SENTENSI NA AINA ZAKE KISINTAKSIA
SENTENSI NA AINA ZAKE KISINTAKSIA
Kimuundo
sentensi ni tungo yenye kiima na kiarifu na inayotoa taarifa kamili.
Sentensi huweza kugawanywa katika aina kuu tatu ambazo ni:
(i) Sentensi sahili
(ii) Sentensi ambatani
(iii) Sentensi changamani
(i) Sentensi sahili/huru
Hii
ni sentensi yenye kishazi huru kimoja tu. Sentensi sahili huweza kuwa
na KN na KT au KT peke yake. Katika sentensi sahili KT ndio muhimu zaidi
kwani hubeba taarifa muhimu ya sentensi.
Miundo ya sentensi sahili
(i) Muundo wa kirai kitenzi (KT) peke yake.
Mfano:
- Anacheza
- Tumekula
- Wanalima
(ii) Muundo wa kirai nomino na kirai kitenzi (KN + KT)
Mfano:
- Mtoto mdogo anacheza
- Shule yetu imefungwa
(ii) Sentensi ambatani
Hii
ni sentensi inayoundwa kwa sentensi mbili zilizounganishwa kwa
kiunganishi. Sentensi ambatani huweza kuundwa kwa sentensi sahili
mbili,sentensi sahili na changamani au sentensi changamani mbili.
MIUNDO YA SENTENSI AMBATANI
(i) Muundo wa sentensi sahili mbili (vishazi sahili)
Mfano:
- Baba analima na mama anapika
- Watoto wanacheza lakini wazazi wao wamelala
(ii) Miundo yenye kishazi sahili na changamani
Mfano:
- Nyumbu aliyepigwa risasi amekufa na kuzikwa
- Shule inayouzwa imenunuliwa ingawa haijakarabatiwa
(iii) Miundo yenye vishazi changamani pekee
Mfano:
- Ng’ombe aliyezaa amekufa na ndama aliyezaliwa amepotea
- Ubao uliopakwa rangi umekauka na fundi aliyefanya kazi hiyo ameondoka.
(iv) Miundo yenye vishazi visivyokuwa na viunganishi.
Mfano:
- Mwache,aende tu
- Wapeni,waondoke
(iii) Sentensi changamani
Hii ni sentensi inayoundwa kwa kishazi tegemezi kimoja au zaidi na kishazi huru kimoja.
MIUNDO YA SENTENSI CHANGAMANI
1.Miundo yenye kishazi huru na kishazi tegemezi.
Mfano:
- Mwizi aliyekamatwa amefungwa
- Kuku anayetaga amechinjwa
2.Miundo yenye kishazi huru kimoja na kishazi tegemezi zaidi ya kimoja.
Mfano:
- Mvua iliyoangusha mti ulioegemea nyumba imekatika
- Paka aliyekimbilia ndani kulikokuwa na watu ametoka.
KATEGORIA ZA KISARUFI
Neno
kategoria linaukilia kila kundi linalotambulika kisarufi. Kwa mantiki
hii tunaweza kuwa na kategoria za maneno kwa maana ya makundi ya maneno
yanayotambulika kisarufi,mathalan Nomino,vitenzi,vivumishi,vielezi,nk
John Habwe na Peter Karanja (2007) wanaeleza kuwa : Kategoria
za kisarufi ni vipengele vya kisarufi vinavyobainishwa ili vitumike
katika uchambuzi wa kiisimu. Vipengele hivi husaidia kuonesha mahusiano
ya kategoria za maneno katika sentensi. Lengo lake kuu ni kujenga
upatanisho wa sentensi. Kategoria hizi ni kama nafsi,jinsia,idadi na
njeo.
(i) Kategoria nafsi
Nafsi ni kipashio kinachodhihirisha mhusika katika usemaji.
