Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
15. Hisia Katika Fasihi Andishi
A.J. Saffari
Utangulizi
Makala haya yanazungumzia fasihi andishi ya Kiswahili. Maarubu
yake ni kuonyesha kuwa kazi nyingi za fasihi andishi ya Kiswahili zimeshindwa
kufikia vipeo vya juu, hususan kisanii, kutokana na utovu wa matumizi ya hisia
katika mazingira yanayohusika au kuzungumziwa.
Kwanza, makala yatafafanua maana ya hisia, kuelezea umuhimu na
mkabala wake katika riwaya na tungo nyingine, hatimaye kutoa mapendekezo
mintaarafu ya suala hili.
Hisia Ni Nini
Kuna aina kuu za hisia zinazotawala na kuongoza maisha ya
mwanadamu: kuona, kusikia, kugusa, kuonja na kunusa. Ni vigumu kusema ni hisia
gani muhimu kuzidi nyingine ingawa ni dhahiri athari kubwa humuangukia mahuluku
asiyeweza kuona. Inasemekana kuwa mishipa ya fahamu inayounga ubongo na macho ni
mikubwa zaidi kuliko mishipa ya fahamu inayounga ubongo na viwambo vya masikio.
Na katika maisha na nyendo za kila siku kuona hupewa uzito mkubwa minghairi ya
kusikia. Pengine basi sio ajabu, kama itakavyobainika punde baadaye, kuwa kazi
nyingi za fasihi andishi zimeelemea mno katika hisia hii kana kwamba zile
nyingine kuu hazipo kabisa. Hakika hili ni kosa. Maana kusikia, kugusa, kuonja,
na kunusa nako ndiko humkamilisha mwanadamu aweze kuyafaidi maisha yake. Na hata
mbele ya sheria, ushahidi huweza kutolewa mintaarafu ya kusikia, kugusa, kuonja
na kunusa alimradi shahidi awe amesikia, kugusa, kuonja, au kunusa mwenyewe.
Ushahidi wa kuambiwa haukubaliwi.1
Kwa hiyo basi kazi ya sanaa ambayo itazituma fikira za msomaji
zihisi kuona, kusikia, kuonja, kugusa, na kunusa matendo na mazingira
yanayosimuliwa humpeleka msomaji huyo katika mipaka na nyanja za juu za ufahamu
na furaha.
Umuhhnu wa Hisia
Kila hisia ina umuhimu wake kutokana na mazingira ya tukio
linalohusika au kusimuliwa. Maana kazi zote za sanaa hutokana na matendo na
maisha ya watu ambao katika matukio, visa na mazingira yao hutumia hisia zao
zote tano ama kwa pamoja au kwa nyakati mbalimbali. Ili basi msomaji aweze
kupata mandhari kamili, na hata yeye mwenyewe ashiriki katika matukio yenyewe
kwa kuchukia, kuonea huruma, n.k., muhimu, kabla ya yote, apate hisia zote hizo
tano. Kazi ya sanaa inayojihusisha na hisia moja tu au mbili huwa muflisi
kisanii kwa vile inashindwa kuwasilisha mandhari za hali halisi kwa msomaji. Je,
mara ngapi nyoyo zetu husononeka au kuripukwa kwa maya kwa sababu ya sauti ndogo
tu ya ndege aliaye pekee nyikani, au nyimbo ya zamani? Sauti ya ndege huweza
kuleta majonzi ya miaka mingi mno ya utotoni wakati ambapo mtu alifiwa na mzazi,
ndugu, jamaa au sahibu wake. Kadhalika nyimbo ya kale huweza kuchimbua ashiki ya
zamani baina ya wapenzi, au kutonesha jeraha la masaibu na madhila yaliyopita.
Na wala sio nyimbo na sauti ya ndege tu, pengine hata harufu ya maua huwa na
nguvu za kumbukumbu kubwa mno.2
Licha ya yote hayo, matumizi ya hisia nyingi yanasaidia kujenga
mandhari kamili ya tukio katika akili ya msomaji. Mathalan badala ya kuelezwa tu
kuwa paliandaliwa chakula kizuri, msomaji anaelezwa vitu ambavyo vimeandaliwa
pamoja na harufu yake. Au badala ya kuambiwa mtu fulani alikuwa na wajihi wa
kutisha, huelezwa na kuelewa vyema zaidi kwa kuainishia jinsi pua, macho, rangi,
nywele, mdomo na meno ya mtu huyo yalivyo. Na hivyohivyo kwa mifano mingine
kadha wa kadha kama vile hasira na ucheshi. Kutokana na maelezo ya kutosha ya
hisia msomaji huweza kumuashiki janabi, au akadondokwa na ute kutamani chakula
ambacho hakipo mbele yake. Na kadhalika.
