaendelea kueleza kuwa wanahistoria
wanakubaliana kuwa Wabantu hao walitamakani eneo la kusini mwa Somalia
pengine miaka ya 200 BK. Pamoja na kwamba wataalamu hawa wanatofautiana
katika miaka wanayotaja Wabantu kutamakani eneo la upwa wa Afrika
Mashariki kimsingi hawa wote wanathibitisha kuwa mpaka kufikia mwaka
800BK na 900BK mjongeo wa Wabantu ulikuwa umeshafika maeneo hayo ya Mto
Juba na Mto Tana.
Hata hivyo, kuna madai
mengine yanayodai kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili (ama waswahili)
ambao kwa asili wataalamu mbalimbali kama vile Wilhem Bleek (1862),
Carl Meinhof (1899), C.M. Doke (1935), Malcom Guthrie (1967,1970,1971),
Dereck Nurse na Thomas Spear, Shihabudin Chiraghdin na Mathias Mnyampala
(1977), Massamba (2002) kwa kuwataja wachache wanakubaliana kuwa,
Kiswahili ni moja wapo ya lugha za Kibantu. Lugha hii inadaiwa kuwa
chimbuko lake ni iliyowahi kuwa himaya ya Shungwaya., Mtetezi wa dai
hili ni James Der ver Allen (1993) (Tazama Massamba 2007:51-55). Dai
hili laelekea pia kuungwa mkono na Mirikau (2013:14) anaeleza kuwa,
baadhi ya Waswahili wametoa maoni yao kwa kusisitiza kwamba Kiswahili
kilianza kusemwa na Wabantu wa zamani walioishi Shungwaya. Kwa hakika
ingawa dai hili linapingwa na wanazuoni wengine kama vile Greenville
(1959) na Massamba kwamba Kiswahili kiliinukia eneo moja mahususi
(Tazama Massamba 2002: 85), na bado mpaka sasa kuna utata ama
kukubaliana au kutokukubaliana miongoni mwa wanazuoni kama himaya hiyo
ilipata kuwepo ama la, Mirikau akijiegemeza katika ushahidi wa fasihi
simulizi anaeleza kuwa, eneo la Shungwaya ilikuwa kati ya Mto Juba
uliopo nchini Somalia na Mto Tana uliopo nchini Kenya.
Massamba (2002:53)
akimnukuu Prins anasema kuwa, Shungwaya ilikuwa himaya kuu ikijumuisha
Wasomali, Wakikuyu, Wameru, Watharaka, Wakamba, Wataita, Wapare,
Wachaga, Washambaa, Wabondei, Wazaramo na Wagara ilichukua eneo lote la
Somalia ya sasa, mashariki ya Kenya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa
Tanzania na inakadiliwa kuwa himaya hii ilipata kuwepo hata kabla ya
mwaka 800 BK. Kutokana na maelezo haya na yale ya Mirikau kuwa eneo la
Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana na madai kuwa, eneo hili
lilipata kuwepo hata kabla ya miaka 800 BK kama anavyodai Prins ni wazi
kuwa wanatuthibitishia kuwa mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia mwaka 800
BK na 900 BK ulikuwa umeshajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana.
Aidha, Shihabuddin Chiraghdin (1974:57) katika makala yake yenye kichwa cha habari Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-“standard Swahili.” ingawa
haelezi wazi ni mwaka gani, lakini anatuambia kuwa chimbuko la
Waswahili (Wabantu) ni huko Ngozini kaskazini ya Kenya pande za visiwa
vya Magunyani inayojumuisha Pate, Faza na Lamu na Tikuu na kushukia
mpaka mipaka ya Mto Tana. Massamba (2002:84) anaafiki kuwa ,kati ya
miaka 400 BK hadi 800 BK upwa wa Mashariki ya Afrika ulikwishakaliwa na
Wabantu na Wakushiti yaani Wasomali na Wagalla. Kwa kuwa Chiraghdin
anaeleza kuwa Waswahili (Wabantu) walianzia Ngozini na kuenea mpaka
mipaka ya Mto Tana ni dhahiri kuwa kwa maelezo yake na tukiyaoainisha na
ya Massamba kuwa, kati ya mwaka 400-800BK Wabantu walikwishatamakani
upwa wa Afrika Mashariki bila shaka kama tutakubaliana na madai kuwa
Wabantu walitokea kusini Somalia na kuteremka mpaka kaskazini ya Kenya,
basi watakuwa pia katika kipindi hicho walikuwa wamejongea maeneo ya
Juba na kufika huko Ngozini hadi Mto Tana.