Mfano:
NAFSI
|
Idadi
|
Mifano
|
I
|
Umoja
|
Mimi ninakula
|
Wingi
|
Sisi tunakula
| |
II
|
Umoja
|
Wewe unakula
|
Wingi
|
Nyinyi mnakula
| |
III
|
Umoja
|
Yeye anakula
|
Wingi
|
Wao wanakula
| |
Njeo
ni uhusiano baina ya wakati wa kitendo na wakati wa kusema. Kiswahili
kina njeo tatu ambazo ni njeo iliyopita (-li-), njeo iliyopo (-na-) na
njeo ijayo (-ta-)
Mfano:
Kiambishi Njeo
|
mifano
|
-li-
|
Mtoto alicheza
|
-na-
|
Mtoto anacheza
|
-ta-
|
Mtoto atacheza
|
(iii) Kategoria kauli
Kauli ni umbo la kitenzi linaloonesha uhusiano baina ya kiima na yambwa.
(i) Kauli ya kutenda
Mfano:
- Mary alimpiga mtoto
- Sakina aliandika barua
(ii) Kauli ya kutendewa
Mfano:
- Mtoto alipigwa na Mary
- Barua iliandikwa na Sakina
(iv) Kategoria jinsia/jenda
Hii
ni sifa ya kisarufi inayobainisha hali ya kuwa au kutokuwa kike au
kiume. Kuna aina mbili za jinsia,jinsia ya kisarufi na jinsia ya
kibayolojia. Lugha husemwa kuwa na jinsia ya kisarufi ikiwa maneno yake
yanatiwa katika makundi bila kuzingatia sifa za kibayolojia.
Mfano:Kifaransa, gari dogo linawekwa katika jinsi ya kike na gari kubwa linawekwa katika jinsi ya kiume.
Mfano:
Ending: eur > euse Noun: un danseur (dancer)
- Masculine singular un danseur(me)
- Feminine singular une danseuse(ke)
- Masculine plural des danseurs (me)
- Feminine plural des danseuses (ke)
- Gari kubwa un camion (me)
- Gari dogo une camion (ke)
Lugha ya Kiswahili haidhihirishi mahusiano ya jinsia kiupatanisho bali hutumia nomino zinazorejelea jinsia moja kwa moja.
Mfano:
- Sabina,Omari,mama,baba,mjomba,nk
(v) Kategoria Idadi
Idadi
ni kategoria ya kisarufi yenye kuonesha umoja na wingi katika tungo.
Idadi katika Kiswahili hudhihirika kupitia viambishi ngeli na upatanisho
wake.
Mfano:
- Mtoto analia (umoja)
- Watoto wanalia (wingi)
- Safari ya mbali inafurahisha (umoja)
- Safari za mbali zinafurahisha (wingi)
DHANA YA SINTAKSIA
Sintaksia
ni utanzu wa isimu unaoshughulika na muundo wa sentensi na elementi
nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za
maneno,virai,vishazi,nk
Mambo yahusuyo sintaksia
(i) Sintaksia ni utanzu wa isimu
(ii) Sintaksia ni tawi la sarufi
(iii) Sintaksia inahusu muundo wa sentensi na vipashio vyake
(iv) Muundo wa sentensi hurejelea jinsi vipashio vyake huungana na kuhusiana ili kuunda sentensi yenye maana.
(v) Vipashio muhimu ni maneno,virai na vishazi
(vi) Sintaksia hushughulikia sheria na nadharia za kuundia sentensi na vipashio vyake kama vikundi na vishazi
(vii) Sintaksia pia hushughulikia uhusiano wa taaluma hii na nyingine kama mofolojia na semantiki.
UPEO WA SINTAKSIA
Sintaksia
huhusika na uchambuzi wa sentensi na viambajengo vyake kama virai na
vishazi. Huhusika na uteuzi,uchunguzi na uchambuzi wa mpangilio na
uhusiano wa maneno katika sentensi. Katika kutekeleza haya sintaksia
hujishughulisha na masuala yafuatayo:
(a) Uainishaji wa maneno na viambajengo vingine vya sentensi.