Na sio hivyo tu. Hisia zinazotumiwa huweza kumfanya msomaji
atafakari zaidi. Ataweza kufikia uamuzi kuhusu picha zinazochorwa kutokana na
hisia mbalimbali na wala sio kauli za mkatomkato za mwandishi kama ilivyogusiwa
hapo juu. Kauli za mkatomkato sio tu hudumaza sanaa, bali pia hudhalilisha hata
akili ya msomaji: kwani umbuji wa mwandishi ni pamoja na kufanya matendo na
mazingira anayoyasimulia yawasilishe na kuwakilisha fikira za wahusika wake na
hata zake mwenyewe.
Hivyo ni dhahiri kuwa hisia humsaidia msomaji kuzama katika
matendo na kuelewa fikra za mwandishi mwenyewe, asili na makazi yake, kuwadadisi
na kuwaelewa wahusika wenyewe, n.k.
Kama ambavyo itazingatiwa punde kidogo, ni nadra kuona waandishi
wa kazi za sanaa wakitumia hisia japo tatu au zotc kwa pamoja. Vibaya zaidi ni
kuwa hata pale hisia moja tuinapotumika haielezwi kwa kimowi. Mathalan
katika riwaya' Ukitoa Siri Utachinjwa3 Bedui, mhusika mkuu,
anaelezwa kuwa "alikuwa na umri mkubwa kuliko umri wake."4 Kutokaoa
na maelezo hayo ni muhali kuivuta sura ya Bedui na kuimaizi kiasi cha kutosha.
Bedui haingii machoni na akilini mwa msomaji bali anapitapita mithili ya kivuli
usiku wa manane. Udhaifu huo unajidhihirisha mno kwa kufananisha namna Sembene
Ousmane alivyomsawiri Daouda5 katika The Last of the Empire,
au Alex la Guma anavyomsawiri Michael Adonis katika A Walk in the
Night.6 Mfano mwingine bora ni jinsi Said Mohammed anavyomuelezea
Shoka katika Utengano7 sa Fauz katika Mti
Mkavu.8 Kutokana na undani pamoja na ustadi wa maelezo ya
waandishi hao watatu, wahusika wao hudhihirika bayana machoni mwa msomaji kama
vile wapo ilihali hawapo. Raha iliyoje hii kwa msomaji kupelekewa mke au mume,
mshenzi au muungwana, mnyama au pengine hata maua na harufu yake kwa maneno tu!
Katika mifano yote ya hapo juu hisia iliyotumiwa ni moja tu:
kuona. Tena imetumiwa kuelezea vitu vyenye uhai, hususan watu. Lakini hisia ya
kuona, hali kadhalika, inaweza kutumiwa vyema au vibaya mintaarafu ya vitu
visivyo na uhai kama vile mazingira. Mfano ni namna Alex La Guma anavyoelezea
jinsi mawingu yalivyosonga, kuugonga kisha kuuambaa Mlima wa Meza9 au
vile anavyoupamba usiku;10 au Willieboy anavyofungwa mikononi mwa
askari dhalimu wa Makaburu.11 Katika faala hizohizo Said Mohammed
anafuzu mno kuelezea kasi ya upepo12 na chano cha
maakuli.13
Hisia Katika Riwaya
Ushahidi unathibitisha riwaya nyingi zinajihusisha na aina moja
kuu ya hisia yaani kuona tu, na pengine kusikia.