Ama kwa hakika,
tukiyatalii mawazo ya wanazuoni na wataalamu mbalimbali tuliowaangalia
hapo juu tutaona kwamba ingawa wanatofautiana katika miaka na wengine
kuonekana kutaja miaka ya kufikirika zaidi, ila kimsingi wote wanaelekea
kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Mijongeo ya
Wabantu ilikwashafika maeneo ya Mto Juba na Tana. Hivyo basi, katika
sehemu inayofuata kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848)
kuafiki madai haya.
2.2 Nadharia ya Barker (1848) na Nadharia ya Turton (1975)
Katika sehemu hii
tutatumia nadharia hizi kutetea ama kuafiki madai kuwa mpaka kufikia
mwaka 800 hadi 900BK mijongeo ya Wabantu ilikwishafika na kutamakani
maeneo ya Mto Juba na Mto Tana kama ambavyo wataalamu wengine
wanavyodai. Tukianza na:
2.2.1 Nadharia ya Barker (1848)
Nadharia hii inaeleza
kuwa, kwenye karne ya 10 BK Wasomali ambao wapo katika kundi la
Wakushiti wa Mashariki walianza kuteremka kusini wakitokea katika ncha
ya Kaskazi ya pembe ya Afrika ambako ndipo inapodaiwa kuwa yalikuwa
maskani yao. Inadaiwa kuwa katika kujongea kwao huko kusini waliwakuta
Wagalla ambao walikuwa wakiishi katika maeneo ya kaskazini na kati ya
Somalia ya sasa na kuwafukuza. Nadharia inaendelea kueleza kuwa, Wagalla
nao wakateremka kusini na wakawakuta Wabantu ambao walikuwa
wametamakani katika eneo la Webi Shebelle. Wagalla wakaanza kupambana na
kuwashinda Wabantu wa taifa la Shungwaya ambao wakawasukuma kusini ya
Mto Juba hadi wakafika chini ya Mito Tana na Sabaki Massamba (2002:81)
Ama kwa hakika,
tukiichunguza nadharia hii, tunaona kwamba kuna mambo ya msingi matatu
yanayotufanya kuafikia kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800
BK hadi 900 BK ilikwishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto
Tana. Jambo la kwanza ni kuwa nadharia inataja kuwa, kwenye karne ya
10 BK ndipo Wasomali walipoanza kujongea kusini na kupambana na Wagalla.
Wagalla nao wakazidi kushuka kusini wakakutana na Wabantu ambao nao
walisukumwa kusini ya Mto Juba hadi chini ya Mto Tana na Mto Sabaki.
Kimsingi hapa karne ya 10 inayotajwa hapa ni sawa na miaka 900 BK. Kwa
maana hiyo basi ni dhahiri kuwa kwa nadharia hii na kwa kutumia sababu
hii tunaweza kuafiki kuwa mpaka mwaka 900 BK Wabantu walikuwa
wameshafika maeneo ya Mto Juba na mto Tana kwa kusukumwa na Wagalla
wakitokea eneo la Webi Shebelle. Ingawa pia dai kwamba Wabantu walifika
huko kutokana na kusukumwa na Wagalla ama kwa kushughuli nyingine ni dai
ambalo linatakiwa kutazamwa zaidi kwa jicho la kitafiti kwa maana kuwa
ni dai ambalo linaweza kusailika kutokana na nadharia hii na ile ya
Turton tutakayoenda kuitazama hivi punde kuwa na utata unaosababisha
kujiuliza maswali ni nani hasa alipambana na Wabantu kati ya Wagalla au
Wasomali? Maana nadharia itakayofuata inaeleza tofauti.