(b) Uchunguzi wa uhusiano wa maneno na vipashio vingine vya sentensi.
(c) Uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi.
(d) Uchambuzi wa miundo ya sentensi.
(e) Uchambuzi wa nadharia na sheria zinazotawala miundo ya sentensi na lugha kwa ujumla.
(f) Kujaribu kuonesha jinsi sintaksia za lugha mbalimbali zinavyoweza kuchangia nadharia ya lugha kwa ujumla.
Kihistoria, sintaksia imepitia awamu tatu ambazo ni: sarufi mapokeo,sarufi miundo na sarufi geuzi.
SARUFI MAPOKEO
Sarufi mapokeo inabeba mawazo ambayo yalianzishwa na vikundi mbalimbali vya wataalamu kama vile wataalamu wa Kiyunani, Kirumi na Kiingereza. Baadhi ya vikundi maarufu ni kikundi cha KristoiKi, Waleksandaria na Wasofisti. Vikundi hivi vilikuwa na wataalamu maarufu kama vile Plato,Aristotle,Dionysius Thrax na Priscian.
Sarufi mapokeo ilijikita katika lugha za ulaya kama vile Kiyunani na Kilatini.
Sifa za lugha hizi zilionekana bora, zikachunguzwa na kutumiwa katika
kuchunguzia lugha nyingine. Lugha zilizokosa sifa zinazoendana na lugha
hizi zilielezwa kuwa lugha duni na hazikutiliwa maanani.
Katika sarufi mapokeo sentensi haikupaswa kuishia na Kihusishi wala kuanza na Kiunganishi.
Sifa kubwa ya sarufi mapokeo ni kueleza kategoria kwa misingi ya maana ya kila kategoria ya sentensi.
Mfano:
- Sentensi ilielezwa kuwa ni tungo yenye maana kamili,kitenzi ni neno linaloashiria kitendo fulani.
Wanamapokeo
ndio waasisi wa dhanna za kiima (k),kiarifu (A),prediketa
(Pr),shamirisho (sh),chagizo (ch),yambwa (y) na yambiwa (yw).
Aina za sentensi kwa mujibu wa wanasarufi mapokeo
Wanasarufi
mapokeo waliainisha sentensi kwa mujibu wa uamilifu (kazi/dhima) ya
kila sentensi. Msingi mkuu wa uainishaji wao ulijiegemeza kwenye taarifa
inayobebwa na sentensi husika. Kwa kigezo hicho wanatambua sentensi
kama;
(i) Sentensi taarifa
Mfano:
- John ametunukiwa zawadi
- Mjomba ameaga dunia
(ii) Sentensi ulizi/swali
Mfano:
- Peter atarudi lini?
- Mama yako anaitwa nani?
- Kitabu chako ni kipi?
(iii) Sentensi agizi/maelekezo
Mfano:
- Lete hiyo kalamu
- Njoo huku chumbani
- Cheza kule uwanjani
(iv) Sentensi masharti/shurutia
Mfano:
- Ukiniona nitakuelekeza
- Angewahi tungeondoka
- Mngalifika mapema mngalimkuta
SARUFI MIUNDO
Nadharia
ya umuundo ilianza mwanzoni mwa karne ya ishirini. Wanaisimu
waliohusishwa na nadharia hii waliongozwa na Ferdinand de Saussure toka
Uswisi. Wengine ni Franz Boaz, Edward Sapir na Leonard Bloomfield.
Sarufi miundo ilikuja kukosoa misingi na taratibu za sarufi mapokeo kama vile:
1.Kueleza
sentensi na vipashio vyake kiuamilifu mf. Sentensi kuwa ni tungo yenye
maana kamili,nomino ni jina linalotaja mtu-mahali au hali. Maelezo haya
yalionekana kukosa vigezo vya kisayansi.