Kwa kawaida mwandishi huandika anayoyaishi, kuyaona, kuyasikia,
kuyaonja, kuyanusa au kuyahisi katika maisha yake ya dunia.14 Hivyo
ni dhahiri mwandishi ataathiriwa na mazingira ya alipozaliwa, kukua na hata
mastakimu yake. Waandishi waliokulia vijijini aghalabu huwapeleka wahusika wao
vijijini, na wale waliokulia mijini huwapeleka mijini.15 Hata William
Shakespeare aliathiriwa na mambo kama haya.16
Waandishi wa riwaya za Kiswahili wameshindwa kuelezea mazingira
wanayoyajua kwa kutumia hisia zote tano au zaidi. Kitabu Sifi Mara
Mbili,17 mathalan, kinazungumzia maisha na mazingira ya kijijini
Maneromango kabla ya kuhamia mjini. Lakini hakuna tafauti yoyote ya wazi
inayobainisha ushamba na mii katika riwaya hii. Ndivyo ilivyo katika riwaya
nyingine nyingi tu kama vile Ukitoa Siri Utachinjwa,18
Mauaji ya Lojingi,19 kwa kutaja chache tu.
Mwandishi anao uhuru wa kuchagua mandhari na wapi kwa kuwapeleka
wahusika wake. Iwe mjini au mashambani hakuna udhuru wa kutotumia hisia nyingi
au zote tano. Hakika mwandishi wa riwaya ana uwanja mpana zaidi wa kuranda
akitumia silaha kali ya kalamu na maneno. Riwaya ina upana na urefu wa
kumwezesha mwandishi kujifaragua, hasa katika majitapo ya wahusika, nafasi ya
mazingira na urefu wake.20
Kila sehemu ina mazingira yake ambayo kwayo mwandishi anaweza
kuranda na kujifaragua. Shamba kuna mashamba, mjini kuna maghorofa; shamba kuna
mito, mjini kuna mitaro; shamba kuna harufu ya maua, mijini harufu ya uturi,
taka, na kadhalika.
Hisia Katika Tungo
Hapa tungo ina maana ya mashairi na tamthiliya. Kwa bahati
mbaya, kama ilivyo katika riwaya, mashairi mengi yanazungumzia hisia ya kusikia
zaidi na pengine kuona. Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa kazi maarufu kama vile
Sauti ya Dhiki21 na Malenga wa Mvita.22
Mathalan hata yale mashairi mwanana "Jana na Leo na Kesho"23 na
"Zindukani"25 yanaelezea hisia hizo mbili tu: kuona na kusikia.
Hakuna haja ya kutoa mifano ya mashairi mengine mengi katika magazeti ya
Uhuru au Mzalendo ambayo aghalabu si ya viwango vya chini kisanii
tu, bali hata kimaudhui.
Kwa upande mwingine mfano mzuri wa shairi ambalo limesheheni
hisia nyingi ni "Kufua Moyo" la Ustadh Hayati Shaaban Robert ambalo lina hisia
ya kuona, kugusa, na kunusa.26
Ukiondoa Mashetani27 hali nayo ni hivyohivyo
kuhusu tamthiliya. Bali kuna juhudi ambayo inaanza kutoa matunda, ingawa
haieleweki kama jitihada hii ni ya kukusudia au ni ajali tu. Isinyago ni
tamthiliya ambayo inafungua ukurasa mpya mintaarafu ya suala hili la
hisia.28
Hitimisho
Kuna haja kubwa ya waandishi kuzichunguza jamii zao kwa makini,
wapenye katika nafsi za wahusika na mazingira yao ambayo ni muhimu mno ili
kuwaelewa wahusika wenyewe pamoja na kuleta maana na taswira kamili ya mkasa
unaoelezewa.
Maneno ni zana ya pekee inayoweza kumkaribisha au kumtenga
mwandishi na wasomaji wake. Kutokana nayo anaweza kuelezea hisia nyingi ambazo
zitamfanya awe kipenzi, mcheshi na pengine hata mkomhozi wa wasomaji. Sio lazima
hisia zote ziwekwe au kuelezewa pamoja, kwani hivyo ni kushurutisha na ni
kinyume cha mambo. Kinachosisitizwa ni kuwa hisia mbalimbali zionekane katika
kazi nzima kwa jumla ili kuipa ubora na sura ya juu.