Aidha, jambo la pili
tunalolipata katika nadharia hii yanayotusukuma kuafika dai hili ni hoja
inayodai kuwa, Wabantu hao waliosukumwa na Wagalla maskani yao ilikuwa
Webi Shebelle. Tukiangalia ramani ya sasa ya Afrika Mashariki, eneo la
Webi Shebelle linapatikana kusini ya Somalia, yaelekea basi kama madai
haya ni ya kweli, inawezekana Wabantu hao walikuwa wakiishi pembezoni
ama katikati ya Mto Shebelle na Mto Juba. Mto Shebelle unatokea katika
nyanda za juu ya Ethiopia unashuka mpaka maeneo ya pwani ya Somalia na
kukutana na Mto Juba na kuingia bahari ya Hindi. Kama ni hivyo basi kuna
uwezekano mkubwa kuwa Wabantu pengine walikuwa wameshajongea mpaka eneo
la Mto Juba katika karne hiyo ya 10 BK (sawa na miaka ya 900 BK)
pengine hata kabla ya kusukumwa na Wagalla.
Jambo la tatu nadharia
hii inatueleza kuwa, Wabantu walioshambuliwa na kushindwa na Wagalla ni
Wabantu wa Shungwaya pia yanatufanya tuafiki kuwa nadharia hii pia
inakubaliana na dai kuwa Wabantu walijongea mpaka maeneo ya Mto Juba na
Tana katika mwaka 800 BK hadi 900 BK kutokana na eneo la kijiografia
linalotajwa kuwa himaya hiyo ilipata kuwepo. Aidha, Mirikau (keshatajwa)
anaeleza eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana.
Eneo hili linatajwa kuwa lilipata kuwepo hata kabla ya mwaka 800 BK kama
anavyodai Prins (keshatajwa) ni wazi kuwa nadharia hii ya Barker
inatufanya pia kuafiki kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800
BK na 900 BK ilikuwa imeshajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na
Mto Tana kama wanavyodai wataalamu wengine.
2.2.2 Nadharia ya Turton
Tumeangalia nadharia
ya Barker (1848), tumeona kuwa, nadharia inaleza kuwa Wasomali
walipambana na Wagalla. Wagalla wakazidi kuteremka chini (kusini)
wakakutana na Wabantu wakaanza kupambana nao, Wabantu wakaelemewa nao
wakasukuMwa hadi kusini maeneo ya Mto Tana. Je, nadharia ya Turton
(1975:19) inasemaje?
Turton (keshatajwa) katika makala yake aliyoipa jina la Bantu, Galla and Somali Migrations in the Horn of Africa: A Reassessment of the Juba/Tana Area inayopatika katika Jarida la African History anaeleza kuwa, Wasomali Wahawiya na Wa-kabla ya Wahawiya walitokeo maeneo ya karibu na Merka na kuanza kusambaa kuelekea magharibi na kusini na kulikalia karibu eneo lote la kati ya Mto Juba na Mto Tana mapema kabisa kabla hata Wagalla hawajawasili eneo la pwani. Anaendelea kufafanua kwamba, katika hatua hii ya Wasomali wale wa kundi la Wa-kabla ya Wahawiya kujitanua na kuzidi kusambaa kwa kuelekea kusini waliwakuta Wabantu na kuanza kupambana nao kwa ajili ya kugombea maeneo ya malisho. Wasomali (Wa-kabla ya Wahawiya) wakawasukuma Wabantu kurudi nyuma hadi Mto Tana.
Aidha, Turton anaendelea kutueleza kuwa, baadaye kabisa inakadiliwa pengine kwenye karne ya 16 BK (sawa na miaka ya 1500) Wagalla wenyewe walijongea kuelekea pwani wakifuata uelekeo wa Mto Tana ambako huko waliwakuta watu wa Mijikenda na kuwafukuza (Kumbuka Barker anatueleza kuwa Wagalla walishambuliwa na Wasomali). Watu hao wa Mijikenda kulazimika kuelekea kusini hadi kufikia Mto Sabaki kisha Wagalla wakapamba na kuwaondoa Wasomali katika eneo la Juba na Tana na kuwalazimisha zaidi Wasomali kurudi kaskazini. Aidha, tunaelezwa kuwa, katika karne ya 18 BK (sawa na miaka 1700 BK) Wasomali wakaanza tena kusonga chini na kufikia miaka 1860 Wagalla wakawa wamenyang’anywa eneo lote kati ya Mto Juba na Mto Tana walilolikalia zaidi ya miaka 100. Kwa mujibu wa Turton Wabantu hawakwenda sana kaskazini mwa pembe ya Afrika.