2.Lugha fulani kufikiriwa kuwa ni bora hali lugha zote ni mifumo ya sauti.
3.Kutoangalia mahusiano ya sentensi moja na nyingine.
4.Kutumia maandishi kama data badala ya lugha ya kusemwa.
5.Kupuuza lugha ya kusemwa kama msingi wa lugha asilia.
6.Kuelekeza matumizi ya lugha badala ya kueleza misingi ya lugha.
Wanamuundo
walisisitiza kutazama na kuchunguza lugha kisayansi. Baba wa isimu ya
kisasa Ferdinand de Saussure alishughulika sana na vipengele vitatu
muhimu ambavyo ni:Langage (lugha),Langue (mfumo) na Parole (utendi).
(i) Langage, Langue na Parole;
Saussure aliona lugha za wanadamu zina sifa za kuzitambulisha kama
lugha. Kila mwanadamu ana uwezo wa kusema lugha kwa kutumia ishara.
(i) Langage; ni jumla ya ishara zinazotumiwa na wanadamu,yaani Languembalimbali pamoja na Parole.
(ii) Langue; ni lugha kama inavyojulikana na watumiaji fulani. Langue ina sifa zifuatazo:
Ø Ina sheria za kisarufi
Ø Ni kipengele cha jamii fulani
Ø Ni dhahania
Ø Haibadiliki kutegemea matumizi
Ø Ni mfumo wa ishara
Ø Si tumikizi.
Langue
ni jumla ya sarufi,msamiati, na sheria za utamkaji pamoja na sheria za
uundaji wa maneno. Lugha hii (langue) iliweza kutumiwa na watu binafsi
kama Parole.
Parole; ina ubinafsi wa yule anayeitumia katika hali halisi. Lugha hii hutokana na sheria za jamii za langue. Hii ni lugha tumikizi,lugha hii ina makosa na kwa hiyo kwa mujibu wa Saussure haikufaa kutumiwa kama data.
DHANNA YA SINKRONIA NA DAIKRONIA
Saussure pia aliibua dhanna mbili muhimu katika uchambuzi wa lugha, dhanna hizo ni Sinkronia na Daikronia.
Sinkronia, ni utafiti wa lugha katika kipindi kimoja maalumu na Daikroniani
utafiti wa lugha katika vipindi tofauti. Lugha inapotizamwa katika
vipindi mbalimbali huweza kudhihirisha mabadiliko makubwa ambayo kwa
kiasi kikubwa huathiri matokeo ya uchunguzi huo.
AINA ZA SENTENSI KIMUUNDO
Kimuundo
sentensi ziliainishwa kwa msingi wa umbo lake na sio maana/taarifa.
Sentensi zilizoainishwa ni sentensi sahili,sentensi ambatani na sentensi
changamani.
MKABALA WA SARUFI MIUNDO VIRAI KWA MUJIBU WA NOAM CHOMSKY
Mkabala huu unagawanywa katika makundi kadhaa yafuatayo.
(i) Mtazamo wa sarufi miundo virai wa awali
(a) Mtazamo huu wa awali wa sarufi miundo virai ulitokana na upungufu wa mtazamo wa awali uliokuwa ukijulikana kama sarufi miundo ukomo.
(a) Hii ni sarufi inayozalisha sentensi kuanzia kushoto kwenda kulia hatua kwa hatua hadi kufikia mwisho wa sentensi.
(b) Baadhi waliita sarufi hii kuwa ni ukomo miundo wa mfanyiko wa Markov.
Sarufi hii ilionekana kutoweza kuhimili muundo wowote wa isimu ambao
unajiegemeza katika nadharia ya Markov unaoweza kueleza uwezo alionao
mzungumzaji wa lugha kama Kiingereza au Kiswahili.