Said Mohammed anasema kwamba uandishi ni kazi ngumu, lakini ni
kazi va hiari pia. Ugumu wake ni kama sabaganga, una kazi nyingi ndani ya
moja29. La muhimu ni idili na saburi. Chambilecho Abdilatif Abdallah:
Mambo yataka busara, kinguvunguvu hayendi,
Yatakatuvu fikira, nyot'u sizo na mapindi,
Fikira za kitwa bora, kitwa bupu hakiundi.30
Tanbihi
1. Fungu la 61, "Sheria ya Ushahidi", Na. 6, 1967.
2. C.G. Mung'ong'o, Mirathi ya Hatari. TPH., Dar es
Salaam, uk. 3.
3. J. Simbamwene, (1987) Ukitoa Siri Utachinjwa. Jomssi
Publications, Dar es Salaam.
4. k.h.j., uk. 4.
5. Sembene Ousmane, (1985) The Last ofthe Empire.
Heinemann, uk. 50.
6. A. La Guma, (1968) A Walk in the Night, Heinemann
Educational Books, London, uk. 2:
The young man wore jeans that had been washed several times and which were now left with a paleblue colour flacked with old grease stains and the newer, darker ones of the day's work going white along the hard seams. The jeans had brass buttons and the legs were too long, so that they had to be turned up six inches at the bottom. He also wore an old khaki shirt and over it a rubbed and scuffed and worn leather coat with slanting pockets and woollen wrists. His shoes were of the moccasin type, with leather thongs stitching the saddle to the rest of the uppers. They had been a bright tan once, but now they were a worn dark brown, beginning to crack in the groves across the insteps. The thongs had broken in two places on one shoe and in one place in the other.
7. Mohamed, S. (1980) Utengano, Longman, Nairobi, uk.
110:
Shoka alikuwa barubaru mmoja, fahali wa mtu, kavundumka mwili na kukecha musuli. Mwili wake haukujali suluba au kitisho chochote. Uso wake tinginya. Macho yake ni maboni yaliyojitahidi kutoka kwenye vibofu vyake, lakini hayakufuzu. Meno ya juu yamemng'oka kwa hivyo mdomo wake wa chini umechomoza mbele na ule wa juu umerudi nyuma. Pua yake ni pande la nyama lenye matundu mawili ya ndonya. Nywele zake zimejenga tuta huku na huku, katikati mlima safi unaoteleza. Nyusi nyingi zimetengana na macho. Juu ya urembo huu akapambwa na mbabuko wa mwili, na kwa hivyo rangi yake hapa na pale ilikuwa nyeusi na ya shaba.
8. Mohamed S. (1980) Dunia Mti Mkavu, Longman, Nairobi,
uk. 6:
Kwisha hivyo alimtazama Fumu kwa ushindi na kejeli. 'Ha, ha, ha' alicheka kicheko cha kiburi ambacho kilimwamsha Fumu kutoka jitimai ya kugandwa na jibwa na ule mlio wa bunduki. Alipozindukana, alijikuta amesimama hatua tatu karibu na Fauz. Macho yao yalikutana; ya Fumu yakiwaka moto na Fauz kama pilipili hoho. Fauz alikwaruza meno, ishara ya hamaki. Fumu alimeza fundo la mate; lililoonekana likisukumwa ndani ya umio. Na sasa Fumu alimwona Fauz amesimama kijeuri - miguu yake kaitawanya mmoja huku na mwingine kule bunduki yake imesimamia tako, ameikamatia kwenye mdomo kwa mikono yake miwili aliyoinyoosha. Alipasua kicheko kingine cha jeuri, na Roket, aliyerejea miguuni pake alikuwa akipungapunga mkia.
9. La Guma, m.y., uk. 48:
In the dark a swamp of a cloud struggled along the edges of the Table Mountains, clawed at the rocks for a foothold, was torn away by the breeze that came in from the south east and disappeared.
10. La Guma, k.h.j., uk. 71:
Night crouched over the city. The glow of street lamps and electric signs formed a yellow haze, giving it a pale underbelly that did not reach far enough upwards to absorb the stars that spotted its purple hide. Under it the city was a patchwork of greys, whites and reds threaded with thick ropes of black where the dark'ness held the scattered pattern together. Along the sea front the tall shadows of masts and spars and cranes towered like tangled bones of prehistoric monsters.