Kwa hakika tukiziangalia nadharia hizi mbili kuhusu mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki ni wazi kuwa kuna mambo ambayo wataalamu wa nadharia hizi wanapingana. Mathalani, wakati Barker anatueleza kuwa, Wasomali waliwashambulia Wagalla na Wagalla wakawashumbulia Wabantu kwa upande wake Turton anapingana na Barker, yeye anatueleza kuwa Wasomali tena wale Wa-kabla ya Wahawiya ndiyo waliopambana na Wabantu na wala si Wagalla kama anavyodai Barker.
Tofauti nyingine inayojitokeza ni kuwa, wakati Barker anatueleza kuwa Wagalla waliwasukuma Wabantu kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito ya Tana na Sabaki, Turton inaelekea hakubaliani na hili, kwa upande wake anadai kuwa katika mapambano kati ya Wasomali na Wabantu, Wabantu hawakwenda zaidi kaskazini mwa Pembe ya Afrika na kutokana na hoja hii Massamba (2002:82) anaona kuwa nadharia hii hailekei kueleza kwamba Wabantu walivuka Mto Juba kwenda kaskazini zaidi. Dai ambalo kwa hakika ni kweli, hakuna tunakoelezwa katika nadharia hii kuwa Wabantu walifika Mto Juba. Ingawa hatuelezwi hilo ila wote wanakubaliana kwamba mpaka miaka hiyo mjongeo ulishafika na kutamakani mto Tana. Lakini tukichunguza vizuri ramani ya Afrika Mashariki hususani Somalia na Kenya na kama tunakubaliana kuwa himaya Shungwaya kuu ilichukua eneo la Somalia, Kenya na Kaskazini ya Tanzania basi kuna uwezekani mkubwa Wabantu walishafika hadi Mto Juba.
Ama kwa hakika ingawa nadharia hizi zinapingana katika maeneo tuliyoyataja hapo juu, tukizichunguza kwa makini nadharia hizi zote zinaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Wabantu walikwishajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Hili linathibitishwa na maelezo ya wataalamu wote hawa wawili, ingawa Barker anataja Wabantu walikuwa wamesukumwa kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito Tana na Sabaki, Turton yeye anatueleza kuwa Wasomali waliwalazimisha Wabantu kurudi hadi mto Tana. Kwa maelezo haya ya Turton ni kuwa Wabantu walirudi Mto Tana inaelekea Wabantu walishaanza kuweka maskani maeneo ya Mto Tana na walikuwa wanaelekea Kaskazini ambako ni Somalia kabla ya kukutana na Wasomali. ingawa haelezi wazi kama walifika Mto Juba ila kimsingi wote wanakubaliana kati ya miaka hiyo Wabantu walikuwa washatamakani maeneo ya Mto Tana.
Si hivyo tu, nadharia hizi pia zaelekea kukubaliana kuwa, Wabantu ndiyo watu wa mwanzo kabisa kufika na kutamakani maeneo hayo kuliko Wasomali ama Wagalla na hii inatokana na ukweli kwamba, tunapoelezwa kuwa, Wagalla waliposhuka chini zaidi waliwakuta Wabantu katika taifa la Shungwa ambalo kama tulivyoelezwa na Mirikau (keshatajwa, uk.14) kuwa eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba nchini Somalia na Mto Tana nchini Kenya, ingawa Prins (keshatajwa) anaongezea kuwa eneo la Shungwaya ilichukua eneo lote la Somalia, Kenya na baadhi ya sehemu za kaskazini ya Tanzania.
3 Hitimisho
Kwa hakika, pamoja na kwamba madai ya wataalamu wengi wanakubaliana kuwa hadi kufikia miaka 800BK hadi 900BK mijongeo ya Wabantu na kutamakani kwa Wabantu katika upya wa Afrika Mashariki hususani katika maeneo ya Mto Juba na Mto Tana ilikwishakuwa tayari kuna uwezekano mkubwa pengine Wabantu walishajongea maeneo hayo mapema zaidi kuliko miaka hiyo inayotajwa, tafiti za kiakolojia ingawa zingine hazitaji wazi ni watu wa jamii gani, zinathibitisha kuwa eneo la upwa wa Afrika Mashariki zilianza kukaliwa na watu kuanzia karne ya 3BK. Mathalani Chittick (1975:37) anasema katika maeneo ya unguja Ukuu huko Zanzibar na Manda katika mwambao wa Kenya kulipatikana vifinyange vya zamani sana kati ya vifaa hivyo vimekadiliwa kuwa vilikuwa vya kati ya karne ya tatu hadi karne ya 14 BK Massamba (2002:190).