Kutokana na udhaifu wa sarufi miundo Chomsky (1957) alianzisha sarufi yenye uwezo wa kufafanua sarufi ya lugha. Chomsky alizingatia yafuatayo:
(a) Kuanza na uwezo wa kidhahania kueleza nadharia ya lugha.
(b) Kuwepo sarufi inayoweza kuzalisha sentensi toka darajia ya juu hadi ya chini.
(c) Kuwepo
seti ya darajia zenye ukomo ambazo zinaundwa katika mazingira
yanayowezesha muundo unaoruhusu darajia ya juu na kila darajia ielekeze
darajia inayofuata chini yake hadi kiwango cha chini kabisa.
Katika
kutekeleza hilo Chomsky alianzisha dhanna ya sarufi miundo virai.
Sarufi hii inazipa umuhimu kanuni zinazozalisha vijenzi mbalimbali
pamoja na uchambuzi wa viambajengo vya tungo.
Mfano:
Chomsky alizingatia muundo wa sentensi kama ifuatavyo:
(b) Hatua ya kwanza ni kuunda kanuni
(i) Mtoto alipiga mpira
v Sentensi KN + KT
v KN N
v N Mtoto,mpira
v KT T + KN
v T alipiga
(Alama ya inamaanisha sentensi isomeke kama/inajitokeza kama/iandikwe kama)
Kwa kanuni hiyo ya muundo virai sentensi hiyo inaweza kunyumbuliwa kama ifuatavyo:
(a) KN + KT
(b) N + KT
(c) N + T + KN
(d) Mtoto + T + KN
(e) Mtoto + alipiga + KN
(f) Mtoto + alipiga + N
(g) Mtoto + alipiga + mpira
Katika
mchoro itaonekana kuwa kanuni ya umuundo inaanzia kiwango cha sentensi
(S) hadi kiwango cha maneno yanyounda sentensi hiyo.
(ii) Mtoto alipiga mpira
Kanuni
hiyo pia inasaidia kuona vifungu ambavyo ni viambajengo na vile ambavyo
si viambajengo ingawa vyote kwa pamoja vinaunda sentensi.
mfano:[alipiga
mpira] inaunda kiambajengo kimoja ambacho kilele chake ni KT, lakini
hatuwezi kuita [mtoto mpira] kuwa ni kiambajengo. Kilele cha neno
[mpira] kabla ya kufikia kilele cha juu kabisa yaani S ni N, KN na KT
wakati [mtoto] kilele chake ni N na KN (ya mwanzo)
kipindi
cha sarufi miundo virai, muambatano wa maneno yanayounda viambajengo
ulitawala sana. Maneno yaliyoonesha kuambatana kiupamoja zaidi kuliko
mengine katika kuunda sentensi, upamoja huo ulioneshwa kwa muundo virai
au mabano mraba.
Mfano:
[Wageni walimaliza chakula chote]
[[Wageni] [[walimaliza] [[chakula]] [chote]]]]
(ii) Hatua ya pili ni kuainisha kategoria mbalimbali za virai kwa kuvipa majina.
Mfano:
- Wageni ni KN na mwisho wake ni N (wageni)
- KT
ni fungu zima la maneno [walimaliza chakula chote]. Ndani ya KT kuna
(T) ambayo ni (walimaliza) na inafuatwa na chakula chote ambayo ni (KN).
KN ina maneno mawili ambayo ni [chakula] (N) na [chote] (v)
Wageni walimaliza chakula chote
(iii) Hatua ya tatu ni kutaja muundo wa kimofolojia katika kiwango cha maneno.
(iii) Binti mdogo alichota maji
[S = Sentensi, kng = kipatanishi ngeli, kpt = kipatanishi cha kisarufi, nj = njeo, mz = mzizi, kt = kiambishi tamati]
(iv) Mtazamo wa sarufi miundo virai wa sasa
Mtazamo
wa sasa wa sarufi miundo virai unazingatia dhanna ya umiliki na usabiki
(utangulia), dhanna ambazo zinatawala mahusiano ya vipashio vya
sentensi.