11. La Guma, k.h.j., uk. 93 - 94: Hapa hisia tatu: kugusa, kuona
na kusikia, zimetumika kama ifuatavyo:
Delirium was an anaesthetic and he no longer felf pain. But his fingers and hands seemed to have thickened and begun to lose all sense of feeling, so that even when he knew that he moved them over his body they did not seem to touch anything. They were like thick, smaller, lifeless things. Also he had difficulty in seeing the darkness inside the van, and there was highpitched ringing sound running through his brain. He tried to look through the darkness but the power of sight had gone from his eyes. They remained open although he could no longer see. Then his mouth was suddenly full of bile and blood and he tasted the sourness and the salt for an infinitesimal instant before he was dead.
12. S.A.M. Khamisi, (1983) "Hatua Mbalimbali za Kubuni na
Kutunga Riwaya", katika TUKI, Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa
Kiswahili, Juzuu III, Fasihi. Dar es Salaam, uk. 242. Hapa hisia tatu
zimetumika: kusikia, kugusa na kuona:
Upepo upepo ulivuma, ulivuma ukanguruma katika hamsauti wenye kuogofya mithili ya mirindimo ya radi, ulimvaa Sibu ukamkumba, ukataka kumpeperusha, ila alikita kwa uzito, akatia nanga huku akimia kanzu yake iliyokuwa ikipeperushwa isimfedhehi. Mbali kwenye bonde alitupa jicho kwenye uwanda, aliona nyasi zikisukwasukwa.
13. S. Mohamed, (1980) m.y.k., uk. 5.
Ilikuwepo treya moja ya vitoweo - kuku wa kupaka wa mbano, katika sahani yake; kuku wa kuchoma, mwekundu kwa pilipili aliyerembwa nayo, kuku wa makshai aliyekaukia, maini kidogo, yamechemshwa kwa malimau na kurashiwa pilipili manga, mnofu wa samaki wa kukaanga, kamba wa kutokosa na zaidi chatne ya kuchachua kinywa.
14. S.A.M. Khamisi, (1983) m.y.k., uk. 241
15. E. Kezilahabi, (1983) "Utunzi wa Riwaya na Hadithi Fupi",
katika TUKI, Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili, Juzuu
III, Fasihi, Dar es Salaam, uk. 227
16. F.E. Caroline, (1961) Shakespeare's Imagery.
Cambridge University Press, Cambridge.
17. Nico ye Mbajo (1984) Sifi Mara Mbili. Mcheshi
Publications, Dar es Salaam.
18. J. Simbamwene (1987) Ukitoa Siri Utachinjwa. Jomsi
Publications, Dar es Salaam.
19. J. Simbamwene (1987) Mauaji ya Lojingi. Jomsi
Publications, Dar es Salaam
20. Khamisi, (1983) m.y.k., uk 245.
21. A. Abdalla, (1973) Sauti ya Dhiki. Oxford University
Press, Nairobi.
22. A. Nassir, (1974) Malenga wa Mvita. Oxford University
Press, Nairobi
23. Abdalla, (1973) m.y.k., uk. 42.
24. k.h.j., uk. 10.
25. k.h.j., uk. 69.
26. S. Robert, (1968) Kielezo cha Fasili. Nelson,
Nairobi, uk. 48.
27. E. Hussein, (1969) Mashetani. Oxford University
Press, Nairobi.
28. E. Mbogo, Isinyago (Ms), uk. 53; ambapo ametumia
hisia nne za kuona, kunusa, kugusa na kuonja.
Namanduta mwana wa Simbaulanga
Na Singo - mwindaji shujaa
Marafiki wa pete na kidole
Mwayaona maisha haya thakili yaliyokithiri?
Watu hawa wenye uvumilivu uliotendesa
Nchi yao kama ujauzito
Wakulu wao kama watoto wao
Jasho lao kama mbeleko zao
Wakiwabeba migongoni waungwana hao
Kama watoto' wachanga wenye
Vitovu vibichi matumboni. mwao
Wakiwanyea, wakiwakojolea migongoni mwao
Na huku akina nani kajamba wakifyonza
Wakisafisha kwa ustadi mkubwa
Kamasi za waungwana hao
Kwa kutumia ndimi na midomo yao.
29. Khamisi, (1983) m.y.k., uk. 240.
30. Abdalla., (1973) m.y.k., uk.
56.