Aidha, Massamba anatudokeza utafiti mwingine wa kiakolojia majengo yaliyochimbuliwa Manda, inakadiliwa kuwa mji huo ulijengwa karne tatu na karne ya tisa, na mji wa Kilwa ulijengwa kati ya nne na karne kumi au karne ya tano na karne ya kumi na moja ama karne ya sita na karne ya kumi na mbili. Kutokana na ugunduzi wa kiakiolojia uliofanywa na Wanakiolojia mbalimbali, Massamba anahitimisha kwa kusema kuwa wenyeji wa asili walioanzisha makazi katika maeneo ya pwani walikuwa ni Wabantu.
Aidha, hata huu ushahidi wa kiakiolojia nao hauwezi kuwa ushahidi wa moja moja kuhitimisha kwa kusema kuwa Wabantu walianza kulikalia eneo la Afrika Mashariki kuanzia karne ya tatu kwa kutegemea kugunduliwa kwa majengo au vyombo/vifaa vya kale kwani vifaa ama amajengo hayo kwa hakika yalijengwa na wageni ambao walikuwa na teknolojia bora zaidi iliyowawezesha kujenga majengo yanayoweza kudumu muda mrefu tofauti na Wabantu ambao kutokana na teknolojia duni iliyokuwa ikitumika katika ujenzi wa nyumba za kibantu isingewezekana majengo hayo kudumu kwa miaka mingi kama yalivyobainika majengo ya wageni. Lakini tatizo lingine tunadokezwa na Massamba (2002:utangulizi) ni kuwa vyanzo vingi vya kihistoria na vya kiakiolojia vilivyopo vinaanzia karne ya kumi na kuendelea. Kutokana na hali hii tunashindwa kupata data zaidi za nyuma ya hapo na hii ni kwa sababu Wabantu hawakuwa na utamaduni wa kuandika au taaluma hiyo ilikuwa bado kuvumbuliwa. Ushahidi unaotumika wakati mwingine unatokana na masimulizi jambo ambalo linatufanya kupata ugumu hasa kujua, Wabantu walianza kuishi lini Pwani ya Afrika Mashariki. Hivyo suala la wabantu walianza lini hasa kujongea na kutamakani maeneo ya upwa wa Afrika Mashariki ni jambo ambalo bado linasawilika. Hivyo basi utafiti zaidi unahitajika kufanyika ili kupata taarifa sahihi kuhusiana na mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki.
MAREJEO
Chiraghdin, S. (1974) “Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-Standard Swahili.” Katika Mulika.
Na. 6 (1974) uk. 57-60.
Charaghdin, S. Na Mnyampala, M. (1977) Historia ya Kiswahili. Nairobi. University Press.
Collins, R.O. (1968) Problem in African History.
Gonzales,R.M (2008) Society, Religion and History: From Hunter land to Motherland, The Northeast-
Central Culture Zone. Columbia University Press. Iimepakuliwa kutoka
Jenkins, O.B (HM) Race and Ethnicity in The Horn of Africa. Imepakuliwa kutoka
Mapunda, H. (1980) Historia ya Mapambano ya Mtanzania. Dar es Salaam. TPH.
Massamba, D.P.B. (2002) Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi.
The Jomo Kenyatta Foundation.
Massamba, D.P.B. (2007) Kiswahili Origins and The Bantu Divergence-Convergence Theory.
Dar es Salaam. TUKI.
Mrikau, S.a. (2013) Msururu wa PTE Kiswahili. Nairobi. East African Educational Publishers ltd.
Nurse, D. Na Spear, T. (1985) The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African
Society, 800 – 1500. University of Pennsylavania Press.
Turton, E.R. (1975) “Bantu, Galla and Somali Migrations in The Horn of
Africa: A Reassessment of the Juba/Tana Area.” Katika Journal of African History. Vol.16. no. 4 (1975) uk.519-537. Cambridge University Press. Imepakuliwa kutoka