(a) Dhanna ya umiliki na usabiki:
Dhanna
hizi zinajaribu kujibu maswali matatu ambayo ni maana,muundo na
uzingatizi wa kanuni mbalimbali. Dhanna hizi husaidia kujibu kwa uhakika
maana ya muundo virai, kwa kuzingatia kanuni.
Dhanna ya muundo virai ni kielelezo chenye vifundo vinavyounganishwa na mistari inayounda kielelezo cha matawi.
Kielelezo cha vifundo katika mchoro kinaonesha kuwa vifundo viko katika kila kategoria ya kikundi.
[S,KN,KT,KV,KH]
na kategoria ya neno [N,T,V,H]. Vifundo chini ya S huitwa vifundo mama
na KN na KT huitwa vifundo binti kwa S na pia KN na KT ni vifundo dada.
Kwa
utaratibu huohuo T na KN ni vifundo binti wa KT lakini T na KN ni
vifundo dada. H na N ni vifundo binti wa KH na pia H na N ni vifundo
dada.
Kutokana
na mfano wa hapo juu N,V,N,H,N huitwa vifundo tamati. Vile vingine
ambavyo si vifundo vya mwisho katika kielelezo cha matawi huitwa vifundo
viso-tamati. Vifundo hivi hupewa msamiati unaohusika kwa mfano katika
sentensi nzima [mwalimu mkuu anafundisha darasa la nne]. Kwa kawaida
vifundo viso-tamati huwa ni vile ambavyo ni vifungu yaani kwa mfano
katika mchoro hapo juu [KN1, KT, KN2, KH] ni vifundo viso-tamati. Kifundo kimoja kimoja yaani viso-vifungu kama [N, V, T, N, H, N] ndiyo vifundo tamati.
Pamoja na kupewa majina, vifundo pia huelezewa uhusiano baina yake. Kuna uhusiano wa namna mbili.
- Uhusiano wa umiliki
- Uhusiano wa usabiki
Kumilikiwa
ni dhanna inayoelezea jinsi kifundo kimoja kinavyokuwa chini ya kifundo
kingine. Kifundo cha juu kinamiliki vifundo vya chini yake. Kifundo
kimoja kinasemwa kuwa kiko katika umiliki sawia [umiliki sisisi] kama
kinafuatwa mara moja chini yake [bila kuwepo kifundo kingine kati yake]
mfano: S inamiliki sawia KN na KT.
Kwa mantiki hii umiliki ni wa mama na binti zake. Ingawa S inamiliki pia T na KN (ya pili) kwa mbali.
Ø Uhusiano wa usabiki;
huu ni uhusiano wa ki-utangulia,yaani kifundo kimoja kinasabiki kifundo
kingine ikiwa kinatokea kushoto kwake. Mfano: N inasabiki V na V
inasabiki vifundo T,KN,N,KH,H na N pamoja na maneno [anafundisha darasa
la nne]. Kifundo kinasabiki sawia kifundo kingine ikiwa kinatokea mara
moja kushoto mwa kifundo kingine. Mfano: V inasabiki sawia T na neno
[anafundisha].
Kwa
kutumia dhanna za umiliki na umiliki sawia tunapata istilahi mbili
muhimu ambazo ni viambajengo na viambajengo vifuasi [viambajengo
sisisi]. Dhanna hizi zinafasiliwa ifuatavyo:
(v) Seti
ya vifundo inaweza kuunda kiambajengo iwapo na iwapo tu (iit) seti hiyo
inamilikiwa na fundo moja na hakuna fundo linalosalia.
(vi) Fundo moja x huwa kiambajengo cha fundo lingine y iwapo na iwapo tu fundo hilo linamilikiwa na y.
(vii) X ni kiambajengo sisisi (sawia) cha y iwapo na iwapo tu x inamilikiwa na y.
Mfano:
Kielelezo
hicho kinaonesha kuwa kwa kanuni ya mfuatano [D,E] haziundi kiambajengo
kwa kuwa fundo moja [F] linabaki, lakini mafundo [D,E,F] yanaunda
kiambajengo kimoja kwa kuwa yanamilikiwa kikamilifu na fundo C na hakuna
fundo
linalobaki.
Mfano:
-Majambazi wakatili waliwaua walinzi hodari bila huruma.
T,KN2 na KH vinaunda kiambajengo [waliwaua walinzi hodari bila huruma] kwa kuwa T,KN2 na KH vinamilikiwa na fundo moja KT na hakuna fundo linalosalia. KN2 na KH haviundi kiambajengo ingawa vinamilikiwa na fundo moja [KT] kwa kuwa kuna fundo moja T [waliwaua] linasalia.
S inamiliki viambajengo vyote vilivyo chini yake [KN,KT,N,V,T,KN2,KH,N2,V2,H na N3] KN na KT ndiyo viambajengo sisisi (sawia) vya S kwa kuwa vinamilikiwa moja kwa moja na S. T,KN2 na KH ni viambajengo vya KT.
UFAFANUZI WA DHANNA YA VIFUNDO
Ø Iwapo
kifundo kimoja x kinamilikiwa moja kwa moja na kifundo y basi kifundo y
ni mama wa kifundo x na kifundo x ni binti wa kifundo y.
Ø Seti ya vifundo viwili au zaidi ni vifundo dada iwapo vyote vinamilikiwa moja kwa moja na kifundo kimoja yaani kifundo mama.
Majambazi wakatili waliwaua walinzi hodari bila huruma
v KN1ni kifundo mama wa vifundo N na V1 kwa kuwa vinamilikiwa na kifundo kimoja KN1
v Vifundo N1na V1 ni vifundo dada.
v T, KN2na KH ni dada kwa kuwa vinamilikiwa moja kwa moja na KT.
UMILIKI REJESHI
Dhanna
ya umiliki imeendelea kutumiwa katika kufasili mahusiano ya miundo tata
kati ya viambajengo kwa kuvihusianisha na sintaksia na semantiki.
X
inamilikiwa na kiambajengo y, iwapo na iwapo tu kifundo cha mstari wa
kwanza wa mchoro wa matawi unaomiliki x unamiliki pia y na x haimiliki y
wala y haimiliki x.
Umiliki
rejeshi ni umiliki wa wima na ulalo. Yaani kifundo cha juu kinamiliki
vya chini yake na kifundo kilicho mstari mmoja toka kifundo cha juu
kinamiliki vifundo vyote vya kulia kwake.
AINA ZA UREJESHI
Kuna
aina mbili za urejeshi ambazo ni urejeshi huru na urejeshi uso huru.
Urejeshi huru ni ule ambao unaweza kubainisha kikamilifu kirejelewa na
urejeshi uso huru ni ule ambao hauwezi kubainisha kirejelewa kikamilifu.
Mfano:
Ø Wanafunzi wanafikiri walimu wote wanawachukia
Ø Fatuma na Ali wanajitangaza
Ø Fatuma na Ali wanatangazana
Dhanna
ya urejeshi inayozungumziwa hapa ni tofauti na ile iliyozoeleka, hapa
mofimu –wa-,-ji- na –an- ndizo zinazoonesha urejeshi.
1 Mofimu –wa- inaweza kurejelea kwa wanafunzi au kwa watu wengine,yaani;
v Wanafunzi wanajihisi kuwachukia walimu
v Wanafunzi wanahisi watu wengine wanawachukia walimu
Aina hii ya urejeshi ndiyo inayoitwa urejeshi huru kutokana na uhuru wa kurejelea kitajwa zaidi ya kimoja.
2 Mofimu
–ji- na –an- ni urejeshi uso huru yani unarejelea Fatuma na Ali na
hauwezi kurejelea kitajwa kingine chochote. Urejeshi uso-huru huwa na
kisabiki ambacho kisipokuwepo inakuwa vigumu kufasilika.
Mfano:
* John wanachukia kila mmoja
Ø John na Ali wanachukia kila mmoja
Kila
mmoja inaashiria zaidi ya mtu mmoja na kila mmoja haiwezi kuwa
kirejeshi cha John (ambaye ni mtu mmoja tu). Kwa hiyo kanuni ifuatayo
itatumika.
Umiliki fuatishi lazima uwe na kiambajengo milikishi kisabiki kinachostahili.
|
Katika
dhanna ya umiliki rejeshi,kifundo kimoja kinamiliki vifundo vingine
kushoto na kulia kwake ilimradi viwe katika darajia ileile. Vilevile
kifundo kimoja kinamiliki vifundo vyote vinavyomilikiwa na kifundo cha
kulia kwake ambacho kiko katika kiwango kilekile.
Sarufi geuza maumbo zalishi
Nadharia
ya sarufi geuza maumbo zalishi huonesha ujuzi alionao mzungumzaji ambao
humwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na kikomo. Uwezo wa
mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na kufahamu
kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua
kutokana na kuwa na umilisi na lugha yake. Kanuni za kutunga
sentensi sahihi hubainisha sentensi sahihi na zisizo sahihi. Kwa mujibu
wa nadharia hii, sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza
katika usemaji na hata inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa
limefichika na hujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea
(maana).
Nadharia hii imeweza kuonesha uhusiano wa tungo ambazo japo zilikuwa na umbo la nje tofauti, zina umbo la ndani sawa. Kwa mfano:
a) Juma anacheza mpira
b) Mpira unachezwa na Juma
Mpira unachezwa na Juma
Mfanano
wa tungo hizo umekitwa katika maana. Japokuwa sentensi (a) inaanza na
Juma, na ile ya (b) inaanza na Mpira, mtenda na mtendwa katika sentensi
zote ni yule yule. Mchakato wa kubadili umbo la nje la sentensi (a) na
kuwa (b) umesababisha uchopekaji wa kihusishi ‘na’ na kiambishi tendwa
‘w’ katika kitenzi ‘cheza’.Kanuni geuzi tendwa ndiyo iliyotumika
kuingiza mabadiliko haya. Sentensi yaweza kubadilishwa kutoka umbo moja
hadi jingine.
Kwa mfano:
(c) John anafanya mtihani na Maria anafanya mtihani
(d) John na Maria wanafanya mtihani
Umbo
la nje la tungo hizi ni tofauti lakini umbo la ndani ni sawa. Tungo (d)
imedondosha baadhi ya maneno yaliyo katika (c). Kanuni ya udondoshaji
imetumika kudondosha ‘anafanya mtihani’ ambayo imerudiwa katika sentensi
(c). Kanuni ya kubadilishana viambishi idadi imetumika kubadili idadi
ya mtenda kutoka umoja ‘a- ya ‘anafanya’ iliyotumika kwa John na Maria
kila mmoja peke yake, na kuingiza kiambishi cha wingi: ‘-wa- ya
‘wanafanya.’
Kwa
hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa sintaksia haiwezi
kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kwa kuwa kuna uhusiano wa
moja kwa moja baina ya vipengele vya lugha na kwa hiyo hutegemeana kati
ya kipengele kimoja na kingine. Kwa mfano; huwezi kupata mofolojia
(neno) bila kupitia ngazi ya fonolojia na pia huwezi kuwa na ngazi ya
sintaksia (sentensi/tungo) bila kupitia ngazi ya fonolojia na mofolojia
lakini vitengo vyote hivi hutawaliwa na kitengo cha semantiki ili kuleta
mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji.